EURO 2008 yaingia robo fainali | Michezo | DW | 19.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

EURO 2008 yaingia robo fainali

Ujerumani na Ureno uwanjani kwanza

default

Moja wa viwanja vya soka nchini Uswisi ambapo mechi za EURO 2008 zinachezwa

Mashindano ya soka ya mwaka huu ya kuwania ubingwa wa Ulaya leo alhamisi ndio yameingia awamu nyingine ya robo fainali.Ujerumani ndio inaingia uwanjani dhidi ya Ureno.

Mashindano haya yameingia katika awamu ngumu ambayo ni duru ya kutoana.Awamu hii inazijumulisha timu nane ambazo ni Italy,Croatia,Uturuki,Uhispania ,Uholanzi ,Ureno na Ujerumani.

Ujerumani ndio inaaza kibarua hicho ikipambana dhidi ya Ureno na ngoma inachezwa katika mji wa Basle.

Ujerumani iliwahi kutwaa kombe hili kwa mara tatu,lakini mambo hayajajiendea vizuri kama ilivyotarajiwa licha ya kufikia awamu hii.

Wengi wanasema kuwa isipochunga inaweza ikalala mbele ya Ureno ambayo imeonyesha mchezo wa kuvutia katika awamu ya mwanzo ambayo ilimalizika rasmi jana,wakati Urusi ilipoilaza Sweden 2 kwa 0 katika kundi D.

Matokeo ya jana yaliifanya Urusi kufuzu kwa awamu ya robo fainali na inasubiri kukutana na Uholanzi siku ya jumamosi.

Kufuzu kwa Urusi ndio kumekuwa kwa mwisho kwa awamu hiyo, hii ikimaanisha kuwa zilizobaki zimefungasha virago.

Miongoni mwa timu hizo ni bingwa mtetezi Ugiriki,Ufaransa ambayo ilicheza fainali za kombe la dunia na wenyeji wa mashindano haya Austria pamoja na Uswisi.

Ikiwa inasubiriwa kuanza kwa awamu ya robo fainali leo,si vibaya kujikumbusha machache yaliyotokea katika awamu ya kwanza iliyojumulisha mech 16.

Mfungaji bora alikuwa David Villa wa Uhispania ambae aliweza kutingisha nyavu mara nne.

Timu iliofunga mabao mengi zaidi ya nyingine ni Uholanzi ambayo imeweka kwapani mabao 9. Timu ambazo zimefunga mabao machache ni timu tano:mwenyeji Austria,Poland, Romania,Ufaransa na Ugiriki.Kila moja ilifunga bao moja tu.

Timu ambazo zilifungwa mabao mengi ni Ufaransa pamoja na Jamhuri ya Czech.Kila moja ilibugia mabao sita.

Croatia na Uholanzi ndio timu pekee ambazo zilifungwa mabao machace kuliko zote.Kila moja ilifungwa bao moja tu.

Timu ambayo ilikuwa na makona mengi katika awamu hiyo ilikuwa ni Urusi yalifikia 27,na timu iliopata makona machache ni Uholanzi.Yalikuwa 7tu.

Timu ya Uturuki ndio timu pekee iliopata kadi nyingi za njano.Ilipata kadi 10 kwa ujumla. Uholanzi ilipata kadi za njano mbili tu.

Kadi zote za njano zilizotolewa katika wamu hiyo ya mwanzo zilikuwa 95.

Kadi nyekundu zilikuwa tatu na walipewa wachezaji Volkan Demirel wa Uturuki huyu ni mlinda lango,Bastian Schweinsteigner wa Ujerumani na mwisho alikuwa Eric Abidal wa Ufaransa.

Sasa inasubiriwa awamu ya robo fainali tuone itakuwa je.

 • Tarehe 19.06.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EMpc
 • Tarehe 19.06.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EMpc
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com