1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini yawekwa chini ya jeshi

Jean Noël Ba-Mweze4 Mei 2021

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza hali ya mzingiro wa kijeshi katika mikoa ya Ituri na Kivu ya Kaskazini ambapo mauaji ya raia yanaripotiwa karibu kila leo. Amri hiyo itaanza kutekelezwa Alhamisi.

https://p.dw.com/p/3svoj
DR Kongo | Nord Ost Ituri | Menschenrechtsverletzungen
Picha: Tom Peyre-Costa/NRC

Tangazo hilo  lilitolewa Jumatatu jioni na Rais Felix Tshisekedi katika hotuba fupi iliyotangazwa kupitia redio na televisheni ya kitaifa. Mamlaka ya utawala na ya kimahakama sasa yatakuwa mikononi mwa jeshi na polisi.

Kuanzia Alhamisi, magavana wa mikoa hiyo miwili watawaachia nafasi askari, manaibu wa magavana watawachia polisi, halafu mawaziri wa mikoa watawachia wanajeshi watakaoteuliwa na magavana hao wa kijeshi.

Hali ya wasiwasi mashariki mwa DRC kufuatia mashambulizi

Hakuna kinga ya kibunge wakati wa utawala huu maalum, kwani mabunge ya mikoa hiyo yamesimamishwa. Mahakama ya kiraia zitabadilishwa na korti ya kijeshi. Rais Félix Tshisekedi amewaomba raia kuunga jeshi mkono.

"Kwa hivyo naalika kila mkongomani popote alipo, kwa uhamasishaji wa jumla ili kusaidiana na vikosi vyetu vinavyoulinda usalama wa eneo letu. Ni lazma raia wote kusimama pamoja na kuunga mkono wanajeshi wetu," amesema Tshisekedi.

Magavana kuripoti kwa Waziri wa Ulinzi

Mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini imekuwa ikishuhnudia machafuko ya mara kwa mara
Mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini imekuwa ikishuhnudia machafuko ya mara kwa maraPicha: Tom Peyre-Costa/NRC

Wakati wa hali hiyo Maalum, magavana wataripoti kwa Waziri wa Ulinzi wa Kitaifa. Viongozi hao wapya watakuwa na mamlaka zaidi, ila wataitumia wakiheshimu sheria, kama inavyoainishwa na amri iliyosomwa na Kasongo Mwema Yambayamba, msemaji wa Rais Tshisekedi.

Vita visivyokwisha vya makundi ya wanamgambo nchini Congo

"Wana uwezo wa kufanya misako  mchana na usiku katika majumba; kuwatenga watu waliopatikana na hatia na wale wasio na makao katika maeneo yaliyo chini ya ulinzi. Kutafuta na  kuamuru ukabidhianaji wa silaha. Kukataza machapisho pia maandamano wanayoyumbisha usalama wa umma," amesema Kasongo Mwema.

Hali hiyo ni ya mwezi mmoja lakini itaendelea kutathminiwa baada ya kila wiki mbili. Hata hivyo, wabunge na mawaziri wa mikoa hiyo wataendelea kushughulikiwa kijamii, licha ya kuwa wamesimamishwa kazi.