1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky kukutana na Erdogan mjini Istanbul Ijumaa

Angela Mdungu
7 Julai 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky leo anakutana na Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan kwa mazungumzo, katika mfululizo wa safari zake za kushinikiza azma ya Ukraine kujiunga na Jumuiya ya kujihami ya NATO.

https://p.dw.com/p/4TZQH
Ukraine Präsident Selenskyj
Picha: Sergei Supinsky/AFP

Mazungumzo ya leo kati ya Zelensky na Erdogan yanatazamiwa kufanyika mjini Istanbul ikiwa ni siku moja kabla ya kukamilika kwa siku 500 tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, huku Zelensky akikiri wazi kuwa mashambulizi ya kuikabili Urusi yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yanaendelea kwa kusuasua.

Licha ya moja ya ajenda za leo kuwa kutaka kuungwa mkono katika kujiunga na Jumuiya ya kujihami ya NATO kwenye mkutano wa wiki ijayo, mazungumzo ya Zelensky na Erdogan ambaye ni msuluhishi muhimu katika mzozo wa Ukraine na Urusi, yatajikita pia katika ukomo wa muda wa mkataba wa kusafirisha nafaka za Ukraine kupitia bahari nyeusi. Mkataba huo unatazamiwa kumaliza muda wake Julai 17 ikiwa Urusi haitoridhia kuurefusha.

Urusi imetishia kutorefusha mkataba wa nafaka

Hata hivyo, Urusi ambayo imekasirishwa na masuala ya utekelezaji wa mkataba huo imetishia kuto kuurefusha. Erdogan, aliyechaguliwa kwa mara nyingine kuiongoza Uturuki amekuwa akijaribu kuendelea kudumisha mahusiano na nchi zote mbili, Urusi na Ukraine.

Wachambuzi wanatarajia pia kuwa, kwenye mazungumzo ya leo, Rais Volodymyr Zelensky atamshinikiza Rais Erdogan kuiunga mkono Sweden, ipewe uanachama wa jumuiya hiyo kwenye mkutano utakaofanyika wiki ijayo.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Irina Yakovleva/ITAR-TASS/imago images

Ziara ya Zelensky nchini Uturuki inafuatia ziara za awali alizozifanya nchini Bulgaria na Czech aliyoitembelea jana alhamisi.

Wakati huohuo, Ukraine, leo imesitisha operesheni ya uokoaji katika mji ulio mashariki wa Lviv ambao ulishambuliwa kwa makombora ya Urusi jana Alhamisi. Kulingana na taarifa ya gavana wa eneo hilo Maksym Kozytskyi idadi ya vifo kutokana na shambulio hilo imefika watu 10. Kotzyskyi aliyelitaja shambulio hilo kuwa kubwa zaidi lililolenga miundombinu ya raia katika mzozo unaoendelea, amesema waokoaji walifanya kazi usiku kucha kuondoa vifusi licha ya mvua kubwa.

Katika hatua nyingine, taarifa iliyotolewa na  jeshi la Ukraine leo imesema wamepata mafanikio zaidi katika mji wa Klichviika, unaodhibitiwa na Urusi huko Bakhmut mashariki mwa jimbo la Donetsk. Licha ya taarifa hiyo, vyanzo kutoka upande wa Urusi vinasema kuwa hadi sasa, bado Ukraine haijafanikiwa kuudhibiti mji huo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa jeshi hilo linazidi pia kuongeza shinikizo kwa majeshi ya Urusi kaskazini mwa Ukraine.