1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Syria auawa

Admin.WagnerD18 Julai 2012

Waziri wa ulinzi wa Syria Daoud Rajiha ameuawa katika shambulizi la kujitoa muhanga mjini Damascus. Mji huo pia unagubikwa na mapigano ya siku 4 kati ya jeshi na waasi, huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea.

https://p.dw.com/p/15ZUV
Jenerali Daoud Rajiha, waziri wa ulinzi wa Syria aliyeuawa
Jenerali Daoud Rajiha, waziri wa ulinzi wa Syria aliyeuawaPicha: Reuters

Jenerali Daoud Rajiha ameuawa katika shambulizi la kujitoa muhanga ambalo lililenga jengo la usalama wa taifa mjini Damascus. Waziri wa mambo ya ndani, mohammed al-Shaar anaripotiwa kuwa miongoni mwa waliojeruhiwa.

Shambulio hilo ni mwendelezo wa mapigano baina ya jeshi la serikali na waasi yameendelea kwa siku ya nne mfululizo katika mji mkuu wa Syria, Damascus, huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijiandaa kuupigia kura mswada ulioletwa na nchi za magharibi, ambao unataka vikwazo zaidi dhidi ya Serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Jeshi lapata hasara kubwa

Mtaa wa Damascus uliokumbwa na mapigano
Mtaa wa Damascus uliokumbwa na mapiganoPicha: picture-alliance/dpa

Wanajeshi zaidi ya 60 wa serikali ya Syria wameuawa katika mapigano ya siku tatu mjini Damascus, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria ambalo lina makao yake nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanajeshi 20 waliuawa jana Jumanne, na wengine kati ya 40 na 50 waliuawa Jumatatu. Mapema leo mapigano zaidi yameripotiwa katika sehemu mbali mbali za mji mkuu, na moshi mweusi umeonekana ukifuka kutoka sehemu hizo.

Kamati ya kuratibu shughuli za wanaharakati imearifu kuwa jeshi la serikali limeishambulia kwa mizinga mitaa ya Qaboon na Barzeh, ambako pia milio ya risasi ilisikika. Mji mkuu Damascus umeghubikwa na mapigano makali tangu Jumapili iliyopita, katika kile ambacho waasi wamekiita ''Volcano na tetemeko la ardhi mjini Damascus''.

Vita na mazungumzo

Mpatanishi Kofi Annan akizungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin
Mpatanishi Kofi Annan akizungumza na rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters

Ghasia hizo zinafanyika sambamba na juhudi za kidiplomasia, ambazo zina lengo la kuzitaka nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zifikio msimamo mmoja juu ya mzozo wa Syria. Jana, mpatanishi wa kimataifa katika mgogoro huo Kofi Annan alikutana na rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow, na kusema Mgogoro wa Syria umefika katika wakati mgumu.

Kofi Annan alisema, ''Mzozo wa Syria umefikia kiwango kibaya kabisa, na ninafurahi kwamba tumepata nafasi ya kuuzungumzia.''

Urusi, mshirika mkuu wa serikali ya rais Bashar al-Assad, imekataa kuunga mkono vikwazo dhidi ya serikali ya Syria. Akizungumza baada ya mkutano wake na Kofi Annan, rais Putin alisema nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za kurejesha amani.

''Tangu mwanzo tumekuwa tukiunga mkono juhudi ya Kofi Annan kama mpatanishi wa kimataifa katika mgogoro huu, kujaribu kuleta utulivu nchini Syria, na tutaendelea kufanya hivyo.'' Alisema rais Putin.

Leo hii rais Vladimir Putin anampokea pia waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kuzungumzia mgogoro huo huo wa Syria. Urusi na Uturuki zinatofautiana kimtazamo juu ya mgogoro huo; wakati ambapo Urusi imekataa katakata maazimio yote yenye kupendekeza vikwazo vikali dhidi ya Rais Bashar al-Assad, Uturuki imekuwa mshirika mkubwa wa makundi yanayoikosoa serikali ya Syria.

Rai kutaka muafaka

Baraza la Usalama limeganyika juu ya hatua ya kuchukuliwa nchini Syria
Baraza la Usalama limeganyika juu ya hatua ya kuchukuliwa nchini SyriaPicha: Reuters

Naye katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye yuko ziarani nchini China katika juhudi hizo hizo za kutafuta suluhu kwa mgogoro wa Syria, amelitaka Baraza la Usalama kufanya kila juhudi kukomesha umwagaji damu nchini Syria.

Baraza hilo linatazamiwa kuupigia kura mswada wa azimio uliowasilishwa na nchi za magharibi kuhusu kurefushwa kwa ujumbe wa waangalizi wa umoja huo. Mswada huo pia unataka vikwazo vikali dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad.

Duru za kidiplomasia zimesema kuwa Rais Putin ameongea na mwenzake wa China Hu Jintao, na wote wawili wamekubaliana kuupinga mswada huo. Urusi na China zina kura za turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/DPA/

Mhariri: Mohammed Khelef