1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Waafghanistan waamue mustakabali wa nchi yao

9 Julai 2021

Rais Joe Biden ameutetea vikali uamuzi wake wa kuviondoa vikosi vya Marekani Afghanistan, akisema Waafghanistan wanastahili kuamua mustakabali wao na hatotuma wanajeshi wengine katika vita hivyo vya zaidi ya miaka 20.

https://p.dw.com/p/3wFd5
USA Washington DC | Unabhängigkeitsfeier
Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Akizungumza katika ikulu ya White House, Biden amesema jeshi la Afghanistan lina uwezo wa kupambana na wanamgambo wa Taliban huku akikanusha ripoti kwamba idara ya ujasusi Marekani inatazamia kwamba serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Marekani itaanguka katika kipindi cha miezi sita ijayo tu huku kukiwa na tahadhari kuhusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini humo.

Rais huyo amesema wanajeshi wote wa Marekani isipokuwa 650 watakaoulinda ubalozi wa Marekani mjini Kabul, watakuwa wameondoka kufikia Agosti 31. Fauka ya hayo, amesema maelfu ya wakalimani wa Afghanistan watapelekwa katika maeneo salama.

Kuendelea kusalia Afghanistan si suluhisho la amani kupatikana nchini humo

Biden lakini amekiri pia kwamba karibu miaka 20 baada ya majeshi ya Marekani kuuangusha utawala wa Talibamn kufuatia yale mashambulizi ya Septemba 11, uwezekano wa serikali ya Afghanistan kuweza kuitawala nchi yote ni mdogo mno. Kulingana na Biden Marekani imeshayatimiza malengo yake katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati yakiwa ni pamoja na kumuua Osama bin Laden, kulidhoofisha kundi la kigaidi la Al-Qaeda na kupunguza mashambulizi Marekani.

TABLEAU | 100 Tage Biden
Biden akitembea katika makaburi ya wanajeshi waliouwawa AfghanistanPicha: Brendan Smialowski/AFP

"Mwaka 2014 wengine walisema tukae mwaka mmoja zaidi, kwa hiyo tukaendelea kupigana na wanajeshi wetu wakaendelea kufa. Mwaka 2015, ikawa vivyo hivyo. Karibu miaka 20 ya uzoefu imetuonyesha na hali ya kisiasa ya sasa inathibitisha kuwa mwaka mmoja zaidi wa mapigano Afghanistan si suluhisho ila mwanzo wa kusalia huko kwa kipindi kisichobainika," alisema Biden.

Biden amesema ana imani na majeshi ya Afghanistan ambayo kwa miaka sasa yamekuwa yakipewa mafunzo na kupokea silaha kutoka kwa Marekani kwa ajili ya kupambana na Taliban.

Mapigano yanaendelea Afghanistan wakaazi wakiyakimbia makaazi yao

Hotuba aliyoitoa Biden ndiyo kauli ya undani zaidi aliyoitoa katika siku za hivi karibuni kuhusiana na uamuzi wake wa kuyaondoa majeshi ya Marekani kufuatia shinikizo kutoka kwa wakosoaji waliokuwa wanataka maelezo zaidi kuhusiana na huo uamuzi wake.

Trump atangaza mkakati wa kijeshi Afghanistan

Rais huyo wa Marekani amezitaka nchi zote katika ukanda huo kusaidia kupatikana kwa suluhisho la kisiasa kati ya pande zinazozozana huku akiitaka serikali ya Afghanistan kutafuta mwafaka na Taliban kwa ajili ya amani ya nchi hiyo.

Haya yanakuja wakati ambapo mapigano yameendelea kwa siku ya pili mfululizo katika mji mkuu wa mkoa wa Badghis huku wakaazi wakiyakimbia makaazi yao na wengine wakijifungia majumbani. Tangu Marekani ianze shughuli ya kuwaondoa wanajeshi wake, kundi la Taliban limeanzisha kampeni ya kuyateka maeneo mapya na kuna hofu kwamba majeshi ya Afghanistan yatashindwa nguvu bila usaidizi wa majeshi ya Marekani.