Ethiopia: Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele washambuliwa vikali | Matukio ya Afrika | DW | 28.11.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ethiopia

Ethiopia: Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele washambuliwa vikali

Majeshi ya serikali kuu ya Ethiopia yameanza operesheni ya kuuteka mji mkuu wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo. Serikali ya jimbo la Tigray imesema mji mkuu wa Mekele umeshambuliwa vikali kwa mizinga.

Kiongozi wa Tigray Debretsion Gebremichael ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mji wa Mekelle unashambuliwa vikali kwa mizinga.

Katika tamko lake serikali ya jimbo la Tigray limetoa wito kwa wote wenye dhamira ya kweli, ikiwa  pamoja na jumuya ya kimataifa kulaani mashambulio ya mizinga na ya ndege pamoja na mauaji ya halaiki  yanayofanyika.

Soma Zaidi:Jeshi la Ethiopia katika 'hatua ya mwisho' ya mashambulizi Tigray

Mwanadiplomasia mmoja aliyewasiliana moja kwa moja na wakaazi wa mji huo pamoja na kiongozi wa jeshi la jimbo la Tigray amesema hayo. Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo milipuko ilisikika kaskazini mwa mji wa Mekelle. Mwanadiplomasia mwingine amethibitisha kuwa majeshi ya serikali kuu yameanza kuushambulia mji wa Mekelle.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Msemaji wa waziri mkuu wa Ethiopia amesema majeshi ya serikali kuu hayakupewa jukumu la kuupiga mabomu mji wa Mekelle na wakaazi wake. Msemaji huyo Billene Seyoum ameeleza kuwa Mekelle ni mji muhimu wa Ethiopia na kwamba juhudi za kuwafikisha wahalifu wachache mbele ya sheria hazitamaanisha kuupiga mabomu mji huo kiholela kama inavyodawiwa na viongozi wa jeshi la Tigray la TPLF na waendesha propaganda wao. Msemaji huyo amehakikisha kwamba usalama wa wananchi wa Ethiopia katika mji wa Mekelle na katika jimbo lote la Tigray utaendelea kupewa kipaumbele na serikali kuu ya Ethiopia.

Taarifa zinafahamisha kuwa ni vigumu kuthibitisha madai yanayotolewa na kila upande kutokana na mawasiliano ya intaneti katika jimbo la Tigray kukatwa tangu kuanza kwa mapigano wiki tatu zilizopita.

Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele

Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele

Serikali kuu ya mjini Addis Ababa iliwapa viongozi wa jeshi la TPLf wa jimbo la Tigray muda wa siku

tatu kuweka silaha chini na kusalimu amri la sivyo mji mkuu wa Mekelle wenye watu nusu milioni utashambuliwa. Muda huo ulimalizika Jumatano iliyopita.

Siku ya Ijumaa,  waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliwaambia wajumbe wa Umoja wa Afrika kwamba serikali yake itawalinda raia wa jimbo la Tigray lakini aliwaambia wajumbe hao kwamba mgogoro wa Tigray ni suala la ndani ya Ethiopia na mpaka sasa amepinga juhudi zote za kuleta usuluhishi.

Soma Zaidi:Jeshi la Ethiopia linasonga mbele katika mji mkuu wa Tigray, Makele

Majeshi ya serikali kuu ya Ethiopia yamekuwa yapambana na jeshi la jimbo hilo la kaskazini la Tigray linalopakana na Eritrea na Sudan. Waziri mkuu Abiy Ahmed amewalaumu viongozi wa Tigray kwa kuanzisha vita baada ya kuishambulia kambi ya jeshi la serikali kuu iliyoko kwenye jimbo hilo.

Viongozi wa Tigray wamejibu kwa kusema kwamba mashambulio hayo yalikuwa ya kujihami. Kwa mujibu wa taarifa, maalfu ya watu wameuawa na wengine 43,000 wamekimbilia nchi jirani ya Sudan. Wakati huohuo serikali ya Ethiopia imeandika barua kwa waambata wa kijeshi wa nchi za nje kuwaonya kuwa

watakuwamo katika hatari ya kufukuzwa nchini ikiwa watawasiliana na maadui wa Ethiopia wasiojulikana.

Vyanzo: AFP/RTRE