1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
6 Oktoba 2017

wiki hii, kati ya mada zilizoandikwa na magazeti ya Ujerumani ni kuhusu mvutano unaotokota nchini Cameroon, juhudi za Nigeria za kujikwamua kiuchumi na kitendawili cha fasihi simulizi juu ya historia ya bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/2lOmr
Nigeria Präsident Buhari Rückkehr
Picha: picture-alliance/Nigeria State House/S. Aghaeze

Kwa  muda mrefu ni mambo matatu ambayo  yamekuwa yanajitokeza mtu alipozungumzia juu ya  Nigeria. Mambo hayo ni mafuta, ufisadi na Boko Haram. Mambo hayo  matatu yanachanganyika katika kuathiri fursa  za siku za  usoni kwa nchi hiyo. Mafuta, bidhaa inayoiingizia Nigeria karibu asilimia  90 ya  fedha za kigeni, yamepungua bei kwenye soko  la  dunia. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba  tangu kuangukua kwa bei ya mafuta, uchumi wa Nigeria  umeshuka. Gazeti hilo linasema changamoto kubwa inayoikabili Nigeria ni kutafuta njia ya kupunguza kutegemea mafuta na kujaribu kuunyambua uchumi wake.  Na ili kuwavutia  wawekezaji vitega uchumi rais Muhammadu Buhari ameahidi  kupambana vikali dhidi ya ufisadi na pia magaidi wa kundi la Boko Haram.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema sehemu ya nchi hiyo inataka kujitenga, lakini serikali haitaki mchezo. Gazeti hilo linaeleza kuwa wanaharakati wa sehemu ya kusini mwa Cameroon iliyokuwa chini ya usimamizi wa wakoloni wa Uingereza wamejitangazia uhuru ili kujitenga na Cameroon inayotawaliwa na rais Paul Biya anayetokea sehemu ya watu wanaotumia  lugha  ya kifaransa. Serikali ya Rais Biya haikuchuchelewa kuchukua hatua madhubuti ili kuuzima uasi. Serikali hiyo  iliufunga mpaka wake na Nigeria na kutangaza amri ya kutotoka nje. Mikutano ya watu zaidi ya wanne ilipigwa  marufuku na usafiri  baina ya miji mikubwa ulisimamishwa.

Gazeti hilo la die tageszeitung  linakumbusha  kwamba mnamo miaka ya 90 yalifanyika  maandamano makubwa dhidi ya rais Paul Biya anayetawala Cameroon tangu mwaka wa1982. Watu wa kusini mwa Cameroon waliokuwa chini ya utawala wa Waingereza  wanasema wanakandamizwa na  serikali  kuu inayodhibitiwa  na wale wanaotumia lugha ya kifaransa.

Berliner Zeitung

Nalo gazeti la Berliner Zeitung wiki hii linatema sumu kwa viongozi kadhaa wa barani Afrika na watoto wao linasema kwamba watawala fulani wa Afrika wanajulikana duniani kwa  tabia ya kutojali haki za binadamu, wanaiba mali za umma na  wanang'ang'ania  madaraka mpaka wanaanguka kwenye  mimbari. Ni sawa kabisa kusema kwamba watawala hao ndio  wanaosababisha bara la Afrika likwame lakini watoto wao  wanavuka mipaka.  Mfano ni Teodorin Obiang Mangae mtoto  wa rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro  Obiang. Mtoto huyo  anaouonyesha utajiri wake hadharani, miongoni mwa wanaserere wake wa kuchezea ni boti ya kifahari yenye   thamani ya dola milioni 150 pamoja na msururu wa magari  aina ya  Limousine nyumba ya kifahari iliyopo  mjini Paris yenye thamani ya Euro milioni mia moja. 

Gazeti hilo la Berliner  Zeitung pia linatufahamisha  juu ya mwanamke tajiri kuliko  wengine wote barani Afrika, Isabel dos Santos binti ya aliekuwa rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos aliyetawala  Angola kwa muda wa miaka 38. Berliner Zeitung limeandika kuwa dada huyo Isabel dos Santos aliutumia utawala wa baba yake  kujijengea utajiri wenye thamani ya dola bilioni 3.5  na yeye hivi sasa ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya mafuta ya Angola Sonangol.Isabel mwenye umri wa miaka 44 anashikilia kazi ya pili iliyo muhimu kabisa katika nchi hiyo ya pili kwa utajiri wa mafuta barani Afrika huku kaka yake Jose akiuongoza mfuko wa fedha wa serikali ya Angola (Fundo Soberano de Angola). 

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman