1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

YANGON:Waandamanaji 5 wauwawa Myanmar

26 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBMP

Taarifa zinasema kiasi cha waandamanaji watano wakiwemo watawa wawili wa kibudha wameuwawa katika mji mkuu wa Myanmar, Yangoon baada ya vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi na kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji wanaoipinga serikali ya kijeshi nchini humo na kiasi cha watu 200 nusu yao wakiwa ni watawa hao wa kibudha wamekamatwa.

Mapema hii leo wanajeshi walitumia gesi na kuwafyatulia risasi waandamanaji walioivunja amri ya kukataza maandamano iliyowekwa na serikali hapo jana.

Kufuatia hali ya mambo nchini humo suala la Myanmar limegubika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa mataifa huko Marekani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumzia juu ya mambo yalivyo nchini Myanmar alisema.

‚’Hali ilivyo nchini Myanmar na kwa muda wa miaka kadhaa sasa haki za binadamu zinavunjwa,Natoa mwito kwa utawala wa nchi hiyo kutoingilia kati maandamano hayo ili kufikia demokrasia.Watu wa Myanmar wameonyesha ujasiri dhidi ya utawala wa Kijeshi bila kutumia nyuvu na kuendelea na maandamano kwa njia ya amani.’’

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown akizungumza kwenye mkutano wa chama chake cha Labour huko Uingereza alitaka paitishwe mara moja kikao cha baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuzungumzia suala hilo na kutumwe mjumbe wa Umoja huo nchini Myanmar.Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Australia Alexander Downer amesema nchi yake haiungi mkono vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Myanmar vilivyotangazwa na rais Bush akitoa sababu kwamba vikwazo hivyo havitasuluhisha mgogoro na badala yake ni bora kutumika njia za kidiplomasia kutuliza hali ya mambo.