Waukraine wamchaguwa tajiri kunusuru nchi | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waukraine wamchaguwa tajiri kunusuru nchi

Matokeo ya awali katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Ukraine yamedokeza kuchaguliwa kwa tajiri mkubwa wa viwanda vya chokoleti Petro Poroshenko kuwa rais wa nchi hiyo na kuitowa nchi yake kwenye mzozo.

Petro Poroshenko akizungumza mjini Kiev. (25.05.2014)

Petro Poroshenko akizungumza mjini Kiev. (25.05.2014)

Petro Poroshenko akijitangazia ushindi muda mfupi baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Ukraine hapo jana kuonyesha kwamba alikuwa akiongoza kwa wingi wa kura,ameapa kukomesha vita,machafuko, uhalifu na kuleta amani katika nchi yake iliogawika vibaya. Anaunga mkono kuwepo kwa uhusiano madhubuti na Ulaya lakini pia anataka kurekebisha uhusiano na Urusi.

Amesema hatua zake za mwanzo akiwa kama rais itakuwa ni kuzuru eneo la viwanda la Donbass lilioko mashariki mwa Ukraine ambapo waasi wanaotaka kujitenga wanoiunga mkono Urusi wamenyakuwa majengo ya serikali na kupambana na vikosi vya serikali katika mapigano yaliodumu kwa wiki kadhaa.Poroshenko pia amesema kwamba serikali ya Ukraine ingelipenda kuzungumzia mkataba mpya wa usalama na Urusi.

Tume ya uchaguzi imesema takriban asilimia 60 ya watu milioni 35.5 wanaostahiki kupiga kura wamejitokeza katika uchaguzi huo hapo jana Jumapili ambapo kulikuwepo na misururu mirefu katika vituo vya kupigia kura katika mjii mkuu wa Kiev.

Wakati asilimia hamsini ya kura zikiwa tayari zimehesabiwa kufikia mapema leo hii Poroshenko alikuwa akiongoza kwa kama asilimia 56 wakati Julia Tymoshenko akishika nafasi ya pili kwa kujipatia asilimia 13 ya kura,iwapo hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati matokeo rasmi yatakapokuwa yametangazwa Poroshenko ataepuka marudio ya uchaguzi na mgombea aliemkaribia anayeshika nafasi ya pili.

Uwanja wa ndege Donetsk wafungwa

Gari la kijeshi lenye wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi likielekea uwanja wa ndege wa Donetsk (26.05.2014).

Gari la kijeshi lenye wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi likielekea uwanja wa ndege wa Donetsk (26.05.2014).

Watu wenye silaha leo wamelazimisha kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Donetsk mashariki mwa Ukraine baada ya hapo jana kuzuwiya sehemu kubwa ya wapiga kura kutoka eneo hilo kushiriki katika uchaguzi huo wa rais.

Mapema mwezi huu waasi wanaoiunga mkono Urusi wamejitangazia kuwa "jamhuri za wananchi" kwa majimbo ya Donetsk na Luhansk baada ya kuwa na kile walichokiita kura ya maoni.Wamesema majimbo hayo mawili likiwemo eneo la migodi ya makaa ya mawe la Donbass sio tena sehemu ya Ukraine.

Ni kama asilimia 20 ya vituo vya kupigia kura katika eneo hilo viliweza kufanya kazi hapo jana na wapiga kura wengi walibaki majumbani mwao kwa kuhofia usalama wao.Hakuna kituo chochote cha kupigia kura kilichofunguliwa katika mji wa Donetsk wenye wakaazi milioni moja.

Mazungumzo na wakaaazi wa mashariki

Waasi wanaoiunga mkono Urusi wakizungumza na wakaazi wa Donetsk. (25.05.2014)

Waasi wanaoiunga mkono Urusi wakizungumza na wakaazi wa Donetsk. (25.05.2014)

Akizungumza baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo Poroshenko ameahidi kuwa na mazungumzo na wakaazi wa mashariki ya Ukraine na kuwahakikishia haki zao ikiwa ni pamoja na zile za kuzungumza Kirusi.Pia amesema yuko tayari kutowa msamaha kwa wale ambao hawakujihusisha na matumizi ya silaha.

Amesema "Kwa wale wanaouwa watu,hao ni magaidi na hakuna nchi duniani inayofanya mazungumzo na magaidi."

Uchaguzi huo ambao unbakuja miezi mitatu baada ya Rais Viktor Yanukovych aliyekuwa akiiunga mkono Urusi kutimuliwa madarakani na umma uliokuwa ukiandamana barabarani kumpinga kwa miezi kadhaa unaonekana kuwa hatua muhimu katika kuutatuwa mzozo wa muda mrefu wa Ukraine.

Urusi imesema iko tayari kushirikiana na rais mpya aliyechaguliwa Ukraine.Rais Barack Obama wa Marekani amewapongeza wananchi wa Ukraine kwa kushiriki katika uchaguzi huo licha ya vitendo vya uchokozi na ghasia mashariki mwa nchi hiyo.

Mwandishi : AP/AFP/Reuters

Mhariri :Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com