Dortmund waacha pointi muhimu Italia
17 Septemba 2025
Dortmund walikuwa wanafikiria kuwa wataondoka Italia na pointi zote tatu baada ya Yan Couto kuwapa uongozi kwa mara ya tatu kwenye mechi hiyo katika dakika ya 74 na Ramy Bensebaini kufunga mkwaju wa penalti wa dakika ya 86 na kuwapa uongozi wa 4-2.
Lakini Dusan Vlahovic aliwafungia Juve bao la tatu katika dakika ya nne ya muda wa ziada na Lloyd Kelly akasawazisha katika dakika ya mwisho kwenye mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa iliyoshuhudia mabao yote kufungwa katika kipindi cha pili.
"Nafikiri hatukuwa watulivu katika dakika za mwisho. Ni uchungu kupoteza kile tulichodhania kuwa ni ushindi wa moja kwa moja," alisema Sebastian Kehl, mkurugenzi wa michezo wa Dortmund.
Mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa ya Dortmund itakuwa nyumbani Signal Iduna Park dhidi ya Athletic Bilbao ambao walifungwa 2-0 na Arsenal huko nchini Uhispania Jumanne.