Ziwa Turkana liko hatarini-UNESCO | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ziwa Turkana mashakani

Ziwa Turkana liko hatarini-UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limelijumuisha Ziwa Turkana nchini Kenya katika orodha ya turathi za dunia zilizo hatarini. Miradi ya Ethiopia katika bwawa Omo inahusishwa

Kamati ya UNESCO jana ililijumussha Ziwa Turkana ambalo ni muhimu sana nchini Kenya na eneo linalojumuishwa kati ya maeneo ya chimbuko la binadamu, katika orodha ya turathi zinazokabiliwa na hatari ambapo wataalamu hao waliokutana Bahrain wameonesha kwamba athari za bwawa la Ethiopia zinaongeza kitisho  katika eneo hilo. Ziwa Turkana ambalo liko kaskazini magharibi mwa Kenya na ambalo pia linajulikana kama Bahari ya Jade ni ziwa lenye kiwango kikubwa cha madini ya Sodium Chloride  katika eneo la Afrika Mashariki na pia ni ziwa kubwa la jangwani duniani.

Visiwa vya eneo hilo la Ziwa Turkana ndiyo sehemu wanakozaliana mamba wanaojulikana kama Mamba wa Mto Nile, viboko na aina tafauti za nyoka wakati ambapo ziwa lenyewe ni muhimu kwa ndege wanaohama. Eneo hilo kwa upande mwingine lina uwezekano wa kuwa chimbuko la binadamu likiwa na sehemu zenye mabaki na mifupa katika eneo la Koobi Fora, mashariki mwa fukwe za Ziwa Turkana.

BdT Kenia Wissenschaft Evolution Fosil Homo erectus (AP)

Mabaki ya viumbe vingi vya mwanzo yamepatikana katika eneo hilo ikiwemo sokwe waliokuwa na mifano ya binadamu, wakifahamika kisayansi kama Australophithecus, Homo Habilis, Homo Erectus na Homo sapiens, ambaye ni kiumbe aliyekuwa sawa kabisa na binadamu wa sasa.

Shirika hilo la UNESCO linasema eneo hilo la Koobi fora lililosheheni mabaki ya viumbe mbali mbali limetowa mchango mkubwa zaidi katika uelewa wa mazingira yanayomzunguka binadamu kuliko eneo jingine lolote duniani. Kadhalika linasema kwamba rikodi za jiolojia na mabaki ya viumbe yanawakilisha hatua kubwa muhimu za historia ya dunia. Ziwa Turkana hata hivyo linakabiliwa na hatari kubwa moja ya msingi ambayo ni ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha nguvu za umeme la Ethiopia katika Mto Omo ambalo linayajaza maji ya Ziwa Turkana kwa msimu.

Bwawa hilo la Ethiopia linatishia kutatiza msimu wa kujaa maji ambo ni muhimu sana katika mzunguuko wa uzalishaji wa samaki katika Ziwa Turkana wakati ikikadiriwa kwamba watu 300,000 wanategemea samaki kutoka ziwa hilo kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku, Mradi wa umwagiliaji wa Ethiopia pia unatarajiwa kupunguza kwa kasi kubwa kiwango cha maji yanayoingia kwenye Ziwa hilo la Kenya.

Mtaalamu wa Kenya kuhusu masuala ya viumbe Richard Leakey anasema kutumiwa kwa madawa ya kuua wadudu na madawa ya mimea pamoja na mbolea na serikali ya Ethiopia katika miradi yake ya pamba na miwa  kupitia umwagiliaji kutoka bwawa la Omo ndiyo sababu itakayolifanya Ziwa Turkana kuwa kama Aral Sea au ziwa la Ulaya ya Kati na Urusi lililoharibiwa kabisa kutokana na sababu kama hizo.

Mwandishi: Saumu Yussuf
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com