China yafungua kituo cha kwanza cha kijeshi Djibouti | Matukio ya Afrika | DW | 12.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

China yafungua kituo cha kwanza cha kijeshi Djibouti

China imewatuma wanajeshi wake watakaohudumu katika kituo chake cha kwanza cha kijeshi nje ya nchi, kitakachokuwa nchini Djibouti.

Nafasi ya Djibouti kwenye ukingo wa Bahari ya Hindi imeongeza wasiwasi nchini India kuwa inaweza kuwa mojawapo ya washirika wa kijeshi wa China, ikiwa ni pamoja na Bangladesh, Manyamar na Sri Lanka.

China ilianza ujenzi wa kituo cha kijeshi nchini Djibouti mwaka jana ambacho kitatumiwa katika kuwasilisha vifaa kwenye meli zake za kivita zinazoshiriki katika operesheni za kulinda amani na za misaada ya kiutu hasa katika pwani za Yemen na Somalia.

Hiki kitakuwa kituo cha kwanza cha kijeshi cha China nje ya nchi, ijapokuwa China inakielezea kuwa ni kituo cha vifaa.

Shirika la habari la taifa Xinhua limesema katika ripoti fupi kuwa meli zilizowabeba askari wa Jeshi la Ukombozi la China ziling'oa nanga kutoka bandari ya kusini mwa China ya Zhanjiang kuelekea Djibouti.

Kamanda wa jeshi la majini Shen Jinlong alisoma taarifa kuhusu ujenzi wa kituo hicho nchini Djibouti lakini ripoti hiyo haikusema ni lini kituo hicho kitaanza operesheni zake.

China Xi Jinping nimmt Militärparade in Hongkong ab (picture-alliance/AP Images/Y. Shimbun)

Rais wa China Xi Jinping akikagua gwaride la kijeshi

Shirika la Xinhua limesema ujenzi wa kituo hicho ulikuwa uamuzi uliofanywa na nchi zote mbili baada ya "mazungumzo ya kirafiki, na mikataba ya maslahi ya pamoja kwa watu wa nchi zote mbili”.

Kituo hicho ktahakikisha ushiriki wa China katika operesheni kama vile za kusindikiza, kulinda amani na za misaada ya kiutu barani Afrika na Asia magharibi

Aidha kituo hicho kitakuwa muhimu katika majukumu ya kigeni yakiwemo operesheni za kijeshi, mazoezi ya pamoja, kuhamisha na kuwalinda Wachina wanaoishi ng'ambo na uokozi wa dharura pamoja na udumishaji wa pamoja wa usalama wa njia muhimu za kimataifa za bahari

Gazeti la Jeshi la Ukombozi la China limesema kwenye ripoti ya ukurasa wake wa mbele kuwa hio ni hatua ya kihistoria ambayo itaongeza uwezo wa China wa kuhakikisha amani ya kimataifa, hasa kwa sababu ina wanajeshi wengi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa barani Afrika na pia inahusika katika doria za kupambana na uharamia.

Ripoti hiyo imesema China haitatafuta kuweka vikosi vyake sehemu mbalimbali duniani lake au kujiingiza katika mashindano ya silaha.  

Djibouti, ambayo inalingana na Wales kwa ukubwa, inapatikana katika mlango wa kusini wa Bahari ya Shamu kuelekea katika Mfereji wa Suez. Nchi hiyo ndogo ambayo iko katikati ya Ethiopia, Eritrea na Somalia, pia ina vituo vya kijeshi vya Marekani, Japan na Ufaransa.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com