1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya8 Februari 2015

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya juhudi za kupambana na magaidi wa Boko Haram na juu ya mpango wa tajiri Bill Gates wa kuwasaidia masikini

https://p.dw.com/p/1EXqn
Wanajeshi wa Chad wapambana na magaidi wa Boko Haram
Wanajeshi wa Chad wapambana na magaidi wa Boko HaramPicha: AFP/Getty Images/M. Medina

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya harakati za kupambana na magaidi wa Boko Haram.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba wakati viongozi wa Umoja wa Afrika walipokuwa wanajadiliana juu ya kukiunda kikosi maalamu cha kupambana na magaidi hao, majeshi ya Chad tayari yalikuwamo kwenye uwanja wa mapambano kuwakabili Boko Haram.

Gazeti la "die tageszeitung" linaeleza kwamba katika azimio lao viongozi wa nchi za Afrika wameridhia kuundwa kikosi cha kimataifa cha wanajeshi 7500 watakaopelekwa kupambana na magaidi wa Boko Haram .Wanajeshi hao watatoka Nigeria,Chad,Cameroon,Niger na Benin.

Lakini gazeti la"die tageszeitung" linasema Umoja wa Afrika upo hatua moja nyuma ya Chad, kwani wanajeshi wa nchi hiyo walianza kupambana na magaidi wa Boko Haram tokea tarehe 17 mwezi wa Januari. Na kwa mujibu wa taarifa iliyokaririwa na gazeti hilo wapiganaji wa Boko Haram 200 waliuliwa na jeshi la Chad wiki iliyopita.

Kampeni za uchaguzi wa Rais nchini Nigeria zakumbwa na ghasia

Gazeti la "die tageszeitung"wiki hii pia limeandika juu ya kampeni za uchaguzi wa Rais nchini Nigeria na linatufahamisha kuwa mpaka sasa majimbo ya mafuta nchini Nigeria yalikuwa ngome kuu za wananchi wanaoiunga mkono serikali.

Lakini sasa hali imebadilika. Katika majimbo hayo, ambako Rais Goodluck Jonathan anatokea ,kampeni za uchaguzi zilikumbwa na ghasia hivi karibuni. Palikuwa na taarifa za mashambulio ya mabomu katika jimbo la Rivers. Gazeti la "die tageszeitung" limearifu kwamba mashambulio hayo yalifanyika baada ya mjumbe wa muungano wa vyama vya upinzani APC kuonekana kuwa anaongoza katika kura za maoni.

Ebola yaathiri utalii

Gazeti la "Handelsblatt" wiki hii limeandika juu athari za maradhi ya Ebola katika biashara ya utalii. Gazeti hilo linasema, ile hofu tu juu ya maradhi hayo inazigharimu nchi za Afrika fedha nyingi. Gazeti hilo linaeleza kwamba maradhi hatari ya Ebola yamewatia hofu watalii ingawa nchi nyingi zenye vivutio vya utalii zipo mbali na maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo.

Wamiliki wa kampuni za kitalii wamearifu kwamba idadi ya watalii wanaoenda katika nchi kama Kenya imepungua sana. Sababu ni kwamba serikali za nchi za magharibi ziliwashauri watu katika nchi hizo, kuepuka safari za kuenda barani Afrika

Gazeti la "Handelsblatt" limemnukuu meneja wa kampuni ya safari, Cheli and Peacock nchini Kenya , Stefano Cheli akisema watalii kutoka Australia na Hongkong waliingiwa hofu kubwa kutokana na maradhi ya Ebola na kuamua kutofanya safari za kitalii nchini Kenya.

Bill Gates anuia kuyapiga vita maradhi

Gazeti la "Die Zeit " linatuarifu juu ya dhamira ya tajiri mkubwa duniani, Bill Gates ya kuwasaidia masikini.Gazeti hilo linauliza jee tajiri huyo ataweza kweli kuwaepusha masikini na maradhi ya hatari?

Gazeti hilo linakumbusha kwamba mkutano juu ya kile kinachoitwa mfungamano wa chanjo za kukinga maradhi, Gavi ulifanyika hivi karibuni mjini Berlin. Mwenyeji wa mkutano alikuwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Gazeti la "Die Zeit" linasema viongozi kutoka nchi mbalimbali hasa za Afrika pia walikuwapo kwenye mkutano huo.Lakini mgeni muhimu kabisa hakuwa kiongozi wa nchi yoyote, na wala halikuwa Shirika la Afya Duniani, WHO, bali ni Wakfu wa Bill na Melinda Gates.

Gazeti la "Die Zeit" limearifu kuwa kuanzia mwaka ujao hadi mwaka 2020 Wakfu wa Bill na Melinda Gates utatoa dola Bilioni saba na nusu kwa ajili ya kuutekeleza mradi wa chanjo, maarufu kama Gavi katika nchi za Afrika.

Lengo la Wakfu wa Bill na Melinda, linasema gazeti la "Die Zeit" ni kupambana na umasikini,maradhi na vifo vya mapema.Lakini gazeti hilo limeuliza jee tajiri mmoja peke yake ataweza kupambana na maadui hao wakubwa wa binadamu?

Mwandishi:Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo