1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chissano aitolea wito IEBC

MjahidA26 Februari 2013

Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika, Joaquim Chissano ameishauri Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa wa huru na haki.

https://p.dw.com/p/17lsS
Kiongozi wa Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika Joachim Chisano
Kiongozi wa Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika Joachim ChisanoPicha: DW

Chissano ambaye pia ni rais wa zamani wa Msumbiji ameyasema hayo leo mjini Nairobi katika mkutano wake na waandishi habari, baada ya kukutana na maafisa wa serikali, makundi ya kijamii na IEBC.

Akizungumza na waandishi habari baada ya kukutana na makundi hayo pamoja na viongozi wa vyama vya kisiasa, na kidini, Chissano alitoa wito kwa tume ya uchaguzi nchini Kenya kuhakikisha inashirikiana na taasisi nyingine muhimu ili kuhakikisha uchaguzi wa Machi 4 unafanyika kwa njia ya amani.

Kwa upande wake mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka, Isaack Hassan, ametoa hakikisho kuwa maafisa wake tayari wamejipanga kukabiliana na uvunjaji wa kanuni zozote za uchaguzi. Chissano ameandamana na mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja huo, Dk. Aisha Abdullahi, ambaye atakuwa msaidizi wake kwenye shuhuli hiyo ya uangalizi wa uchaguzi mkuu nchini Kenya utakaofanyika siku ya jumatatu wiki ijayo.

Joachim Chisano na Dr. Aisha Abdullahi
Joachim Chisano na Dr. Aisha AbdullahiPicha: DW

Umoja wa Afrika una ujumbe wa waangalizi 60 ambao baadhi yao ni waangalizi wa muda mrefu waliowasili Kenya tarehe 12 mwezi Januari.

Ujumbe huo wa waangalizi unatoka mashirika mbalimbali ya mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika likiwemo bunge la umoja huo, jumuiya za kiuchumi barani Afrika na mashirika ya kijamii.

Waangalizi hao kutoka Umoja wa Afrika wanaujiunga na waangalizi wengine 36 kutoka Umoja wa Ulaya na wengine 40 kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki waliowasili mwanzoni mwa mwezi huu.

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Josephat Charo