Al-Shabaab yachinja wanne kwa ″ujasusi″ | Matukio ya Afrika | DW | 07.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Al-Shabaab yachinja wanne kwa "ujasusi"

Wapiganaji wa Al-Shabaab nchini Somalia wamewauwa watu wanne waliowatuhumu kwa kuzifanyia ujasusi serikali za Marekani, Ethiopia na Somalia.

Mauaji hayo yalifanyika katika uwanja wa mji wa Bardhere, ambao ni ngome ya Al-Shabaab katika mkoa wa kusini-magharibi wa Gedo Jumanne jioni, na yametokea wiki moja baada ya Marekani kusema kuwa ilimuuwa mkuu wa ujasusi wa kundi hilo lenye mafungano na mtandao wa Al-Qaeda.

Jaji wa Al-Shabaab alisema kabla ya watu hao wanne kuuawa, kuwa moja wa majasusi hao alilifanyia ujasusi shirika la Marekani la CIA, na kwamba aliwezesha kuuwawa kwa kamanda wa Al-Shabaab.

Kwa mujibu wa jaji huyo mtu mwingine kati ya waliouawa alikuwa akisaidia operesheni za Marekani katika mji wa bandari wa Barawe, ambao ni ngome ya zamani ya kundi hilo walimofurushwa mwaka uliopita na vikosi vya Somalia na Umoja wa Afrika, wakati wengine wawili walituhumiwa kwa kuzifanyia kazi idara za ujasusi za Ethiopia na Somalia.

Wanajeshi wa AMISOM wanaopambana na Al-Shabaab nchini Somalia.

Wanajeshi wa AMISOM wanaopambana na Al-Shabaab nchini Somalia.

Shuhuda wa mji huo Ali Ronow, alisema mamia ya wakaazi walishuhudia utekelezaji wa hukumu hizo, ambapo wanaume hao walifunikwa nyuso zao kwa vitamba na kupigwa risasi za mfululizo mgogoni na walenga shabaha.

Hasira za kuuliwa kwa makamanda wake

Wiki iliyopita Marekani ilifanya shambulizi la angani kwenye eneo la Saacow, lililoko umbali wa kilomita 320 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, na pia katikati mwa mkoa wa Juba, na maafisa wa Somalia walisema mkuu wa ujasusi wa Al-Shabaab Abdishakur Tahlil aliuawa pamoja na wapiganaji wengine wawili.

Kiongozi wa zamani wa Al-Shabaab Ahmed Abdi Godane pia aliuawa katika shambulizi la ndege za Marekani Septemba mwaka 2014.

Katika tukio jengine tofauti, bomu lililoripuka chini ya gari katika mji mkuu Mogadishu limemjeruhi vibaya mhadhiri wa chuo kikuu cha SIMAD, na duru kutoka hospitali ya Madina zimesema alikuwa katika hali mbaya.

Al-Shabaab bado ni tishio

Ingawa Al-Shabaab imefurishwa katika maeneo mengi nchini Somalia, wachambuzi wanasema kundi hilo bado lina uwezo wa kufanya vurugu kwa kutumia mbinu ya kushambulia na kukimbia, na kuzuwia juhudi za serikali inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa kurejesha utulivu katika taifa hilo linalopambana kujiondoa katika mgogoro wa zaidi ya miongo miwili.

Katika eneo lenye utawala wake la Puntland lililoko kaskazini mwa Somalia, rais wake Adiweli Mohamed alisema waasi 20 wa Al-Shabaab na wanajeshi watano waliuawa katika mapigano katika kipindi cha wiki moja iliyopita katika milima ya Galgala.

Msemaji wa kijeshi wa Al-Shabaab Sheikh Abdiasis Abu Musab alisema kundi hilo liliwauwa wanajeshi 23 katika mapambano ya siku tatu na kuongeza kuwa mapigano yalikuwa yanaendelea.

Pamoja na mashambulizi nchini Somalia, Al-Shabaab pia imefanya mashambulizi katika nchi jirani ya Kenya, ambayo imetuma wanajeshi kwenye vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe.
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com