1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gavana Yemen aanzisha operesheni kukomboa maeneo ya kijeshi

2 Januari 2026

Gavana wa mkoa wa Hadramout wa Yemen anayeungwa mkono na Saudia amesema ataanzisha operesheni ya amani ya kuchukua tena udhibiti wa maeneo ya kijeshi kutoka kwa kundi la wapiganaji linalojiita Baraza la Mpito la Kusini.

https://p.dw.com/p/56E5H
Wanajeshi wa STC wakiwa kwenye mojawapo ya vituo vya ukaguzi katika mji wa Aden nchini Yemen
Gavana wa mkoa wa Hadramout wa Yemen ameanzisha operesheni ya kuchukua tena udhibiti wa maeneo ya kijeshiPicha: AP Photo/picture alliance

Gavana huyo lakini amesisitiza kuwa hatua hiyo si tangazo la vita. Serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia imetangaza kuwa Gavana wa Hadramout Salem Ahmed Saeed al-Khunbashi ndiye ataviongoza vikosi vya "ulinzi wa kitaifa" katika jimbo la mashariki, na kumpa mamlaka kamili ya kijeshi, kiusalama na kiutawala katika kile ilichosema ni hatua ya kurejesha usalama na utulivu eneo hilo.

Hatua hiyo inaashiria ongezeko la hivi karibuni la mvutano nchini Yemen unaoshuhudiwa kati ya mataifa ya Ghuba yenye nguvu na ushawishi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo yanaziunga mkono pande pinzani, mvutano ambao umekuwa ukishika kasi tangu Desemba mwaka jana. Umoja wa Falme za Kiarabu unawaunga mkono wapiganaji wa STC, ambao mwezi uliopita walifanikiwa kuchukua udhibiti wa maeneo makubwa ya kusini mwa Yemen ambayo awali yalikuwa mikononi mwa serikali inayotambuliwa kimataifa, inayoungwa mkono na Saudi Arabia, ambayo inaichukulia hatua hiyo kama tishio kubwa la kiusalama. Wiki iliyopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulitangaza kuviondoa vikosi vyake vilivyosalia nchini Yemen baada ya Saudi Arabia kuunga mkono wito wa vikosi vyake kuondoka ndani ya saa 24.