1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCanada

Biden na Trudeau kujadili juu ya biashara na uhamiaji haramu

24 Machi 2023

Canada na Marekani zinaripotiwa kufikia makubaliano ya kuwarudisha makwao wanaotafuta hifadhi hasa kwa wahamiaji wanaovuka mipaka isiyokuwa rasmi kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/4PC8X
Kanada, Ottawa | Joe Biden trifft Justin Trudeau
Picha: Blair Gable/REUTERS

Makubaliano hayo yanaashiria maendeleo makubwa katika wakati ambapo visa vya watu wanaovuka mipaka ya Marekani na kuingia nchini Canada vimefikia rekodi ya kutisha. 

Makubaliano hayo yatairuhusu aidha Marekani ama Canada kuwarejesha makwao wahamiaji ambao huvuka mipaka isiyokuwa rasmi, na kupanua makubaliano ya nchi tatu ya usalama-STCA, ambayo sasa yatajumuisha pia wahamiaji walioruhusiwa kuvuka katika bandari rasmi za kuingia nchi hizo mbili.

Soma pia: Trump na Trudeau watofautiana

Kando na hayo, Canada pia itafungua fursa za nafasi 15,000 kwa wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kaskazini kama vile Mexico, Guatemala, El Salvador, Costa Rica na Honduras kuomba vibali vya kuingia nchini humo, hatua hiyo ikiwa sehemu ya makubaliano hayo.

Biden na Trudeau kujadili juu ya hali ya usalama Haiti 

Symbolbild Gewalt in Haiti
Waandamanaji wakichoma matairi mjini Port-au-Prince.Picha: Jean Mark Herve Abelard/imago images/Agencia EFE

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na Rais wa Marekani Joe Biden wanatarajiwa kando na mambo mengine, kujadili juu ya suala hilo la uhamiaji wakati wa mkutano wao utakaofanyika mjini Ottawa leo Ijumaa. Tangazo juu ya masuala watakayokuwa wameyajadili linatarajiwa kutolewa baadaye ingawa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo bado vinafanyiwa kazi.

Trudeau amekuwa chini ya shinikizo kubwa la kisiasa hasa kutokana na visa vya uhamiaji haramu kuongezeka nchini Canada na mnamo mwezi Februari, kiongozi huyo alisema kuwa ataliweka mezani suala hilo wakati wa ziara ya Biden.

Viongozi hao wawili, katika mazungumzo yao ya mjini Ottawa, pia wanatarajiwa kuzungumzia juu ya kushughulikia hali mbaya ya kiusalama na kibinadamu nchini Haiti.

Makubaliano hayo ya uhamiaji, kulingana na maafisa kutoka Washington na Ottawa, yatairuhusu Canada kuwarudisha wahamiaji kutoka kivukio cha barabara ya Roxham, mpaka usio rasmi kutoka jimbo la New York, ambao hutumiwa na wahamiaji wanaotafuta hifadhi nchini Canada.

Biden aliwasili nchini Canada jana Alhamisi katika ziara iliyocheleweshwa. Madhumuni mengine ya ziara hiyo ni kuieleza Canada juu ya umuhimu wa kuiunga mkono Ukraine.

Biden kulihutubia bunge la Canada

Rais huyo wa Marekani anatarajiwa kulihutubia bunge la Canada leo Ijumaa alafu baadaye, viongozi hao wawili wataanda mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Kanada | Parlament Notstandsgesetz
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau akihutubia bunge la nchi hiyo.Picha: Blair Gable/REUTERS

Shughuli za uhamiaji kati ya mipaka ya nchi hizo mbili zinaongozwa na makubaliano ya nchi tatu ya usalama unaojulikana kama STCA, ambao unairuhusu Marekani na Canada kuwarudisha wahamiaji kutoka nchi zote mbili wanaotumia mipaka rasmi, japo makubaliano hayo hayazingatiwi pindi wahamiaji wanapotumia njia za mkato zisizokubaliwa kwa mfano mpaka wa Quebec Roxham.

Waziri Mkuu wa Quebec François Legault, pamoja na wanasiasa wa upinzani wametoa miito ya kufungwa kwa mpaka wa barabara ya Roxham kutokana na kufurika kwa wahamiaji, lakini kama jibu kwa viongozi wa jimbo hilo, serikali ya Canada imekuwa ikiwasafirisha wahamiaji kwenda katika mikoa mengine.