1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Umoja wa Mataifa waandaa mkutano wa kuisaidia Pakistan

Zainab Aziz
9 Januari 2023

Mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa, ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa na Pakistan, unafanyika Jumatatu tarehe 9 Januari kukusanya fedha za kuisaidia Pakistan baada ya nchi hiyo kukumbwa na mafuriko makubwa.

https://p.dw.com/p/4Ltjn
Schweiz | UN Vereinten Nationen in Genf
Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Mkutano huo ni wa kuisaidia Pakistan kukabiliana na mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha baada ya nchi hiyo kukukumbwa na kiangazi kilichopitiliza. Watu zaidi ya 1,700 walikufa na wengine wapatao milioni 8 waligeuka kuwa wakimbizi wa ndani.

Mkutano huo unawaleta pamoja wawakilishi wa serikali, viongozi kutoka sekta za umma na binafsi, na mashirika ya kiraia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano huo ametoa wito wa uwekezaji mkubwa ili kuisaidia Pakistan kujikwamua kutokana na mafuriko hayo ya mwaka jana, akisema nchi hiyo imeathirika maradufu kwanza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na pili ni kutokana na mfumo wa kifedha wa kimataifa ulioporomoka kimaadili.

Schweiz, Genf | Shehbaz Sharif und Antonio Guterres
Kushoto: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Kulia Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif.Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Guterres aliuambia mkutano wa kimataifa mjini Geneva kwamba hakuna nchi inayostahili kupitia kile watu wa Pakistan walichopitia. Amesema Umoja wa Mataifa unatafuta zaidi ya dola bilioni 16 kutoka kwa wafadhili na misaada mingine kwa nchi hiyo iliyokumbwa na mafuriko ili iweze kufanikisha juhudi za kuijenga upya Pakistan.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amesema nchi yake imepata hasara ya takriban dola bilioni 30 ambazo ni sawa na asilimia 8 ya pato jumla la Pakistan jambo ambalo serikali yake inatafuta uungwaji mkono katika mpango wake endelevu wa kutafuta msaada wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto hiyo iliyosababishwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa.

Tazama:

Mapango yawahifadhi wasio na makaazi Pakistan

Kabla ya kuanza mkutano huo, mkuu wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa, Achim Steiner, aliyaelezea mafuriko hayo kama "janga", na kuongeza kuwa Pakistan itakabiliwa na maafa makubwa ikiwa ulimwengu hautachukua hatua za kuisaidia. Amesema huenda kwa sasa maji yamepungua lakini athari bado zipo na hivyo juhudi kubwa za ujenzi na ukarabati zinahitaji kufanyika.

Mamilioni ya watu wa Pakistan hawana makao na wale ambao wameweza kurudi nyumbani wanafikia kwenye nyumba zilizoharibiwa na mashamba yaliyofunikwa na udongo ambayo hayawezi kupandwa mimea. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa bei za vyakula zimepanda, na idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula imeongezeka maradufu hadi watu milioni 14.6, Benki ya Dunia imekadiria kuwa hadi watu milioni tisa zaidi wanaweza kutumbukia kwenye umaskini kutokana na maafa ya mafuriko nchini Pakistan.

Vyanzo:AFP/RTRE