ZIMBABWE | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

ZIMBABWE

Marekani imeanda rasimu ya azimio litakalowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutaka kuwekewa vikwazo vya silaha, fedha na vya kusafiri Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na wasaidizi wake 11.

default

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye Marekani inaanda azimio la vikwazo vikali dhidi yake

Hatua hiyo inatokana na duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo ambapo Rais Mugabe aliyekuwa mgombea pekee alichaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo.Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai alijitoa katika duru hiyo iliyoshutumiwa na jumuiya ya kimataifa.


Rasimu hiyo pia itautaka utawala wa Mugabe kuingia haraka katika majadiliano na upande wa upinzani ili kufikia suluhisho la amani litakalotoa nafasi kwa matwaka ya wananchi wa Zimbabwe kama walivyoonesha katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa mwezi March mwaka huu.


Katika uchaguzi huo mgombea wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai alimshinda Rais Mugabe lakini alishindwa kupata zaidi ya 50 asilimia ya kura kuweza kutawazwa kuwa rais.Pia chama chake kilipata viti vingi vya ubunge.


Rasimu hiyo ya Marekani inawataka nchi wanachama  wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua muhimu za kuzuia upelekwaji wa aina yoyote ya silaha nchini Zimbabwe pamoja na vitu vinavyotumika katika operesheni za kijeshi.


Aidha Marekani inataka kuwekewa vikwazo vya kusafiri na kuzuiwa kwa mali zao Rais Mugabe, Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo Gideon Gono, Waziri wa Sheria Patrick Chinamasa pamoja na maafisa wengine tisa wa utawala wake.


Hata hivyo rasimu ya azimio hilo inategemewa kupata upinzani kutoka kwa Afrika Kusini ambayo ni msuluhishi katika mzozo huo wa kisiasa nchini Zimbabwe, pamoja na China yenye kura ya turufu.China ni mshirika mkubwa wa Zimbabwe.


Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Zalmay Khalilzad amesema kuwa anaendelea kushauriana ni jinsi gani watawasilisha rasimu hiyo katika Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo Alhamisi ijayo litasikiliza ripoti ya kamati ya Umoja wa Mataifa juu ya Zimbabwe.


Ujumbe wa Marekani umependekeza  kwamba Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dr Asha Rose Migiro ambaye aliudhuria mkutano wa wakuu wa Afrika huko Misri alieleze baraza hilo juu ya kile kilichojadiliwa katika mkutano huo.


Pia inamtaka mjumbe maalum wa Umoja huo wa Mataifa katika mzozo wa Zimbabwe ambaye ameshindwa kuutanzua mzozo huo, Haile Menkerious naye pia awasilishe ripoti yake.


Lakini Balozi wa Vietnam katika Umoja wa Mataifa Le Luong Minh ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo mwezi huu, amesema kuwa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa  miongoni mwa nchi wanachama wa baraza hilo kuhusiana na kuwasilishwa kwa taarifa hizo.


Pia balozi huyo amesema kuwa rasimu ya azimio hilo bado haijawasilishwa rasmi katika baraza hilo.


Hapo siku ya Jumanne wakuu wa Umoja wa Afrika katika mkutano wao wa kilele mjini Sharm el-Sheikh walipitisha azimio linalotaka kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Zimbabwe.


Lakini hapo jana kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai alitangaza kutokubaliana na azimio hilo akisema kuwa serikali hiyo haitokuwa suluhisho la mzozo wa kisiasa nchi humo.


 • Tarehe 03.07.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EVaR
 • Tarehe 03.07.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EVaR
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com