Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe atangaza kujiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe atangaza kujiuzulu

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema anajiuzulu baada ya maradhi sugu yanayomsumbua kujitokeza upya. Abe amethibitisha kusumbuliwa na maradhi ya Ulcerative colitis yanayoathiri utumbo.

 

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema anajiuzulu baada ya maradhi sugu yanayomsumbua kujitokeza upya. Abe aligundulika kurudiwa na maradhi hayo kufuatia vipimo mapema mwezi uliopita wakati alipokuwa akichunguzwa afya yake kwa wiki mbili mfululizo kwenye hospitali ya jijini Tokyo.

Abe amethibitisha kusumbuliwa na maradhi ya Ulcerative colitis, yanayosababisha vidonda na uvimbe kwenye utumbo mpana tangu alipokuwa kijana mdogo na kuongeza kuwa tangu wakati huo amekuwa akipata matibabu.

Abe, ambaye awamu yake inamalizika Septemba 2021 baada ya kuhudumu kwa miaka saba na miezi minane alitarajiwa kusalia madarakani hadi pale kiongozi mpya wa chama atakapochaguliwa na kuidhinishwa rasmi na bunge.

Amesema, hali yake ilianza kudhoofika katikati ya mwezi uliopita na alianza kusikia hali ya kuchoka, lakini amesema hakutaka hali hiyo iathiri maamuzi ya kisera. Alitoa matamshi hayo, wakati akitangaza nia yake hiyo ya kujiuzulu kama kiongozi mkuu wa chama tawala cha Liberal Democratic, pamoja na uwaziri mkuu. Tangazo la Abe la kijiuzulu linatolewa siku nne tu kabla ya kutajwa rasmi kama waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Japan.

Taarifa zinasema mapema leo, waziri mkuu huyo alikutana na baraza lake la mawaziri na baadaye kukutana na waandishi wa habari kutangaza azma yake hiyo, ambayo anasema ilimuwia vigumu kuitekeleza.

Premierminister Shinzo Abe Japan Ausweitung Maßnahmen Coronavirus

Baadhi ya watawala duniani wanasema kujiuzulu kwa Abe ni pigo kwa ushirikiano na mataifa mbalimbali.

"Nilitamani kupambana na ugonjwa huu na kutibiwa na sikuwa katika hali nzuri kabisa kiafya, na bado nilitakiwa nifanye maamuzi muhimu ya kisiasa. Siwezi kufanya makosa yoyote, hasa katika kufanya maamuzi muhimu. Siwezi kufanya hivyo na niliamua kutoendelea na nafasi hii ya uwaziri mkuu." alisema Abe.

Kufuatia hatua hiyo, Korea Kusini imesema imepokea kwa masikitiko taarifa hiyo ya ghafla kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu kwenye mahusiano baina ya mataifa hayo. Msemaji wa makazi ya rais ya Blue House Kang Min-seok amesema kupitia taarifa yake na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo.

Urusi nayo imesema imepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, na kwamba alikuwa kiongozi aliyependa ushirikiano, huku waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akisema Abe ni kiongozi aliyefanikisha mambo makubwa.

Mwaka 2012, wakati Abe alipoingia mamlakani aliapa kuuimarisha upya uchumi wa taifa hilo, chini ya sera ambayo ilipewa jina la utani "Abenomics". Ingawa alifanikiwa kuiondoa Japan kwenye mdororo, lakini uchumi wa taifa hilo umeathiriwa upya na virusi vya corona. Aidha, waziri mkuu huyo ameshindwa kutimiza lengo alilotamani la kuandika upya katiba iliyotayarishwa na Marekani inayopinga matumizi ya vita kama mbinu ya kutatua migogoro ya kimataifa inayolihusu taifa kufuatia uungwaji mkono mdogo wa umma.

Soma Zaidi: Trump kuitumia Japan katika mazungumzo na Iran

Mashirika: APE/RTRE/AFPE