1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Brazil yatoa wito wa mageuzi katika Umoja wa Mataifa

Tatu Karema
22 Februari 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil Mauro Vieira, ametoa wito wa mageuzi makubwa katika UN na taasisi nyingine za kimataifa kama kipaumbele cha urais wa nchi hiyo mwaka huu wa kundi la G20

https://p.dw.com/p/4ciYB
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 nchini Brazil kuzungumzia jukumu la kukabiliana na migogoro ya kimataifa mnamo Februari 21, 2024
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 nchini BrazilPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana Jumatano mjini Rio nchini Brazil kuandaa ajenda ya mkutano wa kilele wa G20 mwezi Novemba, Brazil iliulaumu Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa kwa kushindwa kukomesha vita na migogoro inayoongezeka na kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.

Soma pia:Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G20 wakutana Brazil

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil Mauro Vieira, alitoa wito wa mageuzi makubwa ya utawala wa kimataifa kama kipaumbele cha urais wa nchi hiyo mwaka huu wa kundi hilo la mataifa yenye uchumi mkubwa duniani.

Vieira asema taasisi za kimataifa hazina raslimali za kushughulikia migogoro

Vieira amesema kuwa taasisi za kimataifa hazina raslimali za kutosha kushughulikia changamoto za sasa, kama inavyoshuhudiwa katika hali isiyokubalika ya kushindwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushughulikia migogoro inayoendelea.

Soma pia;Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani ambebesha dhamana rais wa Urusi kuhusu vita vya Ukraine

Mawaziri kutoka mataifa hayo yaG20, ikiwa ni pamoja na Marekani na Urusi, walianza mazungumzo huru kuhusu mivutano ya sasa ulimwenguni na njia za kuboresha mashirika ya kimataifa, suala la kipaumbele lililowasilishwa na Rais wa Brazil Luiz Ignacio Lula da Silva, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza umaskini.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi habari akiwa na mwenzake wa Poland Radoslaw Sikorski mjini Berlin mnamo Januari 30, 2024
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Azma ya Brazil ya uwakilishi mpana wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopanuka inayoonesha dunia inayobadilika, iliungwa mkono na waziri wa mambo ya nje wa Japan Yoko Kamikawa, licha ya ugumu wa kufikia maelewano.

Blinken akutana na Lula mjini Brasilia

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alikutana na Lula mjini Brasilia akielekea kwenye mkutano huo unaofanyika mjini Rio na kuelezea uungaji mkono wa Marekani kwa ajenda ya Brazil ya kufanya utawala wa kimataifa kuwa bora zaidi. Haya ni kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller.

Blinken na Lula wazungumzia mzozo wa Mashariki ya Kati

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alijadili na Lula kuhusu vita vya Israel katika Ukanda waGaza, huku kukiwa na mzozo wa kidiplomasia baada ya kiongozi huyo wa Brazil kufananisha vita hivyo vya Israeli na mauaji dhidi ya Wayahudi ya wakati wa utawala wa Wanazi.

Baerbock atoa wito wa suluhisho kwa migogoro ya Ukraine na Mashariki ya Kati

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, ametoa wito kwa kundi hilo la G20 kushinikiza kupata suluhisho kwa migogoro ya Ukraine na Mashariki ya Kati.

Baerbock amesema hayo pembezoni mwa mkutano huo wa G20 na kuongeza kuwa ulimwengu hautakuwa wa haki ikiwa hawatapa suluhisho la mizozo hiyo.