1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yaahidi kukomesha ghasia dhidi ya wahamiaji

Sylvia Mwehozi AFP, Reuters, dpa
Imechapishwa 22 Juni 2026ilisahihishwa mwisho 25 Juni 2026

Rais Cyril Ramaphosa amesema serikali haitavumilia vitendo vya kuvuruga amani wakati wa maandamano yaliyopangwa Juni 30 dhidi ya wahamiaji wasio na vibali.

https://p.dw.com/p/5FqEk
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa ameahidi kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa watakaokiuka amaniPicha: Ignacio Lopez Isasmendi/ZUMA/picture alliance
Ruka sehemu inayofuata Unachohitaji kujua

Unachohitaji kujua

  • Mashirika ya misaada na mataifa ya Magharibi yanaonya kuwa wanamgambo wa RSF wanajiandaa kushambulia mji wa Al-Obeid
  • DRC yahitaji vituo zaidi vya Ebola huku vifo vikikaribia 300
  • Afrika Kusini yaahidi kukomesha ghasia dhidi ya wahamiaji
  • Kenya yatia saini mkataba wa dola bilioni 1.2 kupanua uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA
  • Shabiki wa DR Congo anayejifanya sanamu hai ya Lumumba atinga Kombe la Dunia
  • Libya ya mashariki yapiga marufuku raia wa nchi nne kuingia nchini

    Karibu katika blogu hii maalum inayomulika taarifa muhimu za Afrika:
Ruka sehemu inayofuata Hofu ya shambulio kubwa la RSF yatanda mji muhimu wa Sudan
25 Juni 2026

Hofu ya shambulio kubwa la RSF yatanda mji muhimu wa Sudan

Sudan El-Obeid 2025 | Abdel Fattah al-Burhan wa Jeshi la Sudan (SAF) baada ya ushindi dhidi ya wanamgambo wa RSF
Mji wa Al-Obeid ulikombolewa na Jeshi la Sudan kutoka mikononi mwa RSF mnamo Septemba 2025.Picha: Mohamed Sid Ahmed/Xinhua/picture alliance

Hatari ya kuongezeka kwa mapigano nchini Sudan imeongezeka baada ya taarifa kwamba wanamgambo wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) wanajiandaa kufanya shambulio kubwa dhidi ya mji wa kimkakati wa Al-Obeid, ulioko jimbo la North Kordofan.

Msemaji wa Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC), Elias Ata, amesema takribani watu 500,000 wamekwama ndani ya mji huo, ambao kwa wiki kadhaa umekuwa ukikumbwa na mashambulizi ya karibu kila siku ya droni za RSF.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi kadhaa za Ulaya, zikiwemo Ujerumani, zimeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali hiyo. Katika taarifa ya pamoja, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway na Uingereza zimeonya kuwa kuna dalili za kuaminika za shambulio linaloweza kuanza wakati wowote.

Nchi hizo zimesema dunia isiruhusu kurudiwa kwa mauaji yaliyotokea mwaka jana mjini El Fasher, ambako Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 6,000 waliuawa, huku wataalamu wa Yale Humanitarian Lab wakikadiria idadi ya vifo kufikia 60,000.

Kwa mujibu wa NRC, mashambulizi ya mara kwa mara tayari yameharibu kwa kiasi kikubwa huduma za umeme, maji na mafuta katika mji wa Al-Obeid, huku bidhaa muhimu zikizidi kupungua.

Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Marekani wamesema wamezungumza kwa simu na uongozi wa RSF wakimtaka kiongozi wake, Mohamed Hamdan Dagalo, kutoshambulia mji huo. Vyombo vinavyohusishwa na RSF vimedai Dagalo ameihakikishia Marekani usalama wa raia na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikishwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Plan International nchini Sudan, Mohamed Kamal, amesema iwapo RSF itauteka mji wa Al-Obeid, vita vinaweza kubadilika kabisa mkondo wake. Alisema jimbo la North Kordofan ni muhimu kwa sababu ndilo makutano ya njia kuu za usafiri nchini, huku Al-Obeid ikitajwa kuwa lango la kuelekea mji mkuu, Khartoum.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

https://p.dw.com/p/5G4rX
Ruka sehemu inayofuata Vituo zaidi vya afya vinahitajika huku idadi ya vifo vya Ebola nchini Congo ikikaribia 300
25 Juni 2026

Vituo zaidi vya afya vinahitajika huku idadi ya vifo vya Ebola nchini Congo ikikaribia 300

DW-Mahojiano | Ujerumani Berlin 2026 | Dkt. Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, wakati wa mahojiano
Mkuu wa Africa CDC Dr. Jean Kaseya amesema kuna haja ya haraka ya kujenga vituo zaidi vya matibabu na kuongeza vitanda vya wagonjwaPicha: DW

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inahitaji vituo zaidi vya matibabu na kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa Ebola, wakati idadi ya vifo kutokana na mlipuko huo ikitarajiwa kuzidi 300 katika siku chache zijazo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afrika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Jean Kaseya, amesema hadi sasa kuna visa 1,118 vilivyothibitishwa vya Ebola nchini humo, huku watu 291 wakiwa wamefariki dunia.

Kaseya amesema ingawa mlipuko huo bado haujafikia kilele chake, asilimia 95 ya vitanda vya wagonjwa tayari vimejaa, hali inayolazimu ujenzi wa vituo vipya vya matibabu na kuongeza nafasi za kulaza wagonjwa.

Kwa mujibu wa Africa CDC, kasi ya maambukizi imezua wasiwasi mkubwa, kwani hakuna mlipuko mwingine wa Ebola barani Afrika uliowahi kufikisha idadi hiyo ya visa vilivyothibitishwa ndani ya wiki tano za kwanza.

Ethiopia Addis Ababa 2026 | Dkt. Mekdes Dhaba na Dkt. Jean Kaseya katika makao makuu ya Africa CDC
Kwa mujibu wa Africa CDC, kasi ya maambukizi imezua wasiwasi mkubwa, kwani hakuna mlipuko mwingine wa Ebola barani Afrika uliowahi kufikisha idadi hiyo ya visa vilivyothibitishwa ndani ya wiki tano za kwanzaPicha: Eskinder Firew/DW

Wakati huo huo, majaribio ya dawa za kutibu Ebola yanatarajiwa kuanza wiki ijayo mjini Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri ambalo limeathiriwa zaidi na mlipuko huo.

Kaseya amesema dawa ya kinga ya Remdisivir, iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa wazalishaji kutoka Marekani na Misri, tayari imewasili nchini DRC na itaanza kufanyiwa majaribio. Dawa hiyo hutolewa kwa watu waliokwishagusana na virusi ili kupunguza hatari ya kuugua. Aidha, dawa nyingine kutoka Marekani, MBP134, inatarajiwa kuwasili katika siku chache zijazo.

Mlipuko wa sasa, ulioripotiwa kwa mara ya kwanza katikati ya mwezi Mei, unasababishwa na aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola, ambayo kwa sasa haina chanjo wala tiba maalumu iliyoidhinishwa.

Katika hatua nyingine, serikali ya DRC imeamuru karantini ya siku 21 kwa watu wanaosafiri kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Ebola kwenda sehemu nyingine za nchi au nje ya nchi. Serikali imesema hatua hiyo inalenga kupunguza maambukizi na kurahisisha ufuatiliaji wa watu walioweza kuathiriwa na virusi.

https://p.dw.com/p/5G4qx
Ruka sehemu inayofuata Rais Cyril Ramaphosa amesema serikali haitavumilia vitendo vya kuvuruga amani wakati wa maandamano yaliyopangwa Juni 30
25 Juni 2026

Rais Cyril Ramaphosa amesema serikali haitavumilia vitendo vya kuvuruga amani wakati wa maandamano yaliyopangwa Juni 30

DW-Eigendreh | Afrika Kusini Durban 2026 | Emmanuel Kachingwe akisubiri kusafirishwa kutoka Afrika Kusini
Emmanuel Kachingwe, raia wa Malawi, akisubiri usafiri wa kuondoka Afrika Kusini baada ya makundi ya wenyeji kuwataka wahamiaji wa Kiafrika kuondoka kabla ya Juni 30Picha: Thuso Khumalo/DW

Serikali ya Afrika Kusini imesema iko tayari kukabiliana vikali na vitendo vyovyote vya vurugu wakati wa maandamano dhidi ya wahamiaji yaliyopangwa kufanyika Juni 30, huku Rais Cyril Ramaphosa akiahidi kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa watakaokiuka amani.

Makundi yanayoongozwa na raia yamewataka wahamiaji wasio na vibali kuondoka nchini ifikapo Juni 30 na yamehamasisha maandamano ya kitaifa kupinga uhamiaji haramu. Wito huo umeibua hofu ya kurejea kwa mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni yaliyowahi kusababisha vifo katika miaka iliyopita.

Akilihutubia bunge, Ramaphosa alisema vikosi vya usalama vimejiandaa kikamilifu kuhakikisha siku hiyo inaendelea kwa utulivu na kwamba yeyote atakayesababisha machafuko atakabiliwa na nguvu ya sheria.

Raia wa Ghana warudi nyumbani kutoka Afrika Kusini

Polisi tayari wametangaza kuimarisha ulinzi kote nchini, huku serikali ikifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali, wakiwemo wa Nyumba ya Kifalme ya Wazulu, ili kuzuia kuzuka kwa vurugu.

Katika wiki za karibuni, machafuko yanayohusishwa na chuki dhidi ya wahamiaji yamesababisha vifo vya watu wasiopungua watatu kwa mujibu wa mamlaka za Afrika Kusini, huku Msumbiji ukisema raia wake watano wameuawa. Wakati huo huo, maelfu ya wahamiaji kutoka Ghana, Malawi, Msumbiji na Nigeria wameanza kurejea kwa hiari makwao, huku kambi za muda zikiongezeka katika miji ya Durban na Johannesburg wakati wakisubiri usafiri.

Afrika Kusini imekuwa kivutio kikubwa cha wahamiaji wanaotafuta ajira, licha ya kiwango cha ukosefu wa kazi kufikia karibu asilimia 32. Serikali na vyama vikubwa vya wafanyakazi vinasema wahamiaji wanageuzwa mbuzi wa kafara kwa matatizo ya kiuchumi na uhalifu, wakati baadhi ya wanasiasa wakilitumia suala hilo kujipatia uungwaji mkono kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu.

https://p.dw.com/p/5G4qO
Ruka sehemu inayofuata Burundi yaunga mkono juhudi za amani mashariki mwa DR Congo
Imechapishwa 24 Juni 2026ilisahihishwa mwisho 24 Juni 2026

Burundi yaunga mkono juhudi za amani mashariki mwa DR Congo

Kongo 2026 | Ziara ya Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye kwa Rais Félix Tshisekedi
Ndayishimiye alikutana na rais Felix Tshisekedi mjini Kinshasa ambapo walikubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa yao.Picha: Giscard Kusema

Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, ametoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kikanda ili kumaliza ukosefu wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza mjini Kinshasa katika mkutano wa pamoja na Rais wa DR Kongo, Félix Tshisekedi, Ndayishimiye amesema anaunga mkono mazungumzo ya amani yanayoendelea Washington na Doha pamoja na juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Waafrika.

Amesisitiza dhamira ya Burundi ya kuendelea kuchangia amani na utulivu katika eneo hilo, ambako mapigano kati ya makundi yenye silaha na waasi wa AFC/M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yanaendelea.

Marais hao wawili pia wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi zao, huku kikao cha Tume ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Burundi na DR Kongo kikitarajiwa kufanyika mwezi Septemba mjini Bujumbura.

Burundi kwa sasa ina wanajeshi waliotumwa mashariki mwa DR Kongo kushirikiana na jeshi la Kongo katika mapambano dhidi ya waasi wa AFC/M23.

https://p.dw.com/p/5G0ZB
Ruka sehemu inayofuata Niger yawasilisha rasmi ombi la kujiondoa ICC
24 Juni 2026

Niger yawasilisha rasmi ombi la kujiondoa ICC

Niger imewasilisha rasmi ombi la kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Kwa mujibu wa ripoti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alipokea barua ya Niger tarehe 18 Juni, hatua inayomaanisha kuwa kujiondoa huko kutaanza rasmi kutekelezwa Juni 18 mwaka 2027 kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.

Serikali ya Niger imesema kwamba licha ya ICC kuanzishwa kwa matumaini makubwa ya kuendeleza haki na amani, mahakama hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa.

Niger ni mwanachama wa Muungano wa Mataifa ya Sahel, AES, unaojumuisha pia Mali na Burkina Faso, ambao uliwahi kutishia kujiondoa kwa pamoja kutoka ICC mwaka jana.

Tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo mwaka 1998, ni nchi mbili pekee zilizowahi kujiondoa rasmi, ambazo ni Burundi na Ufilipino.

https://p.dw.com/p/5G0Yf
Ruka sehemu inayofuata RSF yakaza udhibiti wa viongozi washirika kufuatia wimbi la kujiengua
24 Juni 2026

RSF yakaza udhibiti wa viongozi washirika kufuatia wimbi la kujiengua

Kikosi cha wapiganaji cha Rapid Support Force, RSF, cha nchini Sudan kimeripotiwa kuweka masharti mapya ya usafiri kwa viongozi wa kisiasa na maafisa wanaoshirikiana nacho katika maeneo kinayoyadhibiti.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Darfur24, viongozi hao sasa wanatakiwa kupata kibali maalum kabla ya kusafiri au kuondoka katika maeneo yao ya kazi.

Hatua hiyo inadaiwa kuamriwa na kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, kufuatia ongezeko la matukio ya viongozi wa kisiasa na kijeshi kujiondoa katika kundi hilo na kujiunga na jeshi la Sudan.

Ripoti hiyo pia imesema baadhi ya maafisa wa utawala unaoungwa mkono na RSF katika jimbo la Darfur Kusini walikamatwa wakituhumiwa kujaribu kuelekea Sudan Kusini ili kujiunga na upande wa jeshi la serikali.

RSF imekabiliwa na mfululizo wa kujiengua kwa washirika wake katika miezi ya karibuni, jambo linaloonekana kuongeza shinikizo kwa kundi hilo wakati vita vya Sudan vikiendelea.

Sudan Khartoum 2022 | Mohamed Hamdan Dagalo akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari wa Baraza la Mpito la Uongozi wa Sudan
Inaelezwa kuwa agizo la maafisa kutoondoka maeneo yao ya kazi kibali limetolewa na mkuu wa RSG Mohamed Hamdan Dagalo, kufuatia wimbi la washirika wa kundi hilo kujienguaPicha: Mahmoud Hjaj/picture alliance
https://p.dw.com/p/5G0XZ
Ruka sehemu inayofuata Kenya yatia saini mkataba wa dola bilioni 1.2 kupanua JKIA
24 Juni 2026

Kenya yatia saini mkataba wa dola bilioni 1.2 kupanua JKIA

 Nairobi | Uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA
Uwanja wa JKIA kwa sasa unahudumia abiria milioni 7.5, na serikali inatzamia kuongeza idadi hiyo hadi milioni 22 kwa mwakaPicha: Billy Mutai/AA/picture alliance

Serikali ya Kenya imetia saini mkataba wa shilingi bilioni 154 za Kenya, sawa na dola bilioni 1.2 za Marekani, na kampuni ya China Road and Bridge Corporation kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA, mjini Nairobi.

Waziri wa Uchukuzi, Davis Chirchir, amesema mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa uwanja huo kuhudumia abiria hadi milioni 22 kwa mwaka kutoka milioni 7.5 za sasa.

Kazi zitahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, kuboresha miundombinu iliyopo pamoja na kuimarisha huduma za ndani na nje ya uwanja huo.

Mradi huo ulikuwa umesitishwa mwaka jana baada ya Kenya kufuta makubaliano ya awali na kampuni ya Adani Group ya India.

Kenya inataka kuendelea kuwa kitovu kikuu cha usafiri wa anga katika kanda ya Afrika Mashariki wakati nchi jirani kama Ethiopia na Rwanda zikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika viwanja vya ndege vya kisasa ili kuvutia mashirika ya ndege na wasafiri.

https://p.dw.com/p/5G0Vd
Ruka sehemu inayofuata 'Lumumba wa Goma' atinga Kombe la Dunia kuisapoti DR Kongo
24 Juni 2026

'Lumumba wa Goma' atinga Kombe la Dunia kuisapoti DR Kongo

Kombe la Dunia 2026 | Kundi K | Colombia dhidi ya DR Congo | Shabiki wa DR Congo aliyejivisha sura ya Patrice Lumumba
Michel Nkuka Mboladinga, maarufu kama "Lumumba Vea", akiiunga mkono DR Kongo wakati wa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya ColombiaPicha: Natacha Pisarenko/AP Photo/dpa/picture alliance

Shabiki maarufu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Michel Nkuka Mboladinga , hatimaye ameonekana katika Kombe la Dunia, akiwa amevalia mavazi ya rangi za bendera ya nchi yake na kujifanya sanamu hai ya Patrice Lumumba.

Mboladinga, anayefahamika kama Lumumba Vea kutokana na kufanana kwake na kiongozi huyo wa uhuru wa Kongo, alihudhuria mechi ambayo DR Congo ilifungwa bao 1-0 na Colombia. Alikosa mechi ya kwanza dhidi ya Portugal kutokana na masharti ya karantini ya Ebola.

Akiwa nyuma ya benchi la DR Kongo, alisimama bila kusogea juu ya jukwaa dogo, mkono wake wa kulia ukiwa juu, kama alivyofanya wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika. Baada ya mechi, alikataa kuhojiwa, lakini alitabasamu na kutikisa kichwa alipoulizwa kama alikuwa na furaha kufika Kombe la Dunia.

Mboladinga amekuwa maarufu mitandaoni kwa kumuenzi Patrice Lumumba, kiongozi aliyesaidia kumaliza utawala wa kikoloni wa Ubelgiji nchini Kongo mwaka 1960, kabla ya kuuawa mwaka mmoja baadaye wakati wa mzozo wa kisiasa katika jimbo la Katanga.

Kombe la Dunia 2026 | Kundi K | Colombia dhidi ya DR Congo | Shabiki aliyevalia mavazi ya Patrice Lumumba akiishabikia DR Kongo
Shabiki wa Kongo Michel Nkuka Mboladinga, aliyevalia mavazi ya shujaa wa uhuru Patrice Lumumba, akionyesha hisia kabla ya mechi ya Kundi K ya Kombe la Dunia kati ya Colombia na DR Congo mjini ZapopanPicha: Natacha Pisarenko/AP Photo/dpa/picture alliance
https://p.dw.com/p/5G0RP
Ruka sehemu inayofuata Libya Mashariki yapiga marufuku raia wa Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia kuingia nchini
24 Juni 2026

Libya Mashariki yapiga marufuku raia wa Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia kuingia nchini

Mamlaka za mashariki mwa Libya zimetangaza marufuku ya kuingia nchini kwa raia wa Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia, hatua inayoonekana kulenga kupunguza idadi ya wahamiaji wanaotumia pwani ya Libya kuelekea Ulaya.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku, serikali hiyo ilisema raia wa nchi hizo nne hawataruhusiwa kuingia Libya kupitia mipaka ya nchi kavu, baharini au viwanja vya ndege. Hata hivyo, wanadiplomasia pamoja na wafanyakazi wa sekta za afya na elimu hawataathiriwa na marufuku hiyo.

Hatua hiyo imekuja wakati mvutano ukiongezeka katika maeneo ya mashariki na magharibi mwa Libya kuhusu makazi ya wakimbizi kutoka mataifa mengine. Shirika la Amnesty International limesema maelfu ya wahamiaji wamekamatwa katika operesheni za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Libya ina zaidi ya wahamiaji na wakimbizi 900,000, huku Wasudan wakiongoza kwa idadi. Wengi wao hutumia Libya kama njia ya kujaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya.

Libya imekuwa katika hali ya mgawanyiko wa kisiasa tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa zamani, Muammar Gaddafi, mwaka 2011. Kwa sasa nchi hiyo ina tawala mbili zinazoshindana, moja ikiwa magharibi na nyingine mashariki mwa nchi.

Tigray: Safari ya kutoka kambini hadi utumwani Libya

https://p.dw.com/p/5G0P3
Ruka sehemu inayofuata Waasi wa M23 waimarisha masharti ya usafiri kutokana na Ebola
24 Juni 2026

Waasi wa M23 waimarisha masharti ya usafiri kutokana na Ebola

Mamlaka za waasi wa AFC/M23 wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeimarisha masharti ya usafiri kutoka maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mlipuko wa Ebola, hatua inayolenga kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, madereva wanaotoka miji ya Beni, Butembo na jimbo la Ituri hawataruhusiwa kuingia katika maeneo yanayodhibitiwa na AFC/M23. Kampuni za usafiri pia zimetakiwa kutumia madereva wawili kwa kila gari, huku magari yakifanyiwa usafishaji maalum kabla ya kuendelea na safari.

Hatua hiyo inakuja wakati Kongo ikikabiliana na mlipuko wake wa 17 wa Ebola, ambao hadi sasa umehusisha zaidi ya visa 1,000 na kusababisha vifo zaidi ya 260.

Wakati huo huo, Uganda imethibitisha kisa kipya cha Ebola, cha kwanza katika zaidi ya wiki mbili. Mamlaka zimesema mgonjwa huyo ni raia wa Kongo, hali inayozidisha hofu ya maambukizi kuvuka mipaka.

Katika kukabiliana na tishio hilo, Uganda na Kongo zimezindua mpango wa siku 90 wa kuanzisha vituo vya pamoja vya maabara na matibabu katika eneo la Aru, jimboni Ituri, ili kuimarisha juhudi za kudhibiti mlipuko huo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bunia 2026 | Wahudumu wakibeba jeneza la mtu anayeshukiwa kufariki kutokana na Ebola
Mlipuko wa sasa wa Ebola unahusishwa na vifo vya zaidi ya watu 260 mpaka sasaPicha: Gradel Muyisa Mumbere/REUTERS
https://p.dw.com/p/5G0OF
Ruka sehemu inayofuata Watu wenye itikadi kali waua wakulima 11 kaskazini mwa Nigeria
22 Juni 2026

Watu wenye itikadi kali waua wakulima 11 kaskazini mwa Nigeria

Watu wanaodhaniwa kuwa wanamgambo wa itikadi kali wamewaua wakulima 11 katika mashambulizi mawili tofauti yaliyotokea mwishoni mwa wiki kaskazini mashariki mwa Nigeria, kwa mujibu wa kundi linalopambana na wanamgambo.

Maeneo ya kaskazini na katikati mwa Nigeria yanaendelea kukumbwa na mashambulizi kutoka kwa makundi ya wanajihadi pamoja na makundi ya wahalifu yanayojulikana na wakazi wa eneo hilo kama “majambazi”. Makundi haya yanajihusisha zaidi na utekaji nyara kwa ajili ya fidia na wizi wa mifugo.

Wahalifu hao huwatoza wakulima “kodi” ili kuwaruhusu kufikia mashamba yao wenyewe, na huwatesa au kuwalenga wale wanaokataa kulipa. Hali hii imekuwa mzigo mkubwa kwa wakazi wengi wa vijijini.

Baadhi ya wakulima wamesema tayari walilazimika kulipa fedha nyingi ili kuwaokoa ndugu zao waliotekwa, na sasa hawana uwezo wa tena kulipa tozo hizo. Kutokana na hali hiyo, wengine wameanza kuyakimbia maeneo ya vijijini na kwenda mijini au sehemu zilizo salama zaidi.

Nigeria Maiduguri 2026 | Gari la polisi likifanya doroa sokoni baada ya milipuko mnamo mwezi Machi 2026
Gari la polisi sokoni huko Maiduguri mnamo Machi 17, 2026 siku moja baada ya milipukoPicha: AFP

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linaonya kuwa kupungua kwa shughuli za kilimo kunakosababishwa na hali hii kunaweza “kuongeza umaskini na ukosefu wa chakula” katika nchi ambayo tayari mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa kila siku.

Katika tukio la Jumamosi, washambuliaji waliwakusanya wakulima saba katika kijiji cha Kuwawu, jimbo la Borno, na kuwaua kwa kuwakata koo, kwa mujibu wa kundi linalopambana na wanamgambo. Walisema mashambulizi hayo yamehusishwa na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu ukanda wa Afrika Mgharibi (ISWAP), kundi lililojitenga na Boko Haram.

Mashambulizi hayo yanaongeza hofu na kuimarisha hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo, huku juhudi za serikali na vikosi vya usalama zikiendelea kukabiliana na makundi hayo yenye silaha.

 

https://p.dw.com/p/5FqZY
Ruka sehemu inayofuata Jumla ya watu 254 wafariki kwa Ebola nchini Kongo
22 Juni 2026

Jumla ya watu 254 wafariki kwa Ebola nchini Kongo

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Congo, jumla ya watu 100 wamepona tangu mlipuko huo utangazwe Mei 15 katika jimbo la Ituri. Takriban wagonjwa 365 bado wapo hospitalini au kwenye vituo vya kujitenga.

Mlipuko huu unasababishwa na aina adimu ya virusi vya Bundibugyo, ambayo haina chanjo wala tiba maalum kwa sasa. Katika mwezi wake wa kwanza, tayari umeonekana kuwa mmoja wa milipuko mikubwa zaidi.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bunia 2026 | Kuzikwa kwa mtoto aliyefariki kwa Ebola
Mazishi ya mtoto aliyefariki kwa Ebola mjini BuniaPicha: Benediction Murhabazi/AFP

Maafisa wa afya wanakiri kuwa huenda kuna visa vingi zaidi ambavyo bado havijatambuliwa, huku kilele cha mlipuko kikiwa bado hakijafikiwa.

Ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa umefikia asilimia 55 tu, jambo linalotia wasiwasi mamlaka za afya. Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha kuzuia na kupambana na magonjwa cha Africa CDC Dkt. Jean Kaseya, amesema ukitaka kudhibiti mlipuko hususan mlipuko wa Ebola, "ni lazima kufahamu chanzo chake kwa maana ya mgonjwa wa kwanza."

Hadi sasa, bado haijafahamika nani alikuwa mgonjwa wa kwanza na zaidi ya watu 35,000 waliokuwa wamewasiliana na walioambukizwa bado hawajafuatiliwa kikamilifu.
 

https://p.dw.com/p/5FqKr
Onesha matokeo zaidi