Dimba la CHAN kung′oa nanga Rwanda | Michezo | DW | 15.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Dimba la CHAN kung'oa nanga Rwanda

Awamu ya nne ya dimba la kipekee la kandanda barani Afrika limeng'oa nanga leo nchini Rwanda huku Nigeria na Tunisia zikiwa miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kuponyoka na taji

Ni wanasoka wanaocheza katika ligi za barani Afrika ndio wanaoruhusiwa kushiriki katika dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika – CHAN, ambalo michuano yake inatambuliwa na FIFA kama mechi za kimataifa huku matokeo yakichangia katika orodha ya viwango vya FIFA inayofanywa kila mwezi.

Ikiwa ni wazo la rais wa Shirikisho la Kandanda la Afrika – CAF ambaye ni kaimu rais wa FIFA Issa Hayatou, dimba la CHAN lilizinduliwa ili kuwapa nyota wa ndani ya nchi uzoefu wa kandanda la kitaifa ambao kawaida hawawezi kuupata kwa urahisi kwa sababu ya kupewa nafasi wenzao wanaocheza katika ligi za ng'ambo.

CHAN ina muundo sawa na ule wa AFCON ambapo timu 15 zinazofuzu pamoja na mwenyeji hupangwa katika makundi manne ambayo washindi na nambari mbili hutinga robo fainali. Tunisia na Nigeria ziko katika Kundi C pamoja na Niger na wageni Guinea. Kundi A lina wenyeji Rwanda, Gabon, Cote d'Ivoire na Morocco.

Washindi wa awamu ya kwanza ya CHAN miaka saba iliyopita mjini Abidjan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wako katika Kundi B pamoja na Cameroon, Angola na Ethiopia. Kundi D lina Mali, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Mwandishi: Bruce AmaniAFP
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com