Watu kadhaa wauwawa kwenye ghasia nchini Kenya | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 31.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Watu kadhaa wauwawa kwenye ghasia nchini Kenya

Watu wasiopungua 18 wameuwawa magharibi mwa Kenya katika ngome ya chama cha upinzani cha ODM

Maafisa wa polisi wakabiliana na wafuasi wa chama cha ODM kwenye machafuko yaliyozuka baada ya rais Kibaki kutangazwa mshindi

Maafisa wa polisi wakabiliana na wafuasi wa chama cha ODM kwenye machafuko yaliyozuka baada ya rais Kibaki kutangazwa mshindi

Ghasia na machafuko yanaendelea katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kufuatia hatua ya tume huru ya uchaguzi kumtangaza mgombea wa chama cha PNU, rais Mwai Kibaki, kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika nchini humo Alhamisi iliyopita.

Rais Kibaki aliapishwa muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, hatua ambayo imesababisha wafuasi wa mgombea kiti cha rais wa chama cha ODM, bwana Raila Odinga, kuanza kufanya fujo katika mtaa wa mabanda wa Kibera, wakiamini kumekuwa na udanganyifu katika matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo.

Watu kadhaa wamepigwa risasi katika mitaa ya madongo poromoka ya mjini Nairobi asubuhi ya leo wakati maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia walipokabiliana na waandamanaji wanaopinga ushindi wa rais Kibaki.

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, ameapa kukaidi marufuku ya serikali na kuapa atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Uhuru Park mjini Nairobi. Bwana Odinga anaamini amepokonywa ushindi wake na tume ya uchaguzi

Huko magharibi mwa Kenya, watu takriban 20 wameuwawa usiku wa kuamkia leo. Duru za polisi zinasema watu saba walipigwa risasi na kuuwawa mjini Kisumu, ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga. Wengine saba wameuwawa mjini Nakuru katika machafuko ambayo polisi wameyaelezea kuwa kati ya makabila mawili yanayohasimiana kisiasa. Watu wengine wanne wameuwawa kwenye machafuko mengine yalitokea katika kijiji kimoja karibu na mji wa Kapsabet.

Wakati haya yakiarifiwa, serikali ya Kenya imepiga marufuku matangazo yote ya moja kwa moja ya redio na televisheni kuhusu matokeo yanayoendelea nchini humo kufuatia kutangazwa kwa rais Mwai Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu dhidi ya mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.

 • Tarehe 31.12.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CiOl
 • Tarehe 31.12.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CiOl
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com