1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Amnesty yaorodhesha ukatili dhidi ya waandamanaji Myanmar

John Juma
12 Machi 2021

Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limesema vyombo vya usalama nchini Myanmar vinatumia silaha za vitani dhidi ya waandamanaji na kufanya mauaji ya kukusudia ambayo yamepangwa na wakuu wao wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/3qWrX
Myanmar | Nonne kniet vor Polizei
Picha: MYITKYINA NEWS JOURNAL/REUTERS

Shirika hilo la haki za binadamu limekusanya video za kikatili zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kunakili kile lilichotaja kuwa ‘mauaji ya nchini kote', wiki kadhaa tangu jeshi lilipochukua madaraka Februari 1.

Mkurugenzi wa idara inayoshughulikia masuala ya dharura katika shirika hilo Joanne Mariner amesema kwenye ripoti hiyo mpya kwamba mbinu zinazotumiwa na jeshi la Myanmar si mpya, bali ni mfululizo wa mauaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa hapo awali.

Soma pia: UN yaliambia jeshi la Myanmar liwache kuwauwa waandamanaji

Ameongeza kwamba hayo si matendo ya maafisa binafsi waliolemewa na kufanya maamuzi yasiyo sahihi, bali ni matendo ya makamanda wa kijeshi ambao tayari wametuhumiwa kufanya jinai dhidi ya ubinadamu kwa kuwatumia wanajeshi na mbinu nyingine za mauaji hadharani.

Myanmar | Proteste nach Militärputsch | Soldaten
Amnesty imevituhumu vikosi vya usalama vya Myanmanr kwa matumizi ya nzito dhidi ya rais.Picha: Kaung Zaw Hein/SOPA Images/ZUMA Wire/picture alliance

Shirika la Amnesty limeonyesha kanda 55 za video zilizorekodiwa kati ya Februari 28 hadi Machi 8, katika miji mingi ya Myanmar, ikiwemo Mandalay na Yangon.

Katika video moja iliyosambazwa kwenye mtandao wa Facebook na iliyorekodiwa Fabruari 28 kusini mashariki mwa mji wa Dawei, mwanajeshi anaonekana akimkabidhi afisa wa polisi aliyekuwa karibu naye bunduki. Afisa huyo wa polisi baadaye anachukua bunduki analenga na kufyatua, kisha maafisa waliokuwa karibu wanashangilia.

Video hiyo iliripotiwa katika mazingira ambayo vilio vya wanawake na watoto vinasikika.

Mariner amesema tukio hilo halionyeshi tu namna ambavyo maafisa hawathamini uhai wa binadamu, kwa kufyatua risasi ya moto dhidi ya waandamanaji, lakini pia linafichua hatua makusudi iliyopangwa ya baadhi ya walinda usalama.

Shirika la Amnesty limeongeza kuwa baadhi ya vitengo vya jeshi vilisajiliwa kutoka katika maeneo yenye machafuko ya makabila ya walio wachache nchini Myanmar, ambako visa vingi vya kikatili vinasemekana kutokea ikiwa ni pamoja na madai ya mauaji ya kiholela ya waandamanaji.

Soma pia:Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laombwa kuweka vikwazo Myanmar

Kanda nyingine ya video iliyosambazwa kwenye mtandao wa Twitter Machi 3 inamuonyesha afisa wa jeshi akimuongoza mwanaume mmoja kuelekea kwenye umati mkubwa wa walinda usalama mjini Yangon.

Mtu huyo anayeonekana kukamatwa haonyeshi ukaidi wowote, lakini afisa aliyekuwa nyuma yake alimpiga risasi na kumuua, kisha kuachwa barabarani na sekunde chache baadaye maafisa hao wanaamua kumburura chini kuondoa mwili wake katika eneo hilo.

Matumizi ya silaha nzito dhidi ya raia

Amnesty International pia imerekodi hatua ya vikosi vya usalama Myanmar kutumia silaha ambazo hazifai kabisa kutumiwa kuwakabili waandamanaji, ikiwemo bunduki za vita, za kulenga shabaha na bunduki ambazo ni nusu automatic yaani za moja kwa moja.

Mariner amesema silaha zilizotumiwa na vikosi vya Myanmar vijulikanavyo pia kama Tatmadaw, zinafichua mbinu za makusudi ambazo pia ni hatari.

Shirika hilo limelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.

Soma pia: UN: Myanmar yaendelea kushuhudia umwagaji damu

Mnamo siku ya Jumatano baraza hilo lilikubaliana kwa pamoja kuhusu tarifa ya kushutumu hatua ya jeshi la Myanmar kutumia machafuko dhidi ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi.

Myanmar | Proteste gegen Militärputsch
Mwandamanaji akifanya ishara ya vidole vitatu wakati wa maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar, Machi 6, 2021.Picha: AP/picture-alliance

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwezi mmoja ambapo wanachama 15 wa baraza hilo ikiwemo China ambayo ni mshirika wa tangu zamani wa Myanmar kuonyesha umoja ambao ni nadra dhidi ya taifa hilo ambalo zamani liliitwa Burma.

Myanmar imekuwa katika hali tete tangu jeshi lilipompindua kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi na kumweka kizuizini, hatua iliyochochea maandamano ya nchi nzima kutaka demokrasia irudishwe.

Takriban watu 2,000 wamekamatwa na idadi ya vifo imepita 60.

Chanzo:AFPE