1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy asema vikosi vyake vyazidi kushangaza

12 Juni 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema hakuna mtu anajua vita nchini mwake vitaisha lini lakini vikosi vyake vimewashangaza wengi kwa kuwazuwia wanajeshi wa Urusi kuiteka haraka Ukraine Mashariki kama walivyopanga.

https://p.dw.com/p/4Carg
Ukraine-Krieg Bucha | Präsident Selenskyj
Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS/REUTERS

Katika ujumbe wake wa usiku kwa njia ya vidio, rais Zelenskiy alisema anajivunia watetezi wa Ukraine wanaomudu kuzuwia vikosi vya Urusi kusonga mbele katika mkoa wa Donbas, unaopakana na Urusi na ambako wapiganaji wa kujitenga wanaoungwa mkono na Moscow wamedhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo kwa miaka minane.

"Kumbukeni namna nchini Urusi, mwanzoni mwa Mei, walitumai kuiteka Donbas yote?" alisema rais Jumamosi usiku. Ni tayari siku ya 108 ya vita, ni Juni tayari. Donbas bado inaendelea kusimama kidete.

Soma pia: Vikosi vya Ukraine vyang'ang'ana mjini Severodonetsk

Baada ya kushindwa kuiteka Kyiv, mji mkuu wa Ukraine, mwanzoni mwa vita, Moscow ilielekeza nguvu juu ya kutwaa maeneo ya mkoa wa Donbas ulio na wakaazi wengi wanaozungumza Kirusi yalio bado dhidi ya udhibiti wa Ukraine, pamoja na pwani ya kusini mwa nchi hiyo.

Ursula von der Leyen trifft Präsident  Zelenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akizungumza na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wakati wa mkutano wa habari mjini Kyiv, Aprili, 8, 2022.Picha: Janis Laizans/REUTERS

Lakini badala ya kupata ushindi wa haraka na wa kishindo, vikosi vya Urusi vimevutwa katika mapambano marefu na makali, shukuran kwa sehemu kwa matumizi ya Ukraine ya silaza zilizotolewa na mataifa ya magharibi.

Serikali zote za Ukraine na Urusi zilisema Sievierodonetsk, ambao ni mji wa mashariki uliokuwa na idadi ya wakaazi 100,000 kabla ya vita, unaendelea kuwaniwa.  Mji huo na mji jirani wa Lysychansk ndiyo  maeneo muhimu ya mwisho ya mkoa wa Luhansk wa Donbas yasio chini ya udhibiti kamili wa waasi wanaoegemea Urusi.

Sievierodonetsk bado 'kukombolewa kikamilifu'

Leonid Pesechnik, kiongozi wa eneo lililojitangaza kuwa huru la Jamhuri ya Luhansk, alisema wapiganaji wa Ukraine walisalia katika eneo la viwanda la mji huo, ikiwemo kiwanda cha kemikali ambako raia walijihifadhi kutokana na siku kadhaa za mashambulizi ya Urusi.

Soma pia: Uzuiaji wa nafaka za Ukraine wahatarisha maisha ya mamilioni

"Sievierodonetsk haijakomblewa kwa asilimia 100," Pasechnik alisema Jumamosi, akidai kwamba Waukraine walikuwa wanaushambulia mji kutokea kiwanda cha Azot. "Hivyo ni vigumu kuitaja hali kuwa tulivu mjini Sievierodonetsk, kwamba ni wetu kikamilifu."

Gavana wa Luhansk Serhii Haidai aliripoti Jumamosi kwamba moto mkubwa ulizuka kwenye kiwanda hicho wakati wa mashambulizi ya Urusiyaliodumu kwa saa kadhaa.

Ursula von der Leyen trifft Präsident  Zelenskyj
Zelenskiy asema vikosi vya Ukraine vimevuka matarajio yote kwa kukwamisha uvamizi wa Urusi.Picha: Janis Laizans/REUTERS

Kwingineko nchini Ukraine, mashambulizi ya kujibu yaliwafurusha Warusi nje ya maeneo ya mkoa wa kaskazini mwa Ukraine wa Kherson waliouchukuwa mwanzoni mwa vita, kwa mujibu wa zelenskiy.

Moscow imeweka viongozi wake mkoani Kherson na maeneo mengine yanayokaliwa, huku ikitoa paspoti za Urusi kwa wakaazi mkoa huo, kutangaza habari za Urusi na kuchukua hatua za kuanzisha  mtaala wa shule wa Urusi.

Soma pia: Merkel atetea urathi wake wa Urusi, asema hataomba radhi

Zelenskiy alisema wakati hakuna ishara za kumalizika kwa vita hivyo, Ukraine inapaswa kufanya kila kitu inachoweza kuhakikisha kuwa Warusi "wanajutia kila kitu walichokifanya na wawajibishwe kwa kila mauaji na kila shambulio dhidi ya taifa letu zuri."   

Asema Urusi imepoteza wanajeshi mara tatu zaidi ya Ukraine

Kiongozi huyo wa Ukraine alidai kwamba Urusi imepoteza karibu mara tatu ya idadi ya wanajeshi ikilinganishwa na waliokufa upande wa Ukraine, na kuongeza kuwa: "Kwa ajili ya nini? Imepata nini, Urusi? Hata hivyo hakuna makadirio huru ya kuaminika ya vifo vya vita hivyo mpaka sasa.

Akizungumza kwenye mkutano wa ulinzi nchini Singapore siku ya Jumapili, waziri wa ulinzi wa china Jenerali Wei Fenghe alisema Beijing inaendelea kuunga mkono mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine, na inatumai Marekani na washirika wake wa NATO watazungumza na Urusi ili "kuweka mazingira ya usitishaji mapigano wa mapema."

Ukraine Krieg | Azot Chemiefabrik Sjewjerodonezk
Moshi ukifuka kwenye kiwanda cha kemikali cha Sievierodonetsk kufuatia mashambulizi ya Urusi.Picha: Oleksandr Ratushniak/REUTERS

"China itaendelea kutoa mchango chanya na kuchangia kwenye kutuliza mzozo na kupatikana kwa suluhisho la kisiasa la mzozo huo," alisema Wei.

Soma pia: Ukraine yaendelea kushikilia 'maeneo' ya Sievierodonetsk

Alipendekeza kwamba mataifa yanayoipatia Ukraine silaha yalikuwa yanazuwia amani kwa "kuongezea mafuta kwenye moto" na kusisitiza kwamba China haijatoa msaada wowote wa kivifaa kwa Urusi wakati wa vita hivyo.

"Ukuaji wa uhusiano wa China na Urusi ni ushirika, siyo muungano," Wei alisema.

'Urusi yajiandaa kwa vita virefu'

Taasisi ya mafunzo ya vita, ambayo ni shirika la ushauri lenye makao yake mjini New York, Marekani, ilisema katika tathmini yake ya karibuni zaidi kwamba taarifa za kiuchunguzi za Ukraine zinaonyesha jeshi la Urusi lilikuwa linajipanga "kupigana vita vya muda mrefu."

Taasisi hiyo ilimnukuu naibu mkuu wa idara ya usalama ya Ukraine akisema kwamba Moscow imesogeza ratiba yake ya vita hadi mwezi Oktoba, ambapo mabadiliko yatafanywa kulingana na mafanikio yoyote kwenye kanda ya Donbas.

Soma pia: Mkuu wa Umoja wa Afrika amwambia Putin, Waafrika ndio 'waathirika' wa mzozo wa Ukraine

Uchunguzi huo "unaonekana kuashiria kwamba Kremlin imetambua kwa uchache, kwamba haiwezi kufikia malengo yake nchini Ukraine haraka na hivyo inafanya mabadiliko katika malengo yake ya kijeshi katika jaribio la kurekebisha kasoro za awali katika uvamizi wa Ukraine," lilisema shirika hilo la ushauri.

Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Luhansk nchini Urusi, Rodion Mironshnik, alisema Jumamosi kwamba wanajeshi kati ya 300 hadi 400 wa Ukraine wanaendelea kuzingirwa ndani ya kiwanda cha kemikali cha Sievierodonetsk pamoja na mamia kadhaa ya raia.

Soma pia: Urusi yadhibiti karibu asilimia ishirini ya ardhi ya Ukraine

Warusi walianzisha mawasiliano na wanajeshi wa Ukraine ili kuandaa utaratibu wa kuwaondoa raia, lakini wanajeshi hao wataruhusiwa tu kuondoka iwapo wataweka chini silaha zao na kujisalimisha, alisema Miroshnik.

Masharti sawa na hayo yalikuwepo kwenye kiwanda cha chuma katika mji wa kusini wa Mariupol kabla ya kuandaa uondoaji wa raia na vikosi vya utetezi viliamriwa na makamanda wa jeshi la Ukraine kuacha mapigano. Wapiganaji waliotoka nje ya kiwanda cha Mariupol walichukuliwa kama wafungwa na Warusi.

Pasechnik, kiongozi wa wanaotaka kujitenga katika jamhuri isiyotambuliwa ya Luhansk, alisema Waukraine wanaotoa upinzani mjini Sievierodonetsk wanapaswa kujiepusha na matatizo.

"Ningekuwa wao, tayari ningefanya uamuzi (kujisalimisha)," alisema. "Tutafikia lengo letu kwa namna yoyote ile. Tutalikomboa eneo la viwanda kwa vyovyote vile.  Tutaikomboa Sievierodonetsk kwa vyovyote vile."