Ban Ki Moon aizuru Haiti | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 18.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Ban Ki Moon aizuru Haiti

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amefanya ziara mjini Port-au Prince na kujionea uharibifu mkubwa uliosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea siku sita zilizopita

Katibu mkuu wa UN Ban Ki Moon

Katibu mkuu wa UN Ban Ki Moon

Leo anatazamiwa kutoa tathmini yake mbele ya kikao cha baraza la usalama la Umoja huo mjini New York.Aidha kikubwa kinachohofiwa kwa sasa ni kuzorota kwa hali ya usalama endapo shughuli za kutoa msaada hazidhibitiwa sawasawa. Jana vurugu zilienea katika mji wa Port-au Prince watu wakipigania kupata msaada.Kundi la majambazi wenye silaha pia linasemekana kurudi kwenye mji wa Cite Soleil tangu jela walimokuwa kuporomoka baada ya kutokea tetemeko hilo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alipowasili katika mji wa Porta-au Prince alilakiwa na makelele ya wahanga wa tetemeko hilo la ardhi wakimuuliza kwa fujo uko wapi msaada,wapi chakula?Maelfu ya watu walionusurika wanaishi kwenye makaazi ya muda yaliyotengenezwa kando ya ikulu ya rais iliyoporomoka.Ban Ki Moon ambaye ametembelea maeneo hayo amelifananisha janga hilo na janga la Tsunami lilotokea mwaka 2004 barani Asia.Amesema ni mojawapo ya mzozo mkubwa wa kibinadamu uliopata kushuhudiwa katika kipindi cha muongo mmoja.Aidha akiulizwa ikiwa anahofia kutokea kwa ghasia kutokana na hali ya kuchelewa kufikishwa misaada kwa wahanga kiongozi huyo wa Umoja wa mataifa alitoa mwito kwa wananchi wa Haiti kuwa na subira zaidi na kuwapongeza kwa ujasiri wao.

Hali ni mbaya

Flughafen in Haiti Port au Prince Mc Chord Air Base

Msongamano wa wahanga wa Haiti kwenye uwanja wa ndege

Katibu Mkuu Ban Ki Moon pia alikutana na Rais Rene Preval na leo hii anatazamiwa kutoa tathmini yake mbele ya baraza la Usalama la umoja huo kuhusu hali ya mambo ilivyo katika taifa hilo.Hata hivyo kucheleweshwa kufika kwa misaada kwa wahanga kunaibua masuali mengi juu ya kuzuka kwa ghasia nchini humo.Licha ya kutapakaa kila mahala maafisa wa polisi na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa bado hawajaweza kuzuia fujo na kuweka hali ya usalama kamili huku watu nao wakizidi kupoteza subira .Mamia ya watu walimiminika kwenye maduka yaliyovunjika katika mji huo mkuu wa Porta-Au Prince kwa siku ya pili mfululizo.

Wezi hao wamepigana wenyewe kwa wenyewe kwa visu,nyundo na mawe huku polisi nao wakijaribu kuwatawanya kwa kufyetua risasi.Watu wawili wameuwawa.Kwa mujibu wa serikali ya Haiti kuna majambazi 3000 ambao wametoroka kutoka jela baada ya kutokea tetemeko hilo la ardhi hali ambayo inazusha wasiwasi mkubwa kuhusu usalama.Tayari serikali imetoa jukumu la ulinzi wa uwanja wa ndege unaotumika kwa jeshi la Marekani ili kusimamia ndege zinazoingiza misaada kutoka duniani kote.Hata hivyo hatua ya Marekani ya kupeleka wanajeshi wengi nchini humo imekosolewa na waziri wa ulinzi wa Haiti Patrice Elie,''Hatuhitaji kiasi hicho wanajeshi,hakuna vita hapa.''

Usalama duni

Wanajeshi kiasi cha elfu 3 wa Marekani wameshapelekwa nchini Haiti.Pia waziri huyo wa Ulinzi wa Haiti ameikosoa hatua ya kupewa dhamana jeshi la Marekani la kulinda uwanja wa ndege.

'' Uamuzi juu ya kile kinachotua na kile kisichotakiwa kutua kwenye ardhi ya Haiti,na ndege gani inapewa kipaumbele kutua ni suala linalobidi kuachiwa wa Haiti waamue.Vinginevyo ni kupindua madaraka na kile kitakachotokea ni kwamba maslahi ya wa Haiti hayatozingatiwa bali nchi ya kigeni itaanza kuamua nini wa Haiti wanahitaji au kujaribu kusukuma agenda zake''

Hata hivyo Marekani imesema kwamba lengo lake ni kuweka usalama kwa ajili ya kufanikisha shughuli za kutoa msaada na sio vinginevyo.Tayari taifa hilo limekuwa likisaidiwa na wanajeshi kiasi cha 9,000 wa Umoja wa mataifa kuweka amani tangu mwaka 2004 kufuatia kuzuka kwa machafuko ya kisiasa.

Mwandishi Saumu Mwasimba/ RTRE/AFPE

Mhariri:Mwadzaya,Thelma

 • Tarehe 18.01.2010
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LYnn
 • Tarehe 18.01.2010
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LYnn
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com