Yulia Tymoshenko kuwania urais Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Yulia Tymoshenko kuwania urais Ukraine

Miezi miwili kabla ya uchaguzi, mwanasiasa wa siku nyingi mwenye utata anajaribu tena bahati yake kwa urais. Anataka fidia kutoka kwa Urusi kuhusiana na Crimea na mgogoro wa wanaotaka kujizenga mashariki mwa Ukraine.

Tangu kuibuka kwake kwa umaarufu wa kisiasa na umashuhuri wa kimataifa wakati wa mapinduzi ya 2004 yaliopewa jina la Macungwa, Tymoshenko alikaa gerezani kwa muda, na pia serikalini.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 58 alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais mwaka 2014 akishindwa na rais wa sasa Petro Poroshenko. Tangu wakati huo ametumia muda mwingi kumkosoa.

Tymoshenko amethibitisha kuwa atawania urais katika uchaguzi utakaofanyika Jumapili, Machi 31. "Nawania urais," alisema wakati wa mkutano wa chama chake cha kizalendo cha Batkivshchyna (Fatherland).

Aongoza katika uchunguzi wa maoni

Uchunguzi wa maoni ya wapigakura unaonyesha kuwa Tymoshenko anaongoza, ingawa kwa asilimia 16 tu, mbele ya asilimia 13.8 ya Poroshenko. Lakini ni mwanasiasa mwenye utata sana katika siasa za nchini Ukraine. Kuna wasiwasi kuhusu uwezekano wa uhusiano na rais wa Urusi Vladmir Putin, ambaye wakati mmoja alimzungumzia vyema.

Parteitag Batkiwshchyna (Vaterland) in Kiew (Reuters/V. Ogirenko)

Yulia Tymoshenko akiwa na mauwa wakati akiwasalimia wafuasi wake waakti wa mkutano mkuu wa chama chake cha Batkisshchyna mjini Kiev Januari 22, 2019.

Hata hivyo, anataka fidia kutoka kwa Urusi kuhusiana na hatua ya Moscow kulitwaa kimabavu eneo la Crimea na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine. Pia amezungumzia vyema kuhusu kujiunga na Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami NATO.

Rekodi mchanganyiko

Kiongozi wa shirika la gesi la Ukraine katika miaka ya 1990, Tymoshenko aliajiriwa na kufukuzwa kama naibu waziri mkuu wakati wa utawala wa miaka 10 wa rais Leonid Kuchma mwanzoni mwa Milenia.

Alishinda na kupoteza uchaguzi tena, akihudumu kama waziri mkuu kwa kipindi cha miaka miwili zaidi hadi mwaka 2010 alipokabiliwa na kesi kadhaa za uhalifu. Alishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 kwa kupata zaidi ya asilimia 12 ya kura.

Akitazama mbele, Tymoshenko alikiri kwamba "nimefanya makosa," lakini alisisitiza kuhusu uadilifu wake: "Yumkini wakati mwingine nakosea, lakini nakosea kwa dhati."

"Leo tunaingia enzi mpya - enzi ya ufanisi, ya furaha, ya mwangaza," alisema. "Leo tunaanza safari ya Ukraine kuelekea ukubwa wa kweli na wa nguvu."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW

Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com