Waziri Heiko Maas alitembelea bara la Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 03.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Waziri Heiko Maas alitembelea bara la Afrika

Baada ya mwaka wa Afrika 2017 sera ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika imepwaya. Maas anataka kufanya mazungumzo Afrika na anazitembelea Ethiopia na Tanzania.

Kanada - G7 Toronto | Bundesaußenminister Heiko Maas gibt ein Pressestatement (Imago/photothek/T. Trutschel)

Heiko Maas, waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko Maas ameanza ziara yake barani Afrika. Maas anaanza ziara yake nchini Ethiopia na baadaye kuelekea nchini Tanzania.

Wiki sita tu tangu alipochukua wadhiwa wa waziri wa mambo ya nchi za nje, Heiko Maas anafanya ziara yake ya kwanza katika bara jirani na Ulaya, akizitembelea Ethiopia na Tanzania, ambazo zimeendelea kuwa na ushirikiano wa karibu sana na Ujerumani kihistoria na hata kisiasa.

Nchi hizo mbili ni muhimu katika Umoja wa Afrika na vile vile katika jumuiya ya Afrika Mashariki na wakati huo huo zimekabiliwa na changamoto. Ethiopia ingeweza kung'ara kama taifa lenye ukuaji uchumi lakini limegonga vichwa vya habari kutokana na visa vya ukandamizaji wa haki za binadamu. Rais wa Tanzania John Magufuli alionekana kuanza vyema uongozi wake lakini sasa mkondo umebadilika huku uhuru wa kisiasa ukibanwa.

Hamasa kuhusu bara la Afrika mjini Berlin imepungua

Kisiasa mjini Berlin hali imekuwa tulivu kuhusu bara la Afrika. Mwaka uliopita kulitangazwa mpango kabambe wa kuisaidia Afrika, bara hilo likawa kauli mbiu ya urais wa Ujerumani wa kundi la mataifa ya G20 lakini hakuna mengi yaliyofanikishwa.

Dr. Abiy Ahmed (DW/S. Teshome )

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Mohammed

Mtaalamu wa masuala ya Afrika kutoka chuo kikuu cha Mainz Helmut Asche aliiambia DW kuwa, "Mwaka 2017 kulikuwa na mambo mengi kuhusu Afrika, pengine hata mengi mno kwa siasa na Berlin. Mada hii tumeibeba hadi mwaka uliofuata, ingawa mtu anaweza kusema utekelezaji wake hata kwa upande w aa Ujerumani hakuna mengi yaliyotokea kama tulivyodhamiria."

Sio mpango wa waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Gerhard Müller, al maarufu Marshall Plan, wala ule wa mpambe wa waziri Maas, mwanachama mwenzake katika chama cha Social Democratic, SPD, Brigitte Zypries, mradi wa Pro Afrika, uliofaulu kuwashawiswhi wakosoaji. Hamasa kuhusu bara la Afrika mjini Berlin imeyeyuka kwa mujibu wa kauli za wakosoaji.

Stefan Liebing, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara na makampuni ya Ujerumani barani Afrika alisema, "Kuna matarajio makubwa yaliyochomoza kutoka kwa marafiki zetu barani Afrika baada ya kutangazw amiradi mingi, na sisi hapa Ujerumani tunahisi, na nadhani ndivyo ilivyo barani Afrika, kwamba hakuna lolote lililotekelezwa."

Wasiwasi wajitokeza Tanzania

Ujumbe unaotoka Berlin kwa nchi zilizopiga hatua katika kufanya mageuzi barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara sio mataifa kusimama peke yao kama taifa moja moja, bali miungano ya kikanda ndio ufunguo wa maendeleo na uthabiti.

Hali ya wasiwasi imejitokeza katika ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania. Rais John Magufuli aliyechaguliwa mwishoni mwa mwaka 2015, na kuanza vyema kuleta nidhamu katika afisi za umma na kuanzisha vita dhidi ya rushwa na vita vya uchumi, sasa kunashuhudiwa waandishiwa habari, wanasiasa wa upinzani, wamiliki wa blogu na hata viongozi wa makanisa wakiandamwa.

Tansania - Präsident John Magufuli (picture alliance/AA/M. Mukami)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli

Mtaalamu wa masuala ya Afrika wa chuo kikuu cha Mainz, Helmut Asche alisema, "Kwa namna hiyo mtu anaweza kujidanganya mwenyewe. Tulikuwa na matumaini makubwa kwamba Magufuli kwamba angesaidia kulainisha uwajibikaji na kupambana na rushwa. Lakini sera ya mageuzi imegeuka kuwa ukandamizaji na mwenendo wa kisiasa usiokubalika."

Arsche aidha alisema sasa pana haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu mfumo wa kisiasa wa Tanzania na demokrasia, mambo ambayo yamekuwa thabiti katika muongo mmoja uliopita, na kutafakari njia za kutafuta ufumbuzi.

Upepo wa mageuzi waleta matumaini Ethiopia

Nchini Ethiopia kunavuma upepo wa mageuzi. Waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, Abiy Ahmed, ametangaza mageuzi kadhaa katika siku zake za kwanza madarakani, ambayo yameleta matumaini makubwa katika taifa hilo linaloshikilia nafasi ya pili kwa idadi ya wakazi barani Afrika, likiwa na jumla ya wakazi milioni 100, wengi wao wakiwa vijana.

Mtaalamu wa masuala ya Afrika kutoka chuo kikuu cha Mainz, Helmut Asche, aliiambia DW kwamba lingekuwa jambo zuri na la busara kwa waziri Heiko Maas kuzungumza na waziri mkuu Abiy, kwa kuwa mabadiliko ya uongozi Ethiopia yanaweza kuwa muhimu katika kuboresha hali ya mambo nchini humo.

Ziara ya Heiko Maas barani Afrika haiwekewi matumaini makubwa. Stefan Liebing, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara na makampuni ya Ujerumani barani Afrika alisema waziri Heiko Maas anatakiwa kukaa na wenzake serikalini kutafakari ni vipi mipango mingi ya kuisaidia Afrika inavyoweza kutekelezwa.

Mwandishi: Schadomsky, Ludger (HA Afrika)

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com