1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaidhinisha makambi ya kuwazuilia jamii ya Uighur

Lilian Mtono
11 Oktoba 2018

Serikali ya mkoa wa Xinjiang nchini China imehalalisha uwepo wa makambi ya kuwazuwilia watu wa jamii ya Waislamu walio wachache. Takribani Waislamu milioni 1 wanakadiriwa kushikiliwa kwenye makambi kama hayo. 

https://p.dw.com/p/36L4H
China Ethnie der Uiguren
Picha: picture-alliance/dpa/D. Azubel

Serikali ya mkoa wa Xinjiang nchini China imebadilisha sheria yake kuhalalisha uwepo wa makambi ya kuwazuwilia watu wa jamii ya Waislamu walio wachache. Takribani Waislamu milioni 1 wanakadiriwa kushikiliwa kwenye makambi kama hayo. 

Mamlaka za China, katika mkoa wa Xinjiang ulioko kaskazinimagharibi ya mbali, zimerejelea sheria zake na sasa zimeruhusu matumizi ya kile kinachotajwa kama "vituo vya elimu na mafunzo" katika kukabiliana na itikadi kali za kidini.

Kiuhalisia, vituo hivyo ni makambi ambayo Waislamu walio wachache wapatao milioni 1 wanashikiliwa kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita, hii ikiwa ni kulingana na ripoti za makundi ya haki za binaadamu na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Mabadiliko ya sheria hizo yanasema kwamba, serikali za mikoa za China zinaweza kujenga vituo vya mafunzo na elimu, ili kuwafunza na kuwasaidia wale walioathiriwa na itikadi kali.

Hata hivyo, licha ya kuwafundisha lugha ya Mandarin na elimu ya ufundi, chini ya kifungu kipya, vituo hivyo vinaagizwa kutoa "elimu ya kiitikadi, kuwasaidia kisaikolojia na marekebisho ya tabia".

China Uiguren
Mwanamke wa Kiislamu wa Uighur akiwa amejifunika usoni, hatua iliyosababisha China kuanzisha hatua kaliPicha: P. Parks/AFP/Getty Images

Sophie Richardson wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, alipozungumza na kituo cha televisheni cha DW amesema China inawashikilia Waislamu hao walio wachache wanaotambulika kama Uighur kwenye makambi hayo na kutoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati.

Hata hivyo China inakana madai kwamba vituo hivyo ni makambi yanayowashikilia jamii hiyo ya Waislamu walio wachache, lakini imekiri kwamba hata mashitaka ya uhalifu mdogo yamekuwa yakiwasilishwa kwenye vituo kama hivyo. Mmoja ya aliyewahi kushikiliwa kwenye makambi hayo ameliambia shirika hilo la haki za binaadamu kwamba walikuwa wanalazimishwa kuukana Uislamu na kuthibitisha uaminifu wao kwa chama cha Kikomunisti cha China.

Watu wa jamii za Uighur, Kazakh na Waislamu wengine walio wachache wanaoishi nje ya nchi wamesema hawana uwezo wa kuwasiliana na ndugu zao walioko China.

Serikali ya China kwa miongo kadhaa imejaribu kuyazuia mavuguvuvu yanayounga mkono uhuru miongoni mwa jamii hiyo ya Waislamu ya Xinjiang.

Mamlaka za China zimesema kwamba wafuasi wa itikadi kali kwenye eneo hilo wana mahusiano na makundi ya kigaidi, lakini ilitoa ushaidi finyu wa kuunga mkono madai hayo.

Mabadiliko haya ya hivi karibuni ya kisheria yamekuja baada ya serikali ya mkoa kuanzisha hatua kali dhidi ya bidhaa za halal na kuzuia uvaaji wa vitambaa vinavyofunika uso.

Mwandishi: Lilian Mtono/https://www.dw.com/en/chinas-xinjiang-region-legalizes-muslim-internment-camps/a-45837413

Mhariri: Iddi Ssessanga