1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroEthiopia

Ethiopia yasema msaada umetumwa Tigray , TPLF yakanusha

Saleh Mwanamilongo
11 Novemba 2022

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa asilimia sabini ya eneo la kaskazini lililokumbwa na vita la Tigray sasa liko chini ya udhibiti wa jeshi la serikali na kwamba msaada unatumwa jimboni huko.

https://p.dw.com/p/4JNLt
Misaada ya kibinadamu yahitajika jimboni Tigray
Misaada ya kibinadamu yahitajika jimboni TigrayPicha: Joerg Boethling/IMAGO

Redwan Hussein, mshauri wa usalama wa kitaifa wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ametangaza kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa asilimia sabini ya jimbo la Tigray iko chini ya vikosi vya jeshi la serikali.

Amesema misaada inatiririka kuliko wakati wowote mwingine, akiongeza kuwa malori yanayobeba chakula na dawa yamepelekwa katika mji wa kimkakati wa Shire na kwamba safari za ndege ziliruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Kurejeshwa kwa msaada katika eneo hilo lenye watu wapatao milioni sita ni moja ya nguzo muhimu za makubaliano ya amani kati ya serikali ya shirikisho na Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray,TPLF,ili kumaliza miaka miwili ya vita vya kikatili kaskazini mwa Ethiopia. Lakini waasi walikanusha madai ya serikali ya Ethiopia. Msemaji wa chama cha TPLF, Getachew Reda ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali imeficha ukweli wa mambo. Hakukuwa na duru zisisopendelea upande wowote ilikuthibitisha madai hayo, kwa sababu eneo la Tigray bado haliwezi kufikiwa na waandishi wa habari.

Mito ya upelekaji misaada Tigray

Wawakilishi wa serikali na chama cha TPLF waendelea na mazungumzo Nairobi
Wawakilishi wa serikali na chama cha TPLF waendelea na mazungumzo NairobiPicha: Themba Hadebe/AP/picture alliance

Madai ya afisa wa serikali ya Ethiopia kuhusu kupelekwa misaada huko Tigray pia yalikanushwa na mfanyakazi wa kibinadamu aliyeishi huko. Mfanyakazi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe aliliambia shirika la habari la AFP kuwa alichoandika mshauri wa waziri mkuu Abiy Ahmed ni uongo mtupu  na kuongeza kwamba hakuna msaada unaoruhusiwa kuingia katika mji wa Shire hata kidogo.

Eneo la kaskazini mwa Ethiopia linakabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinadamu kutokana na ukosefu wa chakula na dawa, na upatikanaji mdogo wa huduma za kimsingi zikiwemo umeme, benki na mawasiliano.

Siku ya Jumatano, Shirika la Afya Ulimwenguni lilitoa wito wa kuingizwa kwa wingi kwa chakula na dawa huko Tigray kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano, likisema msaada unaohitajika sana bado haujaruhusiwa.

Ramani ya usitishwaji mapigano

Mazungumzo yamekuwa yakiendelea katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi,wiki hii kati ya wawakilishi wa pande zinazozozana kufuatilia makubaliano ya amani yaliotiwa saini wiki mbili iliopita mjini Pretoria, Afrika ya kusini.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujadili kupokonywa silaha kwa waasi, wakati Umoja wa Afrika, mpatanishi wa mazungumzo hayo, ukisema pande husika zinapaswa kutoa ramani ya usitishwaji haraka mapigano na kurejesha huduma za kibinadamu huko Tigray.