Zimbabwe katika Njia Panda | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Zimbabwe katika Njia Panda

Uchaguzi ulio huru katika Zimbabwe hauwezi kufanyika kwa hivi sasa. Ilikuwa rahisi na wazi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutambua jambo hilo.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano wa hadhara mjini Harare.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano wa hadhara mjini Harare.

Katika taarifa yake ya jana usiku, baraza hilo lililaani namna serekali ya Zimbabwe inavotumia nguvu dhidi ya upinzani wa nchi hiyo. Lilimtaka Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo aache kuendesha usumbufu huo. Lakini, bila ya kujali, Robert Mugabe ameshikilia kwamba uchaguzi wa marudio wa urais utafanywa kama ilivopangwa. Jee Zimbabwe iko katika njia panda? Na jee mambo ni kama ya kawaida kwa Mugabe? Njia gani ya kupita ili kujikwamua na mzozo huo, na kwa umbali gani upatanishi wa nchi za Kiafrika unaweza ukasaidia??? Ute Schaeffer, mkuu wa Idara ya Afrika na Mashariki ya Kati ya hapa Deutsche Welle, anuangalia mzizi wa mzozo huu. Taarifa yake inasomwa studioni na Othman Miraji...


Kwa wananchi wanaohakiki mambo huko Zimbabwe, kwa vyovyote vile, Robert Mugabe ameshindwa. Kumbirai Mafunda, mwandishi wa habari wa gazeti la Financial Gazettte, kama ilivokuwa kabla, anahisi Wa-Zimbabwe wengi wanataka mabadiliko na wataupigia kura upinzani, ikiwa wataweza:

" Mambo yote yanalenga kuwatisha waandishi wa habari, kuutisha upinzani. Lakini uchaguzi wa mwanzo umeonesha wazi: wananchi wa Zimbabwe kile wanachotaka. Wananchi wamechoshwa na mfumo wa chama kimoja cha ZANU-PF, wanataka kujikwamua na hali ya uchumi unaokwenda chini. Tuna hali ngumu hapa Zimbabwe. Utawala wa Mugabe unazibinya jumuiya za kiraia na mbinyo huo umezidi tangu mwezi wa Machi."

Andrew Mwenda, mwandishi wa habari wa kutokea Uganda, naye anahisi kwamba ni demokrasia tu na serekali zilizofanikiwa ndizo zinazoweza kuishi. Uchumi wa Zimbabwe umekwenda chini kabisa kwa kiwango kisichowahi kuonekana. Mnamo miaka 20, nchi hiyo iliokuwa inapigiwa mfano hapo zamani, imegeuka kuwa nyumba ya umaskini barani Afrika. Tarakimu rasmi zinasema mfumko wa bei umefikia asilimia laki moja, lakini tarakimu zisizokuwa rasmi zinasema umefikia asilimia milioni moja. Ukosefu wa kazi umefikia asilimia 80, na idadi kama hiyo ya watu wanaishi kwa kipato cha chini ya dola mbili za Kimarekani kwa siku. Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliotolewa mwaka 2004 inasema karibu nusu ya wakaazi wa Zimbabwe wako kwenye utapio mlo. Kuporomoka kwa uchumi, kwa mujibu wa Andrew Mwenda, ambaye pia ni mwanauchumi, ndio sababu Mugabe atapoteza madaraka:

"Hiyo ndio sababu kwanini Mugabe alishindwa wazi wazi katika duru ya kwanza ya uchaguzi na ataendelea kushindwa. Mugabe hana fedha za kuyasimamisha madaraka yake ya kisiasa. Siwezi kusema hasa vipi mambo yatakavokwenda, lakini kuna hali nzuri ya kuweza kuwa na mbadala."

Umoja wa Ulaya na Marekani zimelalamika vikali dhidi ya kampeni ya utumiaji nguvu inayoendeshwa kabla ya uchaguzi wa urais. Marekani na Uengereza zimeielezea serekali ya Robert Mugabe kuwa sio tena ya kisheria. Nchi za Kiafrika zilizo jirani na Zimbabwe zinajiepusha kutoa tamko wazi kama hilo dhidi ya mpiganaji wa uhuru huyo wa zamani. Lakini jana Umoja wa Afrika, AU, ulielezea kuingiwa na wasiwasi juu ya mambo yanavokwenda nchini humo, na ukavitaka vyama vyote kuachana na matumizi ya nguvu. Rais wa komisheni ya AU, Jean Ping, anawasiliana na Jmuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, kujuwa hatua gani zichukuliwe.Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, ambaye amepewa jukumu na nchi za SADC ajaribu kuleta upatanishi huko Zimbabwe, ametoa mwito wa kuweko mdahalo zaidi baina ya pande zinazogombana.


Mwandishi wa habari wa Zimbabwe, Kumbirai Mafunda, anasema mwito huo hautoshi. Yeye anaudhika namna Mugabe anavoungwa mkono kichini chini, kupitia mpatanishi mkuu Thabo Mbeki:

" Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki ameshindwa katika mazungumzo ya kuleta upatanishi; pia viongozi wengine wa nchi za SADC wameshindwa. Ni Mbeki ambaye hasa aliyesema kwamba hakuna maafa huko Zimbabwe. Kwanini ilikuwa lazima kutumwa huko misaada ya kiutu? IKiwa katika Zimbabwe hakuna maafa ya kiutu, nini kilichoko huko? Mbeki amepoteza uaminifu wowote wa yeye kuwa mpatanishi. Ni wakati atafutwe mpatanishi mwengine."

Lakini kuna wahakiki wanaoshikilia kwamba tataizo la Zimbabwe liwachiwe Wa-Zimbabwe wenyewe walitanzuwe na nchi za nje zisijiingize katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Wengine wanahoji kwamba hata vikwazo vya kiuchumi havitabadilisha sana hali ya mambo.

Upinzani wa Zimbabwe umeshauri iundwe serekali ya mpito baina ya chama cha upinzani cha MDC na kile tawala cha ZANU-PF, lakini bila ya Robert Mugabe kuwemo ndani yake. Lakini jambo hilo linaweza tu kufanyika kwa upatanishi wa nchi jirani za Kiafrika. Hata hivyo, jambo hilo halifikirii Mzee Mugabe. Ni yeye karibuni aliyesema ni Mwenyezi Mungu tu atayeukomesha utawala wake. • Tarehe 24.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQ4J
 • Tarehe 24.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQ4J
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com