Yemen Kusini waachana na tangazo la kujitawala ili kusaka amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Yemen Kusini waachana na tangazo la kujitawala ili kusaka amani

Waasi wanaotaka kujitenga kusini mwa Yemen wamekubali kuachana na tamko lao na kujitawala na kuahidi kutekeleza makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Saudi Arabia, hatua inayoimarish vita dhidi ya waasi wa Kihouthi.

Baraza la Mpito la Kusini, STC, kundi la waasi lililokuwa limetangaza serikali yake upande wa kusini mwezi Aprili baada ya kuishutumu serikali kuu kushindwa kutekeleza majukumu yake na kupanga hujuma dhidi ya eneo hilo, sasa limeamuwa rasmi kuachana na madai yake ya kujitawala.

Tangazo la STC lililotolewa leo kupitia mtandao wa Twitter wa msemaji wake, Nizar Haitham, linasema kwamba dhamira ya kuachana na madai yake ni kutoa muda kwa pande zote kutekeleza makubaliano ya kugawana madaraka chini ya Muafaka wa Riyadh.

Nizar alikiri kwamba tangazo hilo linakuja kufuatia shinikizo kubwa kutoka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambazo ziliwataka waasi wa STC kuufuta uamuzi wao wa kujitangazia mamlaka huru.

Saudi-Arabien Riad | Einigung auf Friedensplan im Jemen (Reuters/Saudi Press Agency)

Wawakilishi wa serikali ya Yemen na Baraza la Mpito la Yemen Kusini wakisaini makubaliano ya kugawana madaraka yalioongozwa na saudi Arabia, Novemba 5, 2019.Mapema leo, Saudi Arabia ilisema ilikuwa imependekeza mpango wa kuharakisha utekelezaji wa Muafaka wa Riyadh, kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo, SPA.

Mpango huo unamtaka waziri mkuu wa Yemen kuunda serikali mpya katika kipindi cha siku 30, na pia kuteuwa gavana mpya na mkurugenzi mpya wa usalama kwa ajili ya mji wa Aden, ambako ndiko yaliko makao makuu ya serikali inayotambuliwa kimataifa, baada ya kufurushwa na Wahouthi kutoka mji mkuu, Sanaa.

Soma zaidi Wanaotaka kujitenga Yemeni wadhibiti mji wa Aden

Likimnukuu afisa wa serikali ambaye halikumtaja jina, shirika la habari la Saudi Arabia limesema mara tu baada ya hatua hiyo kutekelezwa, serikali itapaswa kuanza kazi zake mara moja ikiwa mjini Aden, na kusimamia ukamilishwaji wa kila kifungu na kipengele cha Muafaka wa Riyadh.

Tazama vidio 01:16

Vurugu Yemen

Mwanzo wa utekelezaji wa Muafaka wa Riyadh

Serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa imelipokea kwa mikono miwili tangazo hilo, ambapo msemaji wake, Rajeh Badi, ameelezea matumaini yake kwamba huu utakuwa mwanzo makini na wa kweli katika utekelezaji wa Muafaka wa Riyadh.

Rais Abdrabbo Mansour Hadi, ambaye anaishi uhamishoni mjini Riyadh, alitangaza uteuzi wa kamanda mpya wa polisi na gavana wa Aden, kando ya tangazo hilo.

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Khalid bin Salman, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba juhudi za nchi yake zimefanikisha kuzileta pamoja serikali ya Yemen na Baraza la Mpito la Kusini kwenye kukubaliana muundo uliopendekezwa katika utekelezaji wa Muafaka wa Riyadh.

Ikiwa muafaka huu utadumu, utaupa fursa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia pamoja na washirika wake kuelekeza sasa nguvu zao kwenye vita dhidi ya adui wao wa pamoja, yaani kundi la waasi la Houthi, ambalo linaungwa mkono na Iran.

Saudi-Arabien Riad | Einigung auf Friedensplan im Jemen (Reuters/Saudi Press Agency)

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed al-Nahyan (kushoto), Mrithi wa Kiti cha ufalme cha Saudi Arabia Mohammed bin Salman (kulia) na rais wa Yemen Abd-Rabb Mnsour Hadi (katikati) wakati wa kusainiwa kwa makubaliano ya kugawana mdaraka kati ya serikali na Baraza la Mpito.Kinyang'anyiro cha kuwania udhibiti wa kusini kilibainisha mgawanyiko wa wazi kati ya washirika wakuu wa muungano huo wa kijeshi - Saudi Arabia inayoiunga mkono serikali ya Abderabb Mansour Hadi, na Umoja wa Falme za Kiarabu unaoliunga mkono Baraza la Mpito la Kusini. 

Sikiliza sauti 02:40

Mahojiano na Ahmed Rajab kuhusu kubadilika kwa msimamo wa STCMuafaka huu ulisainiwa awali na Baraza la Mpito tangu mwezi Novemba mwaka jana kwa nia ya kusitisha kile kiitwacho "vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya vita vya wenyewe”, lakini tangu hapo utekelezwaji wake ulikuwa ukisuwasuwa.

Muafaka huu wa Riyadh unatazamwa kama hatua muhimu ya kuzuwia kugawanyika kwa Yemen na yumkini mwanzo wa kuelekea mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa nchi nzima.

Chanzo: AFP

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com