Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 08.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yanazungumzia juu ya ziara ya Waziri Niebel nchini Uganda na Rwanda na juu ya chanjo dhidi ya saratani zinazotolewa kwa wasichana katika nchi kadhaa barani Afrika.

Mtafiti wa saratani Harald zur Hausen

Mtafiti wa saratani, Harald zur Hausen kutoka Ujerumani

Gazeti la "Süddeutsche limeandika makala juu ya ziara ya barani Afrika ya Waziri wa Ujerumani anaeshuhgulikia ushirikiano wa maendeleo Dirk Niebel. Waziri huyo alizitembelea Uganda na Rwanda.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema katika ziara yake nchini Uganda Waziri Niebel aliahidi msaada zaidi wa maendeleo kwa nchi hiyo ikiwa haki za binadamu zitaheshimiwa zaidi. Hata hivyo gazeti la "Süddeutsche" limeandika kwamba Uganda inapendelea zaidi kuwa na uhusiano na China na kwamba itautegemea utajiri wake wa mafuta japo utajiri huo bado umo katika hatua za kuanza kuendelezwa.

Malengo ya Umoja wa Mataifa ya kuuondoa umasikini:

Gazeti la "Süddeutsche" pia limeripoti juu ya malengo ya Umoja wa Mataifa ya kuuondoa umasikini mkubwa duniani hadi kufikia mwaka wa 2030.Gazeti hilo linaarifu katika ripoti yake kwamba kulingana na malengo ya Umoja wa Mataifa, utakapofika mwaka wa 2030 hatapakuwapo mtu atakeakuwa na kipato cha chini ya dola 1,25 kwa siku kwa ajili ya kuyakidhi maisha yake.

Hilo ni lengo kuu mojawapo la kamati iliyoaundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ya wataalamu wa uchumi na viongozi wa serikali ,ikiwa pamoja na Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirlief. Gazeti la "Südeutsche" limefahamisha kwamba kamati hiyo imeyajadili malengo tisa yanayopaswa kutekezwa na jumuiya ya kimataifa ili kupambana umasikini baada ya mpango wa Milenia wa Umoja wa Mataifa kumalizika mnamo mwaka wa 2015. Malengo hayo mapya yaliwasilishwa mjini New York na kamati hiyo ya wajumbe 27 ijumaa iliyopita.

Gazeti la "Süddeutsche" limeripoti kwamba ,katika malengo hayo mapya kamati ya wajumbe 27, watalamu wa uchumi na viongozi wa serikali imeweka kipaumbele katika maendeleo endelevu,ulinzi wa mazingira na haki za binadamu. Hata hivyo gazeti hilo limeandika kwamba malengo hayo bado yamo katika hatua ya mapendekezo yatakayowasilishwa,kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Septemba.

Japan yatoa ahadi kuongeza vitega uchumi Afrika:

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii limeripoti juu ya ahadi iliyotolewa na Japan ya kulisaidia bara la Afrika kwa kuekeza kiasi cha Euro Bilioni 10,7 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.Vitega uchumi hivyo vitakuwa katika sekta za umma na binafsi.Lakini gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeripoti kwamba Japan imetoa masharti. Kampuni za Japan zipewe tenda za miradi ya ujenzi wa miundo mbinu.

Chanjo dhidi ya saratani?

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limechapisha makala juu ya chanjo ya maradhi ya saratani. Gazeti hilo linaarifu kwamba wasichana barani, Afrika wanapewa chanjo ili kuwakinga na maradhi ya kansa, wakati katika nchi za magharibi bado pana mashaka juu ya kinga hiyo.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaeleza kuwa ni ndoto ya mwanadamu duniani kote juu ya kuweza, siyo tu kutibu na kuyaponyesha maradhi ya saratani bali pia kuweza kuyazuia maradhi hayo kwa kutoa chanjo. Sehemu ya ndoto hiyo inaweza kutekelezwa sasa. Ni kweli kwamba mpaka sasa hakuna chanjo ya kuzuia,saratani ya matiti, ya tumboni au ya tezi dume, lakini chanjo ya kukinga sarati ya mfuko wa uzazi inafanyiwa kazi.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limearifu kwamba matumaini ya kupatikana kwa chanjo madhubuti yanatokana na ugunduzi uliofanywa na mtafiti wa Ujerumani Harald zur Hausen mshindi wa nishani ya Nobel katika tiba.Mtafiti huyo amebainisha kuhusika kwa virusi,katika saratani ya mfuko wa uzazi. Gazeti la "Der Tagesspiegel"limefahamisha kwamba wasichana barani Afrika wameanza kupewa chanjo hiyo hivi karibuni.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman