1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Netanyahu yaitia kishindo Ujerumani

Josephat Charo
16 Machi 2023

Serikali ya Ujerumani inakabiliwa na shinikizo kwa kumkaribisha waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa ziara rasmi mjini Berlin. Netanyahu aliwasili Jumatano (15.03.2023)

https://p.dw.com/p/4OlNk
Israel | Premierminister Benjamin Netanjahu
Picha: Ronen Zvulun/POOL/AFP/Getty Images

Kabla Netanyahu kuanza safari kwenda Berlin na kabla ziara anayopanga kuifanya nchini Uingereza, waandishi 1,000 wasanii na wasomi wamewaandikia mabalozi wa nchi hizo mbili za Ulaya kuzihimiza serikali zao zifute ziara zake. Katika barua yao walisema kwa kuzingatia uongozi hatari na wa uharibifu wa Netanyahu, na kwa kutilia maanani upinzani mkali wa umma kupinga kuhujumiwa na kuharibiwa taasisi za dola kwa mchakato wa kutunga sheria usio wa kidemokrasia, wanazitaka Ujerumani na Uingereza zitangaze haraka kufutwa kwa ziara za Netanyahu. Walitahadharisha kwamba ikiwa ziara hizo zitaruhusiwa kuendelea kama ilivyopangwa, basi zitagubikwa na kiza kinene.

Netanyahu anatarajiwa kukutana na Kansela Olaf Scholz na rais wa Ujerumani Fank Walter Steinmeier hivi leo mjini Berlin. Afisi ya Netanyahu imesema kiongozi huyo atajadili masuala ya diplomasia na usalama pamoja na matukio mengine ya ukanda wa Mashariki ya Kati. Netanyahu alisema, "Suala kuu nitakalolizungumzia ni Iran na pia masuala mengine ambayo ni muhimu kwa dola ya Israel. Masuala ya usalama hayasiti na kuacha kuzungumziwa hata kwa muda."

Israel Netanjahu Besuch Deutschland Protest
Magari yenye bendera ya Israel yakishirki maandamano uwanja wa ndege wa Ben Gurion, mjini Tel Aviv, Jumatano Machi 15, 2023Picha: Tsafrir Abayov/AP Photo/picture alliance

Mjini Frankfurt, Meron Mendel, mkuu wa taasisi ya elimu ya Anne Frank, jina la muhanga chipukizi wa mauaji ya Wayahudi, Holacaust, pia alisema serikali ya Berlin ilitakiwa kuikataa ziara ya Netanyahu. Mendel ameiambia redio ya umma Bayerische Rundfunk kwamba ikiwa waziri mkuu wa Israel anataka kufuta maadili ya kawaida ya demokrasia, basi leo ni wakati mbaya kabisa kumualika azuru Berlin.

Mtaalamu huyo wa histora raia wa Ujerumani mwenye asili ya Israel aidha amesema serikali ya Ujerumani ilitakiwa kumfahamisha Netanyahu kwamba haiwezekani kumkaribisha wakati kama huu. Ameongeza kusema serikali ya kansela Olaf Scholz sharti itambue kwamba hakuna biashara inayoweza kufanyika na serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Israel, akitambua kwamba urafiki baina ya Ujerumani na Israel umejikita kwenye msingi wa maadili ya pamoja.

Baadhi ya Waisraeli wanaoishi mjini Berlin pia wameitisha maandamano kupinga ziara ya Netanyahu. Chini ya kauli mbiu "Linda demokrasia ya Israel" wanaharakati watafanya maandamano katika lango la Brandenburg leo mchana.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amesisitiza kuwa Netanyahu ni waziri mkuu wa Israel aliyechaguliwa kidemokrasia na kwa hivyo ni mgeni wa kawaida nchini Ujerumani.

Peter Lintl wa taasisi ya Ujerumani ya masuala ya kimataifa na usalama ameandika kwenye uhariri wake katika gazeti la Tagesspiegel kwamba ziara ya Netanyahu inampa fursa ya kupumua kutokana na shinikizo la ndani na ni jukwaa ambalo anaweza kung'ara kisiasa.

(ape,afpe)