Yemen: Mashambulizi zaidi yafanywa Sanaa | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Yemen: Mashambulizi zaidi yafanywa Sanaa

Muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umefanya mashambulizi ya angani nchini Yemen mapema leo wakati ambapo wasi wa Kihouthi wakiimarisha udhibiti wao wa mji mkuu, Sanaa.

Muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umefanya mashambulizi ya angani nchini Yemen mapema leo wakati ambapo wasi wa Kihouthi wakiimarisha udhibiti wao wa mji mkuu, Sanaa, baada ya kumuua rais wa zamani, Ali Abdullah Saleh, ambaye alibadili msimamo katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe na kuiunga mkono Saudia.

Siku moja baada ya Ahmed Ali, ambaye ni mwana wa kiume wa marehemu Abdullah Saleh, kuapa kuongoza kampeni dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, Saudi Arabia na washirika wake wamefanya mashambulizi makubwa kabisa.

Hatua ya Ahmed Ali, ambaye ni kiongozi wa zamani wa kikosi maalum cha kumlinda rais, Republican Guard, na ambaye awali alitazamwa kuwa mrithi wa baba yake, inawapa wapinzani wa vuguvugu la Kihouthi uwezekano wa kuwa na uongozi mbadala baada ya wiki moja ya mapigano yaliyopelekea kutimuliwa kwa wafuasi wa Saleh kutoka mji mkuu, Sanaa.

Wito umetolewa kwa pande husika kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo

Wito umetolewa kwa pande husika kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo

Ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zimefanya mashambulizi kadhaa kulenga maeneo ya Wahouthi ndani na nje ya mji wa Sanaa na katika mikoa ya kaskazini. Kituo cha televisheni kinachoegemea upande wa Wahouthi, Al Masirah, kimesema muungano huo umeripua makaazi ya Saleh na nyumba za watu wa familia yake. Wakaazi pia wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wamesikia miripuko mikubwa mjini Sanaa. Hakukuwa na taarifa kamili kuhusu waliouawa au waliojeruhiwa.

Wito wa suluhisho kupitia mazungumzo

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema mjumbe maalum wa Umoja huo nchini Yemen,  Ismail Ould Cheikh Ahmed, ametaka pande zinazohusika katika vita hivyo kujizuia kushambuliana:

"Mjumbe maalum Ismail Sheikh amelionya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi vita hivi vinavyowaathiri raia. Ametilia uzito haja ya mazungumzo kupata suluhisho la haraka na kusisitiza kuwa mchakato wa kushirikisha kila mmoja ndio utakaoleta amani na suluhisho la kudumu kwa Wayemen."

Vita vya Yemen vimetajwa kusababisha janga baya zaidi la kibinadamu katika karne ya sasa

Vita vya Yemen vimetajwa kusababisha janga baya zaidi la kibinadamu katika karne ya sasa

Vita hivi ambavyo vinawashirikisha Wahouthi wanaosemekana kuungwana mkono na Iran na ambao wanadhibiti mji mkuu, Sanaa, dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kusaidia serikali iliyoko kusini mwa Yemen, vimesababisha kile Umoja wa Mataifa ulichokitaja kuwa janga baya zaidi la kibinaadamu.

Janga baya la kibinadamu

Umoja wa Mataifa umesema huenda mamilioni ya watu wakafariki nchini Yemen katika janga baya zaidi katika karne ya sasa ambalo limesababishwa na pande zinazopigana kuzuia usambazaji wa chakula cha misaada.

Hapo jana, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis, alisema kuuawa kwa Ali Abdullah huenda kukaibua changamoto zaidi za kibinaadamu katika hali ambayo tayari ni mbaya.

Saleh aliwasaidia Wahouthi kudhibiti sehemu kubwa ya kaskazini ya Yemen ikiwemo Sanaa, lakini hatua yake ya kubadili msimamo wiki iliyopita na kuachana na Wahouthi ilisababisha mabadiliko makubwa katika vita hivyo vya miaka kadhaa. Kwa haraka, Wahouthi waliwashambulia wafuasi wa Saleh na kumua kiongozi huyo wa muda mrefu.

Waasi hao wamekuwa wakiwashikilia zaidi ya wafanyakazi 40 wa vyombo vya habari mjini Sanaa. Kwa mujibu wa shirika la Waandishi wa Habari Wasio Mipaka, RSF, miongoni mwa waliokamatwa ni wafanyakazi wa kituo kimoja cha televisheni kinachoegemea upande wa Saleh. Shirika hilo limetaka wanahabari hao waachiwe mara moja na bila masharti.

Mwandishi: John Juma/RTRE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com