Boris Johnson aelekea bungeni na mpango wake mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Wabunge nchini Uingereza kufikishiwa mpango mpya

Boris Johnson aelekea bungeni na mpango wake mpya

Baada ya kuuwasilisha mpango wake mpya kuhusu Brexit Umoja wa Ulaya sasa anaupeleka bungeni ambako anakabiliwa na kimbembe kutokana na kukosa wingi unaomuunga mkono. Hata Umoja wa Ulaya mpango huo unaonesha haukubaliki

Waziri Mkuu Boris Johsnon anaupeleka  mpango wake mpya anaouamini mbele ya bunge la nchi yake mjini London baada ya jana kuwapelekea viongozi wa Umoja wa Ulaya. Mpango huo unajumuisha mabadiliko  yanayohusu mipango na taratibu za kusimamia biashara kati ya Ireland na Ireland Kaskazini baada ya Uingereza kuuaga Umoja wa Ulaya,katika kile kinachoitwa Brexit.

Mpango huu umepokelewa kwa hisia mchanganyiko na viongozi wa Umoja wa Ulaya na inaonesha kwamba haujayafikia hata chembe yale yanayotakiwa na viongozi hao ili waridhie suala la kuuacha wazi mpaka wa Ireland. Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika Umoja huo ambaye hakutajwa jina,amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema mpango wa Johnson hauna nguvu kwa maneno mengine hauna unakokwenda,kwasababu hauna suluhisho bali unaleta mtengano kati ya pande hizo mbili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa anayehusika na masuala ya Ulaya Amelie De Montchalin anasema waziri mkuu Johnson ana matatizo.

''Boris Johnson ana matatizo. Kwa hakika hivyo ndivyo ilivyo, ameshauriana na Umoja wa Ulaya lakini kitu cha muhimu ni kwamba hana tena wingi bungeni. Mtazamo wa kisiasa nchini Uingereza umegawika kabisa. Na kwa hivyo anapambana ndani ya bunge lake, ndani ya kambi yake ya kisiasa kama ambavyo anapambana na sisi katika Umoja wa Ulaya.''

Boris Johnson anasisitiza kwamba Uingereza itaondoka Umoja wa Ulaya Octoba 31 iwe ni kwa makubaliano au bila makubaliano lakini bunge limeshapitisha sheria inayomtaka kutafuta njia za kurefusha muda ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa.

Lakini kwa upande mwingine sio tu Uingereza iko kwenye mgawanyiko mkubwa kisiasa pia hali ya kiuchumi inaonesha Uingereza inaueleka kutumbukia kwenye mporomoko wa kiuchumi ambapo makampuni yanajiandaa kukabiliwa na  kitisho Brexit ya mparaganyiko katika kipindi cha wiki chache zijazo.

Hata waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo Jana alitowa kauli yake juu ya Brexit na kusema kwamba kuna hatari kwa kiasi fulani kwamba ikiwa Uingereza itaondokla Umoja wa Ulaya kuna uwezekano wa kuhujumiwa kwa uchumi wa Uingereza,Ulaya na hata uchumi wa dunia kwa ujumla.

Uingereza yenyewe leo imeitolea mwito Umoja wa Ulaya kuwa wabunifu na kuwa tayari kubadilika kuhusu suala la Brexit baada ya waziri mkuu Boris Johnson kutowa mpango wake mpya.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo