1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Italia atangaza kujiuzulu

Grace Kabogo
5 Desemba 2016

Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi amesema atajiuzulu, baada ya kushindwa katika kura ya maoni iliyofanyika jana Jumapili, kuhusu mapendekezo yake ya kuifanyika mageuzi katiba ya nchi hiyo. 

https://p.dw.com/p/2TjWw
Italien | Ministerpräsident Matteo Renzi kündigt nach gescheitertem Referendum seinen Rücktritt an
Picha: REUTERS/A. Bianchi

Akilihutubia taifa kupitia televisheni baada ya matokeo ya awali kutangazwa, Renzi amesema majukumu ya serikali yake yamemalizika leo na kwamba anawajibika kikamilifu kwa kushindwa. ''Leo demokrasia ya Italia inazingatia mfumo wa bunge. Nasikitika inanibidi niondoke bila kujutia chochote, kwa sababu demokrasia imeshinda na kambi ya 'Hapana' imeshinda. Pia ni ukweli kwamba tumepambana vizuri kwa shauku kubwa na uamuzi. Kitu ambacho kilikuwa dhahiri tangu siku ya kwanza. Uzoefu wangu unaishia hapa,'' alisema Renzi.

Renzi amesema hawezi kuyapinga matokeo ya kura hiyo ya maoni ambayo yako wazi na amewataka wapinzani wake kutoa mapendekezo imara na mwelekeo ulio wa wazi kwa ajili ya kumaliza mzunguko wa mkwamo wa kisiasa nchini Italia. Matokeo hayo yanaonyesha kambi yake ya kura ya 'Ndiyo' imeshindwa katika uchaguzi huo kwa kupata kati ya asilimia 42 na 46, huku kambi ya 'Hapana' inayoongozwa na Vuguvugu la Nyota Tano-M5S, ambalo linapinga sera za wahamiaji, ikiwa imepata asilimia 59.5 ya kura.

Symbolbild | Italien nach Referendum
Moja ya mitaa ya jiji la RomaPicha: Getty Images/G. Cosulich

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani, asilimia 70 ya watu wanaoruhusiwa kupiga kura walijitokeza katika vituo vya kupigia kura. Renzi amewapa pole wale wote waliokuwa kwenye kambi ya 'Ndiyo' na amewapongeza kwa kampeni nzuri waliyoifanya. Renzi ambaye amekuwa Waziri Mkuu wa Italia kwa muda wa miaka miwili na nusu, amesema leo mchana atakuwa na kikao cha mwisho na baraza lake la mawaziri na kisha atawasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Sergio Mattarella.

Mageuzi aliyoyataka Renzi

Mageuzi yaliyokuwa yanapiganiwa na Renzi na chama chake cha mrengo wa kati-kushoto cha Democratic, ni pamoja na kufanyika mageuzi kadhaa katika serikali, kurahisisha mfumo wa utendaji, kupunguza gharama za siasa, kupunguza idadi ya wawakilishi katika bunge la Senate pamoja na kumuongezea rais madaraka katika serikali.

Italien Five Star Bewegung vor dem Referendum
Wanachama wa Vuguvugu la Nyota Tano walioongoza kambi ya 'Hapana'Picha: DW/M. Williams

Kiongozi wa upinzani Matteo Salvini wa chama cha Northern League ambacho kinapinga sera za wahamiaji na aliyeongoza kambi ya 'Hapana', ameyataja matokeo hayo kama ushindi wa watu dhidi ya nguvu zinazodhibiti robo tatu ya dunia. Meya wa Roma, Virginia Raggi na mwanasiasa wa vuguvugu la M5S, amesema Wataliano wameshinda na hawatoacha mapinduzi yao na kwamba sasa ni muda wa kuijenga upya Italia.

Vyama vingine vya mrengo mkali wa kulia vimeyafurahia matokeo hayo ya kura ya maoni, akiwemo kiongozi wa chama cha National Front nchini Ufaransa, Marine Le Pen. Mara baada ya matokeo kutangazwa, Le Pen aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Twitter kwamba Wataliano wamejitenga na Umoja wa Ulaya pamoja na Renzi.

Wakati huo huo, sarafu ya Euro ilishuka thamani mara baada ya Renzi kutangaza kujiuzulu. Sarafu hiyo imeshuka hadi Dola 1.0506 katika soko la hisa la Tokyo, kutoka Dola 1.0664 Ijumaa jioni, ikiwa ni kiwango cha chini kabisa tangu Machi 2015.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DPA
Mhariri: Daniel Gakuba