1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia awaonya wanasiasa wanaochochea chuki

11 Septemba 2023

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaonya wanasiasa nchini humo kuacha mara moja kutumia uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara kuchochea chuki na vurugu.

https://p.dw.com/p/4WCRV
Tansania Sansibar Präsidentin Samia Suluhu Hassan bei Kizimkazi Festival
Picha: Presidential Press Service Tanzania

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema nia ya serikali yake ni kujenga taifa lenye umoja na kwamba hakuna Mtanzania anayeweza kujifanya ndiye mwenye uchungu zaidi na taifa kushinda mwenzake. 

Akiwa katika mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaowashirikisha wadau wa demokrasia na vyama vingi vya siasa, Rais Samia ameonyesha hasira zake kwa wanasiasa wanaoyatumia majukwaa kuanzisha chokochoko.

Amesema utawala wake uliondoa marufuku ya mikutano ya hadhara si kwa lengo la kufungua milango ya kuanzisha mihadhara ya kukashifiana, bali ilifungua milango kwa vyama vya siasa kuzungumza na wafuasi wao masuala yanayohusu sera na mikakati ya kuelekea chaguzi za usoni.

Aliongeza "Hatukutoa fursa ile watu wakavunje sheria, watu wakasimame kutukana, watu wakasimame kuchambua dini za watu, lakini sishangai kwa nini haya yanatokea, sababu ya kuzungumza hakuna.."

Hivi sasa vyama vya siasa vimekuwa vikizunguka kuzungumza na wafuasi wao baada ya maruku ya mikutano ya kisiasa iliyowekwa na rais aliyepita Hayati John Magufuli kwa miaka sita kuondolewa miezi ya karibuni. 

ChADEMA kimekuwa kikifanya mikutano ya hadhara nchini Tanzania kunadi azma yake ya kushinikiza masuala mbalimbali ya kidemokrasia
Mwenyekiti wwa CHADEMA Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari katika moja ya mikutano yake jijini Dar es SalaamPicha: Ericky Boniphace/DW

Mabadiliko ya katiba yatawala ajenda za mikutano ya vyama vya upinzani.

Baadhi ya ajenda zinazotawala katika mikutano mingi ya vyama hivyo zinahusu mabadiliko ya katiba, ugumu wa maisha pamoja na suala tete lililoibuka hivi karibuni kuhusu mkataba wa bandari baina ya serikali ya Tanzania na kampuni ya kigeni ya DP World ya Dubai.

Rais Samia amewakosoa pia wanasiasa wanaovalia njuga suala la mabadiliko ya katiba akisema mabadiliko hayo yataletwa na Watanzania wote na kamwe haiwezi kuwa ajenda ya wanasiasa pekee, huku akihimiza mjadala wa muda mrefu. "Kwa hiyo kuna uhuru wa maoni, lakini huu uhuru wa maoni una mipaka yake", alisema rais Samia.

Mwenyekiti wa zamu wa taasisi za demokrasia Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba amekumbusha nia ya vyama vya siasa kuona suala la katiba mpya linaendelea kuwa kipaumbele cha majadiliano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.

Kongamano hili la siku tatu linawajumuisha wadau mbalimbali wa masuala ya demokrasia huku vyama vyote 19 vyenye usajili rasmi vikishiriki. Zaidi ya wajumbe 600 wanashiriki kongamano hilo ambalo mwishoni linakusudia kuwasilisha mapendekezo yake serikalini.

Rais Samia ameyazungumza hayo wakati ambapo Makamu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA,Tundu Lissu akiwa ameachiwa kwa dhamana baada ya kukamatwa na polisi siku ya Jumapili huko Karatu mkoani Arusha, kwa madai ya kutaka kufanya mkutano bila ya kibali maalumu katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambako jamii ya Wamaasai wanaishi. 

Sikiliza Zaidi: 

Polisi Tanzania yawaonya wanaotaka kuipindua serikali