1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yatuma wanajeshi kupambana na Taliban

Bruce Amani
6 Julai 2021

Serikali leo imepeleka mamia ya makomando na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali kupambana na mashambulizi ya kasi yanayofanywa na wanamgambo wa Taliban katika upande wa kaskazini.

https://p.dw.com/p/3w5Wq
Afghanistan Regierungstruppen in Faizabad
Picha: Afghanistan Ministry of Defence/REUTERS

Mapigano yamepamba moto katika mikoa kadhaa ya Aghanistan, lakini waasi wameelekeza zaidi kampeni yao kali katika eneo la kaskazini mwa nchi, ambako wamekamata wilaya kadhaa katika miezi miwili iliyopita.

Wiki iliyopita, wanajeshi wote wa Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO waliondoka katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Bagram karibu na Kabul – ambayo ndio makao makuu ya operesheni za kijeshi dhidi ya Taliban – na hatimaye kuhitimisha operesheni zao za miaka 20 zilizoanza baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11.

Soma pia: Ujerumani yawaondoa wanajeshi wake wote Afghanistan

Kamanda mpya wa kituo hicho, Jenerali Mir Asadullah Kohistani, anasema Wamarekani waliondoka kisiri saa za usiku. "Baada ya kusikia uvumi kuwa Wamarekani wameondoka Bagram, kwa kuongeza na ripoti yetu ya intelijensia na hatimaye kufikia saa moja asubuhi, tukafahamu imethitibishwa kwamba tayari wameondoka Bagram." Amesema Kohistani.

Afghanistan Soldaten
wanajeshi wa Afghanistan waimarisha ulinzi BadakhshanPicha: Nazim Qasmy/AP/picture alliance

Mamia ya wanajeshi na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wamepelekwa katika mikoa ya kaskazini ya Takhar na Badakshan ambako Mataliban wamekamata maeneo makubwa, bila mapigano yoyote.

Maafisa wa ulinzi wa Afghanistan wamesema wanakusudia kuzingatia Zaidi katika kuilinda miji mikubwa, barabara na miji ya mipakani kutokana na mashambulizi ya Taliban, yaliyoanzishwa wakati wanajeshi wa Marekani na NATO wakikamilisha shughuli zao za kuondoka kabisa mapema Mei.

Hapo jana, Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Kiafghanistan walikimbilia nchi jirani Tajikistan hatua amabyo imeilazimu nchi hiyo jirani kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo kwa kuwapeleka wanajeshi wake. Mamia kadhaa ya wanajeshi tayari waliingia Tajikistan katika wiki za karibuni kufuatia mashambulizi ya Taliban.

Rais wa Tajikistan Emomali Rakhmon ameamuru kupelekwa wanajeshi 20,000 wa akiba ili kuongeza ulinzi katika mpaka kati ya Tajikistan na Afghanistan.

Soma zaidi: Jamii ya kimataifa yataka Afghanistan kuendeleza mazungumzo

Mapigano hayo ya kaskazini pia yameilazimu Urusi kufunga ubalozi wake mdogo katika mji wa Mazar-i-Sharif, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Balkh na mojawapo ya miji mikubwa sana nchini Afghanistan karibu na mpaka na Uzbekistan.

Namna ambavyo Mataliban waliingia kwa kasi na kuyakamata maeneo makubwa ya Takhar na Badakhshan ni pigo kubwa la kisaikolojia kwa serikali ya Afghanistan. Mikoa hiyo miwili kwa wakati mmoja ilitumika kama ngome za Muungano wa Kijeshi uliopambana na Taliban katika upande wa kaskazini wakati wa vita vikali vya miaka ya 1990 na haikuwahi kukamatwa na wanamgambo wa itikadi kali.

AFP