1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yawaalika Chelsea, Frankfurt wenyeji wa Galatasaray

17 Septemba 2025

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich Jumatano watawaalika miamba wa England Chelsea katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

https://p.dw.com/p/50cma
Wachezaji wa Bayern Munich wakisherehekea kufunga goli
Wachezaji wa Bayern Munich wakisherehekea kufunga goliPicha: Frank Hoermann/SvenSimon/picture alliance

Mechi hiyo itakayochezwa katika uwanja wa nyumbani wa Bayern itawampatanisha mchezaji aliye kwa mkopo Bayern Nicolas Jackson na klabu yake ya Chelsea.

Kocha wa Bayern Vincent Kompany na washambuliaji wake Harry Kane, Luis Diaz na Michael Olise wanaifahamu vyema Chelsea kutokana na kuwa waliwahi kucheza kwa muda mrefu katika ligi kuu ya nchini humo katika vilabu vya Manchester City, Tottenham Hotspur, Liverpool na Crysital Palace.

Kwengineko timu nyengine ya Ujerumani Eintracht Frankfurt itakuwa mwenyeji wa Galatasaray ya Uturuki siku ya Alhamis.

Kocha wa Frankfurt Dino Toppmöller amewaambia wachezaji wake wafurahie mashindano hayo ya vilabu bora zaidi Ulaya.

Mchezaji wa Eintracht Frankfurt Ritsu Doan
Mchezaji wa Eintracht Frankfurt Ritsu DoanPicha: Uwe Anspach/dpa/picture alliance

Frankfurt wana mechi ngumu za makundi ambapo watakuwa wanakwaana pia na Liverpool, Napoli, Barcelona, Tottenham Hotspur na Atletico Madrid.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Frankfurt kushiriki mashindano hayo katika historia yao baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Bundesliga msimu uliopita.

Bayer Leverkusen, mwakilishi mwengine wa Ujerumani atakuwa Copenhagen, nchini Denmark siku ya Alhamis kupambana na FC Kobenhavn.