1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 65 wauawa katika shambulizi la itikadi kali Nigeria

Bruce Amani
29 Julai 2019

Kiasi cha watu 65 wameuawa katika shambulizi linalodaiwa kufanywa na wanamgambo wa itikadi kali dhidi kikundi cha waombolezaji waliokuwa wakitoka matangani katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

https://p.dw.com/p/3MsXp
Nigeria 65 Menschen von Islamisten der Gruppe Boko Haram getötet
Picha: AFP/A. Marte

Hakujawa na kauli yoyote ya kudai kuhusika na shambulizi hilo, lakini kundi la Boko Haram na kundi pinzani la Dola la Kiislamu tawi la Afrika Magharibi ISWA aghalabu hufanya mashambulizi katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa serikali ya eneo hilo Mohammed Bulama amenukuliwa na televisheni ya taifa akisema kuwa washambuliaji waliwauwa watu 21 waliokuwa njiani kutoka matangani Jumamosi, na wengine 44 wakauawa wakati wakijaribu kujipanga upya ili kujilinda. Wengine walijeruhiwa, kumaanisha kuwa idadi ya vifo huenda ikapanda."Wakati wa mazishi, waliwashambulia katika eneo la makaburi. mara moja wakawauwa watu 21. Baadaye, wakati watu waliobaki walisikia habari hizo, nao wakaenda kuwakabili. Majihadi wakawauwa. Hiyo inafikisha idadi ya waliouawa kufika 65."

Bulama amesema mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi baada ya wanakijiji na makundi ya ulinzi wa raia kupambana kuzuia shambulizi la Boko Haram katika eneo hilo wiki mbili zilizopita na kuwauwa wapiganaji 11

Nigeria 65 Menschen von Islamisten der Gruppe Boko Haram getötet
Shambulizi lilifanywa dhidi ya waombolezajiPicha: AFP/A. Marte

Rais Muhammadu Buhari amelaani shambulizi hilo na kuliamuru jeshi kuwawinda watuhumiwa. Jimbo la Borno ni kitovu cha uasi wa Boko Haram na ISWA.

Mzozo huo umedumu kwa muongo mmoja, ambapo wanamgambo wamewauwa maelfu ya watu na mamilioni kukimbia makwao katika eneo hilo. Mkaazi mmoja kwa jina Bakura Mallam Amadu ameema aliwaona wanamgambo hao wakikusanyika kabla ya kuanza kufyatua risasi dhidi ya waombolezaji. Duru ya usalama imesema wapiganaji hao walishambulia wakiwa kwenye pikipiki na magari. Jeshi la Nigeria limekataa kuzungumzia tukio hilo.

Wakati huo huo, serikali ya Nigeria imepiga marufuku kundi la Waislamu wa Shia ambalo wafuasi wake wamekuwa wakiandamana kudai kuachiwa huru kwa kiongozi wao anayezuiliwa. Serikali inalituhumu kundi hilo kwa kuchochea machafuko.

Kiasi ya wanachama 20 wa Vuguvugu la Kiislamu nchini Nigeria wameuawa katika kipindi cha wiki moja iliyopita kufuatia wimbi la maandamano ambayo hayaonyeshi dalili za kusitishwa, na hivyo kuongezea serikali mbinyo. Wanachama wa kundi hilo, ambalo ndilo kubwa kabisa la Kishia nchini Nigeria, wamekuwa wakifanya maandamano mjini Abuja, kutaka aachiwe huru kiongozi wao Ibrahim Zakzaky, ambaye amekuwa kizuizini tangu 2015 licha ya amri ya mahakama ya kutaka aachiwe huru.