1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia: Wanamgambo waingia DRC

Mitima Delachance4 Mei 2021

Asasi za kiraia katika bonde la mto Ruzizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimetoa malalamiko kuhusu watu wenye silaha wanaoingia nchini humo kisiri wakivuka mto Ruzizi.

https://p.dw.com/p/3sx3L
DRK Symbolbild FARDC
Picha: Alain Wandimoyi/AFP

Muda mfupi baada ya kutangazwa kuanzishwa kwa utawala wa dharurakatika mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Ituri mashariki ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, asasi nyingi za kiraia katika bonde la mto Ruzizi zinatoa malalamiko kuhusu kuingia kwa siri kwa watu wenye silaha ambao asasi hizo zinasema  wanavuka mto Ruzizi tangu Jumatatu kutoka nchi jirani ya Burundi.

Asasi hizo zimesema kwamba watu wenye silaha ambao utambulisho wao na idadi yao havijulikani bayana wamevuka mto Ruzizi kutoka nchi ya Burundi hadi kwenye ardhi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo katika vijiji vya maeneo ya Sange, Kiliba na Mataba ambapo imedaiwa kuwa waliharibu mimea mashambani, katika bonde la mto Ruzizi, na baadae walielekea katika nyanda za wilaya ya Uvira.

Wakimbizi 3,000 DRC wajificha bondeni kufuatia mashambulizi

Wanaharakati hao akiwemo Jimmy Katuruma ambaye ni kiongozi wa shirika linalotetea amani, watoto walio hatarini, yatima na wajane, maarufu APEVOV, wamesema matukio mengine kama hayo yanafanyika mara kwa mara katika bonde hilo tangu zaidi ya miaka mitatu na kusikitikia hali ya kuwa Serikali ya Congo inaonekana kupuuza tahadhari zote kuhusu hali hiyo.

Hali ya wasiwasi mashariki mwa DRC kufuatia mashambulizi

Wakati huu mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Ituri inatarajia kuongozwa na wanajeshi katika hali ya dharura ili kujaribu kumaliza hali ya ukosefu wa usalama iliyokithiri upande huo wa Congo kwa muda mrefu, kulingana na amri ya rais wa Congo Felix Tshisekedi.

mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Ituri inatarajia kuongozwa na wanajeshi katika hali ya dharura
mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Ituri inatarajia kuongozwa na wanajeshi katika hali ya dharura.Picha: Alain Wandimoyi/AFP

Kulingana na André Byadunia ambaye ni kiongozi wa shirika mpya la kiraia katika wilaya ya Uvira, baadhi ya asasi za kiraia katika mkoa wa Kivu kusini zinaamini kuwa mkoa huo pia ungepaswa kujumuishwa katika hali hiyo kwa vile unaathirika pia na hali ya ukosefu wa usalama, hasa katika wilaya za Kalehe, Uvira, Fizi, Mwenga, Shabunda, Walungu na Kabare.

Zinahofia pia kwamba huenda wanamgambo wa ADF watakuwa na hofu na kujihifadhi katika mkoa huu jirani wa Kivu kusini.

Rais Tshisekedi atuma ujumbe Ituru ili kurejesha amani

Lakini hadi sasa, jeshi la jamhuri ya kidemokrasia ya Congo linahakikisha kuwa linafanya kila kitu ili kurejesha usalama katika bonde la mto Ruzizi na katika maeneo yote yanayodhibitiwa na wanamgambo wenye silaha.

Hata hivyo, msemaji wa jeshi hili katika wilaya za Uvira na Fizi, kapiteni Dieudonné Kasereka anasikitikia hali yakuwa baadhi ya vikundi vya wanamgambo raia wa Congo vinashirikiana na waasi toka nchi za kigeni, na hali hii inakwamisha juhudi za kurejesha usalama haraka katika baadhi ya maeneo husika.

Kuvuka kwa watu hao wenye silaha hadi kwenye ardhi ya Congo kunakoripotiwa na asasi za kiraia kunawapa wasiwasi  raia waliokimbia mapigano kati ya makundi yenye silaha katika nyanda za Uvira hadi ndani ya bonde hilo la mto Ruzizi, na wanatoa mwito kwa serikali ya Congo kuwahakikishia usalama.