Idadi ya wahanga wa tetemeko la ardhi la China yaongezeka | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Idadi ya wahanga wa tetemeko la ardhi la China yaongezeka

Takriban watu 20,000 wanategemewa kufa na wengine zaidi kunaswa katika vifusi

Picha iliotolewa na shirika la habari la China la Xinhua,yaonyesha magari yakiwa yamezikwa na vifusi baada ya nyumba kadhaa kuharibiwa na tetemeko la ardhi.Juhudi za uokozi zinaendelea.

Picha iliotolewa na shirika la habari la China la Xinhua,yaonyesha magari yakiwa yamezikwa na vifusi baada ya nyumba kadhaa kuharibiwa na tetemeko la ardhi.Juhudi za uokozi zinaendelea.

Idadi ya waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi nchini China imepanda hadi 20,000 baada ya waokoaji kufanikiwa kufika katika mkoa wa kusini magharibi wa Sichuan ambao uliharibiwa sana na tetemeko hilo.

Wanajeshi wa China wanaendelea na kuwatafuta walionusurika baada ya miji kadhaa kuharibiwa vibaya.

Juhudi za uokozi zimepamba moto baada ya wanajeshi pamoja na polisi kujipenyeza katika sehemu ya katikati kulikea janga hilo.Helkopta za kijeshi zinadondosha chakula na dawa katika eneo lililokumbwa na tetemeko.

Wanajeshi 100 walilazimishwa kutua kwa miavuli katika maeneo yaliyoathirika kufuatia barabara za huko kuzibwa na maporomoko ya udongo. Tetemeko hilo ambalo lilitokea jumatatu lilikuwa na nguvu za 7.9 katika kipimo cha Ritcher.

Taarifa zaidi kutoka eneo hilo lenye milima zinaeleza kama miji kadhaa iliharibiwa vibaya kiasi cha miji fulani kubaki bila hata na nyumba moja ikiwa imesimama.Takriban watu zaidi ya elf saba inasemekana walifariki katika mji mmoja unaoitwa Ying xiu unakadiriwa kuwa na wakazi 10,000(elf 10).Afisa mmoja wa serikali huko amenukuliwa kusema kuwa ni watu 2,300 ndio wamenusurika.

Katika maeneo mengine ya mkoa huo watu maelefu kadhaa baado hawajulikani waliko,aidha wengine wamefukiwa na vifusi vya majengo kama vile nyumba,shule na viwanda.

Shughuli za uokozi zikiwa zinaendelea msichana mmoja mwenye umri wa miaka mitatu ameokolewa leo baada ya kukaa zaidi ya saa 40 chini ya vifusi vya jengo lilobomoka.

Lakini kisa hicho mbali na kufurahisha lakini pia kinasikitisha .Shirika la habari la Xinhua limearifu kuwa msichana huyo alisalimika kutokana na kufunikwa na miili ya wazazi wake ambao walifariki jumatatu wakati tetemekeo hilo lilipotokea.

Ingawa waokoaji walimpata jumanne lakini hawakuweza kumtoa chini ya vifusi haraka.Wakati shughuli za kumuokoa zilipokuwa zinaendelea waokoaji waliendelea kumpa chakula,na maziwa na pia kumkinga dhidi ya mvua ambayo ilikuwa ikinyesha huku juhudi za kutoa vifusi zikiendelea.

Mvua kali nayo imetatiza juhudi za uokozi hususan siku ya jumatatu, na idara ya utabiri wa hali ya hewa inasema kuwa huenda mvua ikaendelea kunyesha kwa mda wa wiki nzima na hiyo kuzusha hofu nyingine ya uwezekano wa kutokea maporomoko mengine ya ardhi.

Hayo yakiendelea ,shughuli za mbio za mwenge wa michezo ya olimipiki zinaendelea. Awamu ya leo jumatano katika mkoa wa mashariki ilianza kwa kunyamaza kidogo ili kuwakumbuka wahanga wa tetemeko hilo.

Mataifa kadhaa ya nje mkiwemo Marekani,Umoja wa Ulaya,Umoja w mataifa pamoja na kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki imeahidi kutoa msaada kusaidia wahanga.

Ingawa China imekaribisha ahadi za kupewa msaada lakini imesema wakati baado muafaka kwa misaada ya kigeni ikitoa hoja kuwa haiwezi kuwaruhusu sasa watoaji msada wa kigeni kutokana na kuharibika kwa miundo mbinu.

Afisa wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Japan anaehusika na msaada wa dharura amesema kuwa serikali yake imeahidi kutoa kikosi cha uokozi kikiwa na mbwa,lakini China haijaomba msaada kama huo.

Mafundi wa Australia na Korea kusini nao wamekataliwa kiungwana japo China imekubali msaada kutoka Korea Kusini wa thamani ya dola millioni moja.

Juhudi za uokozi zinaendelea.

 • Tarehe 14.05.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DzlE
 • Tarehe 14.05.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DzlE
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com