Zilzala ya uchaguzi mkuu magazetini | Magazetini | DW | 26.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Zilzala ya uchaguzi mkuu magazetini

Matokeo ya chaguzi mkuu yanaendelea kugonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani.

 

Tunaanza na gazeti la "Schwäbische Zeitung" linaloyataja matokeo ya uchaguzi kuwa ni "zilzala ya kisiasa." Gazeti linaendelea kuandika: "Kwa vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU/ na Christian Social Union CSU, uchaguzi huo umesababisha zilzala ya kisiasa, pigo la kihistoria. Lakini kwa Angela Merkel hali ni nyengine. Ni sawa kwamba sasa watajishughulisha na kutafuta sababu za hali hiyo. Kwa maneno mengine matatizo watayashughulikia-kama kawaida. Mwenyekiti wa CSU, Horst Seehofer yeye anaonyesha yu hamkani, na si bure. Amepoteza asili mia 10.5 ya kura, inamaanisha enzi za chama chake cha CSU katika jimbo la kusini la Bavaria zinaonyesha ziko hatarini. Na kwamba watu hawaridhiki hata kidogo na mkondo wa vyama ndugu vya CDU/CSU. Suala kama hawaridhiki na Merkel, na Seehofer, na wote wawili au hawafurahishwi na mivutano ya kila mara ya vyama hivyo ndugu, suala hilo linajibiwa kwa namna tofauti na wahusika. Katika wakati ambapo kansela Merkel anataka mambo yaendelee kama yalivyo, Seehofer anapigania marekebisho. Inamaanisha marekebisho mpaka katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano mjini Berlin. Kwa hivyo njia ni ndefu hadi muungano wa Jamaica utakapoundwa, kama utaundwa."

Pengine mungano wa Jamaica ukaleta tija

Gazeti la Badische Zeitung linahisi licha ya ugumu wa mazungumzo, juhudi za  kuunda serikali ya muungano wa vyama vinne: CDU, CSU, FDP na walinzi wa mazingira die Grüne, serikali inayotajwa kuwa  ya muungano wa Jamaica, zinaweza kuleta tija. Gazeti linaendelea kuandika: "Lisilokuwa na budi ni ushahidi wa bidii. Sio mbinu za kisiasa, ni busara za kitaifa na moyo wa bidii kufanya majaribio na hilo linaweza kusababisha ufanisi ambao hakuna aliyeufikiria. Kwa sharti kama hawatajishughulisha na mada chungu nzima, kama watajiwekea vipaumbele bayana na kama Umoja wa Ulaya hautoachwa kando. Hasa kwakua kwa wakati huu hakuna anaevutiwa na muungano wa Jamaica ndipo nayo nafasi ya kufanikiwa muungano kati ya CDU, CSU, FDP na die Grüne inaonyesha kuwa kubwa. Ni fursa inayoweza kudhihirisha kwamba sera za wastani bado zina nguvu humu nchini, hata kama nguzo ya SPD ina lega lega."

Mivutano ndani ya chama cha AfD

Zilzala inapiga pia katika chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,"Chaguo Mbadala kwa Ujerumani"-AfD. Siku moja baada ya ushindi wao mkubwa, mwenyekiti wa chama hicho Frauke Petry ametangaza kujitenga na kundi la wabunge wa chama hicho. Hata hivyo gazeti la "Landeszeitung" linatahadharisha: Msiamini kama AfD watatawanyika haraka hivyo. Hata kama siku moja tu baada ya ushindi wao wameanza kuzozana. Kwamba Petry amejitoa katika kundi la wabunge wa AfD,hilo ni pigo kubwa kwa chama hicho lakini sio mwisho wa chama hicho. Pasitokee yeyote atakaeamini kuwa wapiga kura watakilinganisha chama cha AfD na kundi la wafanya fujo wasiokuwa na muongozo. Wananchi wengi wamekipigia kura chama hicho kwasababu ya mchanganyiko wa hasira, kuvunjika moyo na malalamiko.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com