Chanjo kwa ajili ya watoto Milioni 300 | Masuala ya Jamii | DW | 28.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Chanjo kwa ajili ya watoto Milioni 300

Idadi ya watoto wanaokufa kutokana na maradhi yanayoweza kuepukwa, kama vile surua bado ni kubwa katika nchi zinazoendelea. Lakini sasa wafadhili wa kimataifa wanakusudia kuibadilisha hali hiyo.

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller aahidi chanjo kwa watoto wote

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller aahidi chanjo kwa watoto wote

Waziri wa Ujerumani anaeshughulikia ushirikiano wa maendeleo Gerd Müller amesema hadi kufikia mwaka wa 2030, hakuna mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano atakeachiwa afe kutokana na maradhi yanayoweza kuepukwa.

Waziri Müller aliyasema hayo kwenye mkutano wa wafadhali wa kimataifa uliofanyika mjini Berlin ambapo washiriki walijadili mikakati ya kutoa chanjo za kuyakinga maradhi kama surua, kifaduro,homa ya manjano na maradhi ya kupooza.

Mkutano huo wa kile kinachofahamika kama mfungamano wa kimataifa wa chanjo dhidi ya maradhi yanayoweza kuepukwa Gavi, uliwaleta pamoja viongozi,kutoka nchi zinazoendelea na wafadhili kutoka duniani kote.

Tanzania yapata mafanikio

GAVI Konferenz in Berlin 27.01.2015

Mkutano wa GAVI mjini Berlin, Bilionea Bill Gates Waziri Mkuu wa Norway Erna Solberg, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita

Akihutubia kwenye mkutano huo wa "Gavi" Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania aliarifu juu ya mafanikio ya nchi yake katika kutoa chanjo kutokana na msaada wa Gavi Amesema kutokana na msaada wa Gavi ,Tanzania imeweza kutoa chanjo mpya 11. Rais Kikwete amefahamisha kwamba Tanzania imo miongoni mwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara zinazotoa chanjo kwa mafanikio.

Rais Kikwete amesema asilimia 90 ya watoto nchini Tanzania wamechanjwa ili kukinga maradhi ya kupooza na asimilia 90 nyingine wamepewa chanjo ya kuuzuia ugonjwa wa surua.

Mpango unaokusudiwa kutekelezwa na asasi ya Gavi ni kutoa chanjo kwa watoto Milioni 300 katika nchi zinazoendelea hadi mwaka wa 2020.

Mfungamano wa Gavi ni ushirikiano baina ya Shirika la Afya Duniani,WHO,Benki ya Dunia, Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa na wafadhili kadhaa wa kimataifa ikiwa pamoja na Wakfu wa Bill Gates.

Kiasi cha fedha kinachohitajika ili kuweza kuendelea huduma ya chanjo ni Euro Bilioni 6.6 . Wakfu wa Bill Gates umechangia kiasi cha dola Bilioni 1.5. Gates amesema ndoto yake ni kuona kwamba kila mtoto anapata chanjo za kukinga maradhi. Ujerumani itachangia kiasi cha Euro Milioni mia sita.

Kutokana na mradi wa Gavi watoto nusu Bilioni wameshapatiwa chanjo dhidi ya maradhi kama kichomi na surua katika nchi zinazoendelea.

Mwandishi:Werkhäuser Nina

Tafsiri:Mtullya abdu.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com