FIFA yaisimamisha Mali soka la kimataifa | Michezo | DW | 17.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

FIFA yaisimamisha Mali soka la kimataifa

Shirikisho la soka duniani, FIFA limeisimamisha timu ya Mali na maafisa wake kushiriki kwenye michuano ya kimataifa kutokana na hatua ya serikali kuingilia uendeshwaji wa shirikisho hilo

Hata hivyo programu ya Mali kushiriki michuano ya kufuzu kombe la dunia haitaathirika kwa wakati huu. Mechi yake inayofuata itachezwa August 28 nchini Morocco. Timu zote za Mali zilikwishaondolewa kwenye michuano ya kombe la klabu bingwa Afrika, ya mwaka 2017.

FIFA limesema imefikia maamuzi hayo baada ya waziri wa michezo wa Mali kuamua kuivunja kamati tendaji ya shirikisho la kitaifa la soka la Mali.

Sheria za FIFA zinalinda uhuru wa maafisa wa soka waliochaguliwa kutoingiliwa na wanasiasa. Shirikisho hilo litaondoa kikwazo hicho cha kusimamishwa kwa Mali, iwapo uamuzi huo wa waziri utafutwa na kamati hiyo tendaji chini ya Rais wake Boubacar baba Diarra kurejeshwa.

Mali imesimishwa ikiwa ni siku moja baada ya kushiriki kupiga kura kwenye uchaguzi wa rais wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF. Ahmad Ahmad alifanikiwa kushinda kwenye uchaguzi huo na kumuangusha kigogo Issa Hayatou wa Cameroon.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Ssessanga Idd