1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouteflika ajiandaa kurudi Algeria Jumapili

Saumu Mwasimba
10 Machi 2019

Ndege ya rais huyo itaondoka ndani ya muda mfupi kutoka Geneva kuelekea Algiers nchini Algeria

https://p.dw.com/p/3EkY4
Schweiz Genf algerischer Regierungsflieger trifft ein
Picha: Reuters/D. Balibouse

Ndege ya rais wa Algeria AbdelAziz Bouteflika itaondoka ndani ya muda mfupi kutoka Geneva kumpeleka nyumbani kiongozi huyo,kimetangaza kituo cha televisheni cha Ennahar,leo jumapili. Bouteflika anayekabiliwa na maandamano makubwa nchini Algeria alikuwa akitibiwa hospitali  mjini Geneva katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Ndege hiyo itakayomrudisha rais Bouteflika nyumbani imetajwa kwamba ilituwa Geneva asubuhi Jumapili huku zikiwepo taarifa kwamba rais huyo anayeugua huenda akarudi nyumbani baada ya ziara ya wiki mbili ya matibabu nchini Uswisi. Msemaji wa harakati za kampeini za rais huyo Hamrawi Habib Shawki ameliambia shirika la habari la kijerumani dpa kwamba Bouteflika atarudi nyumbani katika kipindi cha saa kadhaa.

Ikumbukwe kwamba Algeria imegubikwa na maandamano ya umma tangu Februari 22 ambapo mamia kwa maelfu ya wananchi wamekuwa wakiandamana kuipinga mipango ya rais huyo mwenye umri wa miaka 82 ya kutaka kugombea muhula wa tano madarakani katika uchaguzi wa Aprili.

Algerien Studenten protestieren in Algier gegen Bouteflika
Picha: Reuters/R. Boudina

Leo Jumapili 10.03.2019 umefanyika mgomo ukishirikisha makampuni ya serikali ya binafasi pamoja na taasisi kupinga harakati hizo za rais Bouteflika. Mgomo huo umefanyika kutokana na miito iliyotolewa na wanaharakati katika mitandao ya kijamii. Wafanyakazi wa shirika la huduma za mawasiliano ya simu  la Algeria Telecom, bandari ya Skikda na benki ya Algeria pamoja na shirika la umeme na gesi la Sonelgaz linalomilikiwa na serikali walishiriki mgomo huo. Kadhalika imeelezwa maduka chungunzima yalifunga milango yao nchini humo.

Mkuu wa majeshi Gald Saleh amesema kupitia hotuba yake Jumapili kwamba jeshi la nchi hiyo pamoja na wananchi wana mtazamo wa mshikamano. Awali mkuu huyo wa majeshi alitowa onyo kwamba jeshi halitoruhusu uvunjaji wa sheria za usalama. Rais Bouteflika alipata ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013 na tangu wakati huo hajawahi kuonekana hadharani . Ni rais pekee katika eneo hilo la afrika Kaskazini aliyenusurika katika harakati za vuguvugu lililopiga katika nchi za kiarabu la kudai demokrasia lililoanzia nchini Tunisia mwaka 2010.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sylvia Mwehozi