Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 18.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani ,wiki hii pia yameandika juu ya Simba Cecil, kampuni za teknolojia za kisasa nchini kenya na juu ya Jenerali Karake wa Rwanda

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatufahamisha kwamba mahakama ya mjini London imemwachia Jenerali Karake baada ya kuifutilia mbali kesi iliyohusu kumpeleka Uhispania. Serikali ya Rwanda imetoa shukurani zake juu ya kuachiwa mwananchi wake lakini imesema Karake alikamatwa kwa makosa.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatuarifu kwamba Jenerali Karake alikamatwa mjini London mnamo mwezi wa Juni baada ya Uhispania kutoa hati ya kisheria ili akamatwe ,kutokana na kumtuhumu kuhusika na mauaji ya raia wa Uhispania waliokuwapo nchini Rwanda mnamo miaka ya nyuma.

Watalii waruhusiwa kuwinda tena Zimbabwe

Gazeti la "Berliner" linasema watalii bado wanaendelea kuwinda nchini Zimbabwe hata baada ya kuuliwa simba maarufu Cecil. Gazeti hilo linaeleza .Watalii wanaruhusiwa kuwinda tena nchini Zimbabwe kwa sababu kila mtu anataka kuujaza mfuko wake.

Gazeti la "Berliner" limemnukulu Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akilaani kuuliwa Simba ,Cecil. Mugabe amesema watu wa Zimbabwe walishindwa kumlinda shujaa wao Cecil. Lakini gazeti la "Berliner " linamkumbusha Rais Mugabe kwamba ,kila mwaka simba zaidi ya 40 wanauliwa nchini Zimbabwe.

Gazeti hilo linasema , katika siku hiyo hiyo ambapo Rais Mugabe alizitoa shutuma juu ya kuuliwa Cecil, amri ya kuwakataza watalii kuwinda iliondolewa. Gazeti la "Berliner " linasema shughuli ya uwindaji wa nyara inayofanywa na watalii kutoka nje , inaingiza dola zaidi ya Milioni 200 kila mwaka kwa nchi 23 za kusini mwa jangwa la Sahara.

Gazeti la Berliner linakumbusha katika makala yake kuwa mnamo miaka ya 70 idadi ya ndovu iliongezeka nchini Kenya ,ambako uwindaji ulifanyika kwa kudhibitiwa.

Lakini gazeti la NZZ linakumbusha kwamba walikuwapo ndovu Milioni tano barani Afrika hadi mnamo miaka ya 40. Lakini kutokana na ujangili sasa wamebakia tembo nusu Milioni tu!

Gazeti la NZZ limearifu kwamba wiki iliyopita kilogramu 262 za pembe za ndovu zilikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Zürich nchini Uswisi.Mzigo huo ulikuwa unatokea Tanzania na safari yake ilikuwa inaishia katika nchi mojawapo ya barani Asia. Gazeti la NZZ linaeleza, kwa nini majangili wanavutiwa na biashara hiyo haramu yakuuza vipusa. Kilogramu moja inanunuliwa kwa dola hadi 2000.

Silicon Savanna

Gazeti la " Frankfutrer Allgemeine" wiki hii limendika juu ya kampuni za tekilonojia za kisasa zinazochipuka kama uyoga nchini Kenya. Gazeti hilo linaarifu kwamba baada ya mafanikio ya "Mpesa" na "Ushahidi-App, kampuni chungutele, za tekinolojia ya tasnia ya habari, zimeanzishwa nchini Kenya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Gazeti hilo linasema Kenya inadhamiria kushindana na Afrika Kusini, inayoongoza barani Afrika ,katika maendeleo ya tekinolojia za kisasa. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema watu sasa wanazungumzia juu ya Silicon Savannah ya nchini Kenya kama jinsi walivyozungumzia juu ya Silicon Valley ya California.

Kwa mujibu wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" serikali ya Kenya inatumai , tekinolojia za kisasa zitachangia hadi asilimia 10 katika pato jumla la taifa kuanzia mwaka wa 2017. Gazeti hilo linafahamisha kwamba serikali ya Kenya inakusudia kugawa Laptop M.1.3 mashuleni.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limefahamisha kuwa Kenya inaekeza Euro, Bilioni 13 kwa ajili ya mradi maarufu wa mjini Konza- "Konza Techno City, unaotarajiwa kuleta maalfu ya nafasi za ajira katika siku za usoni.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Daniel Gakuba