China yakumbwa na tetemeko la ardhi | Masuala ya Jamii | DW | 20.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

China yakumbwa na tetemeko la ardhi

Mamia ya watu wanahofiwa kuuawa au kujeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi leo nchini China karibu na mji wa Ya'an kusini-magharibi mwa jimbo la Sichuan.

Tetemeko la ardhi lililotokea China 2008

Tetemeko la ardhi lililotokea China 2008

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.6 kwenye kipimo cha Richter, na ambalo kiini chake kilikuwa umbali wa km 13 chini ya ardhi limetokea mapema leo asubuhi katika eneo la Lushan, karibu na eneo lilipotokea tetemeko jingine mwaka 2008 na kuwaua zaidi ya watu 85,000.

Awali idara ya tetemeko la ardhi ya China, ilitangaza kuwa tetemeko hilo la ardhi lilikuwa na ukubwa wa 7.0 kwenye kipimo cha Richter, lakini idara ya utafiti wa jiolojia ya Marekani ikaweka sawa kipimo hicho na kutangaza kuwa ni cha 6.6.

Shirika la habari la China-Xinhua, limethibitisha kuwa watu 20 wamekufa hadi sasa na wengine zaidi ya 400 wamejeruhiwa, wanne kati yao wakiwa katika hali mbaya, huku taarifa zikieleza kuwa idadi hiyo inaweza ikaongezeka.

Matetemeko yalisikika katika mji wa Chongping eneo wanapoishi kiasi watu milioni 30. Xinhua imeonyesha picha za wakaazi hao wakiwa nje za nyumba zao baada kusikia mitikisiko.

Nyumba zilizoharibiwa na tetemeko la 2008, Sichuan

Nyumba zilizoharibiwa na tetemeko la 2008, Sichuan, China

Likimnukuu mkaazi wa Chengdu, Xinhua, limesema kuwa mkaazi huyo aliona mitikisiko kwa sekunde 20 na baada ya hapo aliona kuta za nyumba ya jirani zikaanza kubomoka.

Wanajeshi wapelekwa kutoa msaada

Kwa mujibu wa Xinhua, kiasi wanajeshi 2,000 wamepelekwa katika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada katika zoezi la uokozi. Ofisi ya majanga na tetemeko la ardhi ya Sichuan, imesema kuwa miji kadhaa imelisikia tetemeko hilo, ambalo limetikisa sana majengo ya mji mkuu wa jimbo hilo, Chengdu.

Uwanja wa ndege ulifungwa kutokana na tetemeko hilo, kabla ya kufunguliwa tena saa moja baadaye. Timu mbalimbali za uokozi zimeelekea katika eneo hilo la Chengdu kwa ajili ya kutoa msaada na taarifa zinaeleza kuwa Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao ameelekea pia katika eneo la tukio.

Wakaazi wa eneo hilo wanaotumia mitandao ya kijamii, wamesema kuwa tetemeko hilo limekata huduma za umeme na maji. Mwaka 2008 eneo hilo lilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.9 katika kipimo cha Richter na kusababisha vifo vya watu 90,000, kujeruhiwa maelfu pamoja na kufanya uharibifu mkubwa wa mali katika eneo hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE
Mhariri: Daniel Gakuba

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com